TAHARIRI: Ukaidi wa Tanzania tishio kwa eneo zima
Na MHARIRI
TANGU kuzuka kwa janga la korona katika pembe mbalimbali za dunia, serikali ziliamua kuchukua hatua madhubuti kudhibiti msambao wa maradhi ya Covid-19.
Mataifa haya yalichukua hatua baada ya kupokea ushauri kutoka kwa Shirika la Afya Duniani.
Mengi ya mataifa yaliyochukua hatua za mapema kupiga marufuku safari za ndege kuingia na kutoka nchini mwao yalipata maambukizi machache mno. Iwapo hatua hii ilifuatiwa na kuanzishwa kwa hamasisho kwa wananchi kuhusu namna ya kuepuka maambukizi ya korona, basi nchi hizi hadi leo hazijaandikisha visa vingi vya maambukizi.
Takwimu pia zimeonyesha kwamba baadhi ya mataifa yaliyochukua hatua za tahadhari mapema hiyo kisha baadaye yakalegeza masharti yalipata awamu ya pili ya maambukizi. Baadhi ya mataifa haya ya ughaibuni yalilemewa katika juhudi za kuwahudumia wagonjwa. Hospitali zilijaa wagonjwa na wahudumu wa afya ama kuzidiwa kazi. Matokeo yalikuwa kuaga dunia kwa wengi wa wagonjwa.
Matukio haya yanafaa kuwa funzo kwa mataifa yetu ya Afrika Mashariki na Kati. Hasa ikizingatiwa kwamba mengi ya mataifa ya Afrika ni maskini na yana miundomsingi ya afya iliyo dhaifu, tunafaa kuchukua hatua madhubuti zaidi kama njia ya kudhibiti maambukizi ya korona la sivyo tutabwagwa.
Ni katika muktadha huu ambapo mvutano unaoendelea kati ya Kenya na Tanzania unakuwa tishio kubwa kwa ukanda mzima. Baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuchukua hatua ya kufunga mipaka ya Kenya na mataifa ya Somalia na Tanzania, hali haijakuwa hali.
Kenya ilichukua hatua hii baada ya kubaini kwamba wengi wa raia kutoka Tanzania wanaotangamana na majirani zao Wakenya mipakani ni waathiriwa wa korona.
Isitoshe, kufikia Jumanne, Kenya ilitangaza kwamba iliwazuia madereva 126 wa Tanzania kuingia nchini baada ya kuwapima na kubaini kwamba walikuwa waathiriwa wa korona.
Tanzania ilihisi kudhulumiwa na hatua ya Kenya na ilichofanya ni kuzuia malori kutoka Kenya kuingia nchini kwao. Hata hivyo, Kenya kwa upande wake haijazuia malori ya mizigo kutoka Tanzania kuingia humu nchini.
Tanzania ilichukua hatua hii kwa hasira bila kujali athari zake. Tanzania inafaa kuwajibika na kuacha utepetevu wa namna inavyoshughulikia janga la korona la sivyo si nchi hiyo tu itaumia bali ukanda mzima wa Afrika Mashariki. Hakuna ubabe katika kulikabili janga linalotukumba kwa sasa, ipo haja kubwa ya kushirikiana.