TAHARIRI: Usalama wa wanafunzi uzingatiwe mno shuleni
KITENGO CHA UHARIRI
KIINI cha maandamano ya wanafunzi, na hatimaye kufungwa kwa Shule ya Upili ya Lugulu Girls, kinatokana na madai kuwa mwanafunzi mmoja alinajisiwa.
Madai kwamba wasimamizi wa shule walitaka kuficha uovu huo unapaswa kukashifiwa kwa kinywa kipana, na iwapo uchunguzi utabainisha kwamba kweli yalitokea basi mkondo wa sheria ufuatwe.
Wakuu wa shule hawafai kunyamazia ukatili kama huo katika shule zao. Mwalimu Mkuu katika shule yoyote ile ni kama dereva wa gari lenye abiria; chombo kinapoenda mrama wa kulaumiwa ni yeye tu, kwani inatarajiwa kuwa mafunzo aliyopata mwalimu yanajumuisha umakinifu wa kuhakikisha maisha ya wasomi yanaendelea vema.
Mwalimu mkuu anapaswa kuziba mianya yoyote ya uhalifu dhidi ya wanafunzi na watu wote wanaohudumu shuleni mwake.
Tukio la Lugulu Girls sio kisa cha pekee kwani hapo awali kulitokea kadhia kama hiyo katika Shule ya Wasichana ya Moi mjini Nairobi.
Suala hili halipaswi kuzingatiwa tu kama uhalifu, lakini wito wa kufanya ukaguzi wa kina kuhusu usalama wa wanafunzi shuleni.
Katika siku za hapo nyuma, kulikuwa na visa vya wasichana wa shule kudhulumiwa na hata kuuawa. Kwa mfano mnamo 1991, wasichana 19 waliuawa na wengine 71 kubakwa na wenzao wa kiume katika Shule ya Sekondari ya St Kizito huko Meru.
Kwa bahati mbaya, Wizara ya Elimu na serikali ilionekana kutojifunza chochote kutokana na visa hivi.
Baada ya shambulio la St Kizito, mengi yalizungumzwa kuhusu njia ya kuwalinda wasichana shuleni. Mapendekezo yalifanywa, ikiwemo kuwataka walimu wakuu na manaibu wao waishi ndani ya shule zote za bweni. Ilipendekezwa pia kwamba shule ziwekwe ua la mawe kuzizingira na ziwe na walinzi.
Kulikuwa na mazungumzo mengi wakati huo jinsi ya kuwalinda wanafunzi katika shule za bweni, iwe ni wavulana au wasichana. Shule, iwe ya bweni au ya kutwa, inapaswa kuwa salama kwa wanafunzi na walimu.
Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), hakuna mwanafunzi, mwanamume au mwanamke anayepaswa kufanya vurugu zozote au kuhatarisha maisha yao wakati wanapata elimu katika nchi yoyote.
“Serikali zinahimizwa kuhakikisha shule ni mahali ambapo watoto wanahisi kuwa huru na kulindwa,” inasema UNESCO.