Makala

TAHARIRI: Ushuru wa mafuta utumiwe ipasavyo

July 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MHARIRI

WAKENYA Jumatano walianza kutozwa bei za juu za mafuta, wakati huu ambapo wanapambana kujikimu kufuatia athari za janga la corona.

Mojawapo ya sababu zilizotolewa na Halmashauri ya Kawi na Bidhaa za Petroli (EPRA), ni kwamba kupanda huko kumesababishwa na Kodi ya Maendeleo, yaani Petroleum Development Levy. Kodi hiyo imepanda kutoka senti 40 hadi Sh5.40.

Kupandishwa kwa kodi kunajiri chini ya mwaka mmoja tangu Bunge lilipokataa Ushuru wa Mafuta, uliotaka kutoza bidhaa za mafuta kodi ya asilimia nane. Kupandishwa kwa ushuru wa sasa ni zaidi ya asilimia 1,000, jambo ambalo halifai kuruhusiwa bila ya Wakenya kuketi chini na kulijadili.

Lengo la kutoza Petroleum Development Levy ni kuwezesha kuwepo maendeleo ya ustawishaji wa barabara, mabomba ya mafuta miongoni mwa maendeleo mengine.

Wakati huu ambapo sekta karibu zote za uchumi zimesambaratishwa na janga la corona, mafuta ni bidhaa muhimu inayotegemewa.

Kupanda kwa mafuta mara nyingi hupandisha bei za bidhaa zinazotegemewa na wananchi mashinani au walio mjini lakini hawana kibarua cha kuwapa riziki.

Alipokuwa akitangaza baadhi ya mikakati ya kumwepushia mwananchi ugumu wa maisha kutokana na janga la corona, Rais Uhuru Kenyatta aliagiza hata kampuni ya nguvu za umeme ya Kenya Power (KPLC) iwape muda wananchi walipe bili zao pole pole. Bili za baadhi ya watu tayari zinaonekana kuwa za kupanda kuliko kawaida, ilhali wafanyikazi wa Kenya Power hawajawahi kutembelea nyumba za watu na kusoma mita.

Serikali huwa ndilo kimbilio kwa mwananchi. Inatarajiwa kuwa, sera zake na maamuzi yanayowahusu raia huwa yamejadiliwa. Lakini katika kuongeza ushuru wa mafuta, ni wazi kwamba uamuzi huo ulifanywa haraka bila kuzingatia namna ambavyo mwananchi atazidi kuteseka.

Mafuta ya petroli hayatumiwi na wanaomiliki magari pekee. Viwanda na hata kampuni ya kuzalisha umeme hutumia mafuta hayo. Gharama ya juu kawaida hulimbikiziwa mwananchi, ambaye ni mteja wa huduma na bidhaa hizo. Si vibaya kwa serikali kutafuta fedha za ziada za maendeleo. Kisichofaa ni kuongeza ushuru zaidi ya mara 1,000 wakati ambapo ulimwengu mzima unapitia kipindi kigumu kiuchumi. Pesa hizi za ziada zinazokusanywa, itabidi maendeleo zitakayofanya, yaonekane na wananchi.