• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
TAHARIRI: Utata wa Huduma Namba utatuliwe

TAHARIRI: Utata wa Huduma Namba utatuliwe

KITENGO CHA UHARIRI

SASA ni rasmi kuwa Kenya imeanza safari mpya kuhusu vitambulisho vya raia.

Hatua ya serikali kutangaza jana kuwa vitambulisho vinavyotumika sasa vitakoma kuwa halali mwishoni mwa mwaka ujao, ni tangazo kubwa ambalo bila shaka limeibua msisimko miongoni mwa wananchi wengi.

Safari ya utekelezaji wa utumizi wa kadi za Huduma Namba imekuwa ndefu na yenye misukosuko mingi. Kufikia sasa, bado kuna idadi kubwa ya wananchi ambao wanatilia shaka uaminifu wa serikali katika Huduma Namba.

Kwa mtazamo wao, huenda kuna nia fiche ambayo serikali inalenga, ikiwemo kutumia vibaya data zilizokusanywa kutoka kwa umma.

Ni wajibu wa serikali sasa kuweka mikakati ya kuwashawishi wananchi kwamba Huduma Namba haina nia fiche.

Huenda itakuwa ni changamoto kwa vile tayari baadhi ya wanasiasa washaingilia mdahalo huo na kudai mpango ni kuiba kura ifikapo mwaka wa 2022.

Kinachowatia hofu ni kwamba huu ni mpango ambao ulisajili pia watoto wenye umri wa chini ya miaka 18 ambao kisheria hawaruhusiwi kupiga kura. Madai haya yote, ijapokuwa hayajathibitishwa ipasavyo, yanaweza kuibua wasiwasi miongoni mwa wananchi.

Serikali imekuwa ikisisitiza kwamba haina nia fiche katika mpango mzima wa Huduma Namba. Msimamo wake ni kuwa, mpango huo ni sawa na uliotekelezwa katika mataifa mengine yaliyoendelea ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi na vile vile kuboresha usalama kwa kutambua raia wote wa nchi kwa urahisi.

Wakati serikali iliposhtakiwa mahakamani kuhusu Huduma Namba, kuna mambo kadha ambayo korti iliagiza yafanywe ndipo mpango mzima uwe halali.

Ni matumaini yetu kuwa mambo yote yaliyoagizwa mahakamani, ikiwemo kupitishwa kwa sheria zinazohitajika, yamefanikishwa kikamilifu sasa. Kama Huduma Namba ni mpango mwema, huu ndio wakati mwafaka wa serikali kufafanua mambo yote ambayo yaliibua utata.

Tunafahamu kuwa mamilioni ya Wakenya walijisajili kupokea kadi hizo, lakini hiki kisiwe kisingizio kwa serikali kukaa kimya wakati wengine wachache wanapolalamika.

You can share this post!

Salim Babu apokezwa mikoba ya Kisumu All Stars baada ya...

NGILA: Nchi za Afrika ziungane kufaidika kiteknolojia