TAHARIRI: Vijana hawahitaji maneno matupu
Na MHARIRI
KENYA Jumatano iliungana na mataifa mengine ulimwenguni kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Vijana.
Maadhimisho hayo yalishuhudia sifa kochokocho kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu uwezo wa vijana kuleta mabadiliko katika nchi hii.
Sifa hizo si mpya kwani vijana wamekuwa wakipakwa mafuta kwa tako la chupa kwa miongo mingi. Licha ya kujaribu kujikakamua ili wajikwamue katika hali ngumu zinazowakumba kimaisha, wengi hugonga mwamba kwa sababu nchi haina nafasi bora kwa watu wengi wanaotaka kutegemea jasho lao.
Katika ulingo wa kibiashara, utakuta vijana wakiahidiwa watapewa kandarasi serikalini ili kuwainua, lakini nafasi inapotokea, kandarasi zinaenda kwa wakongwe au vijana walio na uhusiano wa karibu na watu mashuhuri serikalini.
Mtindo huu wa kujuana ndio pia hutumiwa kujaza nafasi za kazi, sio serikalini pekee bali pia katika baadhi ya mashirika ya kibinafsi. Aina hii ya ufisadi imefanywa kuwa jambo la kawaida kwa kiwango kuwa, utasikia vijana wakilaumiwa kwa ‘kutojua watu’ wakati wanaposhindwa kufanikiwa maishani.
Vijana katika nchi ya Kenya wamethibitisha wana uwezo wa kufanya mambo makuu wakipewa nafasi kwa njia ya haki, lakini wengi hubaguliwa na kuishia kufanya vibarua ambavyo havifai kwa watu wa tajiriba zao.
Ukabila na aina nyingine za ubaguzi zimefanya nchi kuwa na watu wasio na uwezo wa kuhudumia umma huku wale wenye uwezo wakiachwa nje.
Haitoshi kusifu vijana kwa uwezo wao kila kukicha. Kinachohitajika ni utekelezaji bora wa sera zilizopo zinazonuia kuwakwamua vijana kutoka kwa changamoto zinazowakumba, hasa ukosefu wa ajira.
Tafiti zimeonyesha kuwa, ukosefu wa mbinu za kujitafutia riziki miongoni mwa vijana ni chanzo cha maovu mengi ambayo yanakumba taifa ikiwemo ugaidi na ulanguzi wa mihadarati.
Wahalifu sugu wakongwe wamepata mwanya wa kuendeleza na kukuza biashara zao haramu kwa vile kuna mamia ya maelfu ya vijana ambao wako hiari kujitolea mhanga kwa jambo lolote lile mradi tu wapate riziki yao ya kila siku.
Ni lazima serikali na jamii yote kwa jumla itambue kuwa kuna umuhimu wa kuboresha maisha ya vijana ikiwa tunataka kuokoa nchi hii kutokana na matatizo yanayoikumba.