Makala

TAHARIRI: Wabunge wafahamu mswada hauepukiki

December 1st, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA MHARIRI

WABUNGE  kwa mara ya tatu juzi waliahirisha kupitisha mswada wa usawa wa kijinsia. Kiongozi wa Wengi Bungeni Aden Duale aliahirisha mswada huo akisema bado haukuwa na idadi ya kutosha ya uungwaji.

Juhudi za Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto kupigia debe mswada huo, hazikusaidia kufanikisha mswada ambao ni hitaji la Katiba. Maneno mazito ya Bw Ruto siku iliyotangulia kwamba wanaopinga mswada huo “ni sawa na wakoloni” hayakutosha kugusa nyoyo za wabunge kujitokeza kwa wingi na kuupitisha.

Hata uwepo wa vinara wa Nasa Raila Odinga na Kalonzo Musyoka bungeni hakukuibua msisimko wala hisani ya kuchukulia shughuli hiyo kwa umuhimu uliostahili.

Badala yake tulichobakia nacho ni kumbukumbu za cheche za maneno na matusi zilizotanguliza mswada huo kufikishwa bungeni. Mbunge Maalum David Ole Sankok aliibua hasira za wengi kwa matamshi yake kwamba wanawake hawafai kutengewa nyadhifa za kisiasa kwa sababu wengi wao, haswa wale ambao hawana waume sio watu wa kuaminika.

Alichukulia uwezo wa wanawake hao kushikilia kiti cha kisiasa kuwa usiowezekana kisa na maana wamezaa na wanaume tofauti. Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino naye aliona anaweza kuunga mkono tu mswada huo kwa sababu “wanawake wana kitu cha kumpa” kinyume na waume ambao alidai hawawezi “kumfaa kwa lolote”.

Kwa kuangalia semi hizi, ni wazi kwamba zinatoka vinywani mwa watu wasioelewa wala kutambua maana halisi ya hitaji hilo lililofikiriwa na waliounda Katiba kuwa muhimu zaidi kiasi cha kulinakili kinaga ubaga.

Inasikitisha kwamba suala la usawa wa kijinsia, na jinsia hapa ikiwa na maana ya wake kwa waume, limedhalilishwa kuwa jambo la mapenzi au vitendo vya kimapenzi huku wengine wakiona kuwa litakalotumiwa kama nafasi ya wakuu wa vyama kuteua wake na wapenzi wao wa pembeni kwa nyadhifa hizo.

Kile wengi wanachosahau katika mjadala huu ni kwamba usawa wa kijinsia unaathiri jinsia zote. Huenda leo ni idadi kubwa ya wanaume walio uongozini lakini hakuna ajuaye ya kesho.

Mswada huo sharti utakuja kupitishwa. Itakuwa jambo la busara kwa wabunge kutafuta mbinu za kukabili hizo ‘shida’ zote walizoziona na kupitisha mswada huo haraka iwezekanavyo.