Makala

TAHARIRI: Wabunge wazimwe kujiongezea ujira

January 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA MHARIRI

Hakikisho la Spika wa bunge la taifa Justin Muturi kwamba itakuwa kinyume cha katiba kwa wabunge kujiongezea mishahara ni jambo la kutia moyo kwa Wakenya ambao siku zote wamekuwa wakilalamikia hatua ya wabunge kujilimbikizia mishahara na marupurupu.

Jukumu la kuratibu mishahara ya wafanyakazi wa umma ni la Tume ya Mishahara na Marupurupu(SRC). Hata hivyo, SRC ililaumiwa sana mwaka jana kwa kuwapunguzia wabunge mishahara yao.

Jambo moja ambalo wabunge wamejisahau na kusahau mirengo mbalimbali ya kisiasa wanamotoka ni hili la kupiga kura ili kujiongezea mishahara na marupurupu.

Matokeo yake ni kwamba wabunge wetu ni mojawapo wa wanaolipwa vizuri zaidi ulimwenguni na si kwamba wamefanya kazi kubwa au wana maarifa ya kipekee yanayoweza kuinua hali ya wananchi. Wengi wao wana rekodi mbaya za maendeleo, licha ya kusimamia hazina kubwa ya fedha za maendeleo ya maeneo bunge almaarufu CDF.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga ameutaka uongozi wa bunge la kitaifa kufafanua kuhusu tetesi za wabunge kutaka kujiongezea mishahara na mrupurupu. Amemtaka Bw Muturi kuhakikishia Wakenya kwamba mipango hiyo haipo na kwamba hawana nia ya kufanya hivyo.

Sote tunakubaliana kwamba kwa kauli hii kwamba hapana haja tena ya wabunge kuongezewa marupurupu na wazo la kuwaongezea si zuri hasa ikizingatiwa kwamba uchumi haujatengemaa sawasawa.

Hili linapelekea sisi kujiuliza kama kweli viongozi hawa walisaka nyadhifa hizi ili kujitajirisha au kuhudumia wananchi. Inatia moyo Spika Muturi kutuhakikishia kwamba iwapo hoja kama hiyo itafika bungeni basi itaangushwa kwa kishindo.

Uhakikisho kama huu umewafanya Wakenya sasa kumwangalia Muturi iwapo atapesa jicho na kuruhusu hoja hiyo ipite au la.

Wabunge anapaswa kuzingatia hali ya uchumi wa nchi na namna Wakenya wanateseka kila uchao kufuatia hali ngumu ya maisha, kisha wakatae kujadili hoja yoyote ya kuwaongezea mishahara na marupurupu yao.

Badala yake watekeleze majukumu yao ipasavyo kama Wakenya wazalendo.