TAHARIRI: Wahanga wa mkasa wa maporomoko Pokot wasaidiwe
NA MHARIRI
Mkasa uliotokea Kaunti ya Pokot Magharibi ambapo watu 37 wanahofiwa kuzikwa na maporomoko ya ardhi usiku unasikitisha jinsi unavyohuzunisha.
Kwamba wakazi wasio na hatia waliangamia ni hasara kubwa kwa taifa alivyosema Rais Uhuru Kenyatta.
Ikizingatiwa kwamba barabara zinazoelekea eneo hilo ziliharibiwa ni jambo la kutia moyo kuona Rais alichukua hatua na kuagiza Jeshi la Kenya kuungana na idara zinazohusika kuhakikisha zimerekebishwa na kusaidia wakazi.
Ni kweli wakazi hao wanahitaji chakula na dawa na pia makazi. Pia wanahitaji kusaidiwa kuzika wapendwa wao. Waliolazwa hospitali hawafai kudaiwa chochote.
Ni uchungu kwa familia kupoteza watu zaidi ya kumi kwa wakati mmoja. Hii inahitaji walionusuruka kupatiwa ushauri nasaha na kufuatiliwa kwa karibu kwa muda ili waweze kurudia hali yao ya kawaida ikiwa ni pamoja na kujenga makao yao upya.
Na sio hivyo pekee, wote wanaokabiliwa na hatari ya kukumbwa na maporomoko katika maeneo tofauti ya nchi wanafaa kusaidiwa kuhamia maeneo salama.
Haitoshi kuwataka wahame bila kuwaonyesha mahali pa kwenda. Baadhi yao ni masikini wasioweza kupata cha kutia tumboni.
Wakati huu ambao mvua inaendelea kunyesha kuna uwezekano wa mikasa zaidi kutokea maeneo tofauti nchini ilivyoonya idara ya utabiri wa hewa na idara husika zinapaswa kuwatambua na kuwaelekeza maeneo salama.
Kwa kuwa idara ya utabiri wa hali ya hewa hutoa onyo la uwezekano wa mikasa kutokea mapema, idara hizi zinajukumu la kuchukua hatua kuepusha maafa kama yaliyotokea Pokot Magharibi.
Mazoea yetu huwa ni kusahau haraka mikasa inapotokea na kukumbuka ikitokea tena. Huu ni mtindo mbaya ambao hutusababishia hasara ambayo inaweza kuepukwa.
Serikali kupitia idara ya mipango maalumu inafaa kuwajibika na kuhakikisha hakuna atakayepoteza maisha kwa kuzikwa na maporomoko ya ardhi. Hili linawezekana kila afisa wa nyanjani akiwajibika.
Msimu huu wa mvua, kila mtu anafaa kuwa mwangalifu na kuepuka mito na maeneo yaliyofurika. Madereva wanapaswa kuendesha magari kwa uangalifu kwa sababu barabara ni telezi na ajali zinaweza kutokea. Aidha, daraja zinaweza kusombwa na maji ya mafuriko.