Makala

TAHARIRI: Walioagiza mahindi mabovu waanikwe

November 2nd, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA MHARIRI

Ripoti za hivi majuzi kwamba takribani magunia milioni nne ya mahindi ambayo yamehifadhiwa kwenye maghala ya Halmashauri ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) yameharibika na hayafai kwa matumizi ya binadamu ni za kusikitisha na kila hatua zinapasa kuchukuliwa kuhakikisha wahusika wote kwenye kashfa hii kubwa wanachukuliwa hatua za kisheria.

Serikali ilitumia Sh7.6bilioni kugharimia ununuzi wa nafaka hizo mwaka jana. Bila shaka kuna utaratibu maalumu unaofuatwa na taasisi hiyo inaponunua chakula hicho.

Huu ndio wakati mwafaka kwa Wakenya kujua ni nani aliyeagiza chakula kibovu ambacho kinahatarisha maisha ya mamilioni ya Wakenya.

Kama tulivyowahi kutaja kwenye safu hizi mbeleni, Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri hawezi kujinasua kutokana na uozo huu. Amenukuliwa akisema mara si moja kwamba, kashfa hii ilifanyika kabla hajachukua usukani katika wizara hiyo.

Huenda hilo ni kweli, lakini ilivyo ni kwamba, waziri ndiye kinara wa wizara na ana uwezo wa kupekua rundo la stakabadhi zinazoonyesha aliyeagiza chakula hicho na aliyeidhinisha malipo kwa chakula kisichofaa kwa matumizi ya binadamu.

Kuna taasisi mbalimbali ambazo zinahusika katika kutathmini ubora wa vyakula nchini. Mwanakemia wa Serikali, Taasisi ya Kukagua Afya ya Mimea nchini (Kephis) pamoja na Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa (KEBS).

Kwa kweli Bw Kiunjuri hawezi kudai kwamba hana uwezo wa kuendesha uchunguzi wa kina kubaini masuala kama vile, iwapo chakula hicho kilinunuliwa kikiwa tayari kimeoza au ni uhifadhi duni ulichangia katika uharibifu huo.

Inashangaza kwamba, baadhi ya Wakenya wako radhi kuagiza chakula kilichooza kutoka ugenini kwa lengo la kujitajirisha bila kujali athari yake kwa usalama wa raia wenzao.

Mbona ni vigumu kwa Waziri kutangaza hadharani wahusika wakuu kwenye kashfa hiyo ili Wakenya wamfahamu aliyegubikwa na tamaa ya kutajirika haraka kiasi cha kutaka kutoa kafara mamilioni ya raia wenzake!

Tunaungana na Seneta wa Uasin Gishu Margaret Kamar kuhimiza Wizara ya Kilimo kuhakikisha mahindi hayo yaliyooza yanalindwa na pengine hata kuharibiwa ili yasije yakasambazwa na maafisa walaghai katika Halmashauri ya Nafaka na Mazao kama ilivyofanyika wakati sukari ilibainika kuwa mbaya na hatimaye ikasambazwa licha ya kupigwa marufuku na Serikali.