• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 1:24 PM
TAHARIRI: Wazazi wasaidie kukuza maadili

TAHARIRI: Wazazi wasaidie kukuza maadili

Na MHARIRI

Ufichuzi wa Wizara ya Elimu na Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) kuhusiana na mbinu zinazotumika kuiba mitihani ni jambo la kusikitisha kwa taifa ambalo linalenga kujinasua kutoka kwa ufisadi.

Taarifa hizi pia zinaudhi kwa sababu kuna wanafunzi ambao wanakesha wakisoma kwa kuwa wanatambua umuhimu wa kutia bidii kwa matumaini ya kuboresha siku zao za usoni, na utulivu unafaa ili waweze kumakinika.

Imebainika kuwa baadhi ya wanafunzi hufanya fujo ili kuweza kufanyia mitihani yao ya kitaifa hasa ya Kidato cha Nne (KCSE) kama wanafunzi wa kutwa, hasa wakiwa wako kwa shule za bweni.

Kinachoibua hofu zaidi ni kuwa baadhi ya wazazi wanaruhusu hili, na isitoshe kuendeleza wizi huo kwa kusaidia wana wao kupata mbinu za kudanganya katika mitihani hiyo.

Hali hii inaibua hofu kuu kwa jamii ambayo kwa sasa inakabiliana na uovu wa kila aina na kushangaza ikiwa ni kina nani ambao watasimama kuwa vielelezo wema kwa wanafunzi na kusaidia vizazi kujirekebisha na kukusudia kufanya mambo yanayofaa.

Wapo wazazi ambaoi husaidia watoto wao kujiunga na shule fulani hata ingawaje alama zao haziwaruhusu kuwa hapo na baadaye kushindwa kumudu masomo kulingana na kozi wanazojiunga nazo, na hatimaye kuvuruga sekta mbali mbali kwa kuwa hawana utaalam unaofaa.

Serikali imeonyesha juhudi zake za kujaribu kukabiliana na baadhi ya maovu yanayoathiri jamii na itakuwa muhimu kuona wananchi nao kufuata mkondo huo. Itashangaza sana kuona jamii ikiwa ya kwanza kupiga kelele ilhali yenyewe inakubali kuhujumu kanuni na taratibu zilizowekwa.

Wazazi wahimize watoto kumakinika na sio iwe ni wao ambao wananunua mitihani na kuwapelekea ili waweze kushiriki udanganyifu ama kuwafichia simu ambazo watatumia shuleni kwa madhumuni hayo ya udanganyifu.

Mzazi anapofanya jambo kama hilo anafaa kutambua kuwa hatua yake itaathiri maadili ya mwana huyo maishani mwake, na huenda akaishia kufunzwa na ulimwengu.

Haifai kuona serikali ikiendelea kulalama kuhusu desturi ambayo msingi wake ni watu wazima waliopotoka maadili na ambao lengo lao ni kuonyesha jamii umahiri wao na kusifika bila kujali athari zake kwa kizazi husika ambacho inakivuruga.

You can share this post!

Gavana awarudisha kazini mawaziri kisha kuwapiga kalamu tena

Junet: Ruto ni kama sisi, hajui lolote kuhusu muafaka,...

adminleo