TAHARIRI: Wazazi wawajibike katika kulipa karo
KITENGO CHA UHARIRI
WIKI iliyopita, Waziri wa Elimu, Prof George Magoha aliwaamuru wakuu wa shule wawaruhusu wanafunzi kurudi shuleni bila kulipa karo.
Alichukua uamuzi huo, labda kutokana na kilio cha wazazi wengi kwamba walifahamishwa ghafla kuhusu ufunguzi huo.
Awali, waziri alikuwa ametangazia umma kwamba wanafuzni wangeendelea kukaa nyumbani hadi Januari 2021.
Lakini baada ya wadau wa sekta ya elimu kutathmini hali ya maambukizi ya Corona, walimshauri Prof Magoha aanze kwa kufungua madarasa ambayo wanafunzi wake ni watahiniwa watarajiwa.
Baadhi ya wanafunzi waliorejea shuleni, hasa wa kidato cha nne, hawakuwa wamekamilisha karo ya muhula wa kwanza. Lakini waziri alipowaomba walimu wakuu wasiwafukuze wanafunzi wa sababu ya karo, wazazi wengi walichukua fursa kupeleka watoto wao bila karo yoyote.
Wakuu wa shule za upili wanasema shule nyingi hazimudu kuwaweka wanafunzi shuleni, kutokana na changamoto za kifedha. Na huo si uongo. Shule, hasa za bweni, hutegemea fedha kutoka kwa karo zinazolipwa na wanafunzi. Huduma muhimu kama kuwapa chakula wanafunzi, haziwezi kufanyika iwapo hakuna pesa.
Wazazi walio na watoto katika shule za bweni wanajua kwamba wanahitajika kulipa ada za bweni. Wakuu wa shule wanakabiliwa na wakati mgumu. Bila fedha, ni vigumu kuwalisha wanafunzi na pia kutimiza mahitaji yao ya bweni. Wakulima wanaosambaza nafaka na bidhaa nyingine kwa shule, hutaka pesa.
Wazazi lazima watimize wajibu wao na kuwalipia watoto wao karo ya shule ya muhula wa pili.
Japokuwa hali ya uchumi haijaimarika jinsi ilivyotarahiwa, ugumu wanaokumbana nao wazazi ni mara mbili ya wanaopitia wasimamizi wa shule za bweni. Je, kama mtoto hangeenda shuleni, mzazi angemwacha mwanawe na njaa?
Aidha, wizara ya Elimu yapaswa kuharakisha kupeleka pesa kwa shule ili walimu wakuu wawe na uwezo wa kutekeleza baadhi ya majukumu muhimu. Pesa zilizotumwa wiki iliyopita zilikuwa chache sana, na hazitoshi kuendesha shule. Muhula huu, wizara ilitoa Sh14.4 bilioni kwa shule za msingi na sekondari kuwasaidia kujiandaa kwa ufunguzi wa awamu baada ya awamu.
Pesa hizo, bila ya mchango wa wazazi, ni kama tone la maji baharini.