TAHARIRI: Wizara ihakikishe kila mtoto anapata elimu
Na MHARIRI
MTIHANI wa Darasa la Nane (KCPE) ulikamilika Alhamisi huku visanga kadha wa kadha vikishuhudiwa nchini.
Mojawapo ya visa vya kusikitisha ni ripoti kwamba, watahiniwa 11 wafuasi wa dhehebu la Kavonokya katika Kaunti Ndogo ya Tharaka Kaskazini, Kaunti ya Tharaka Nithi, hawakufanya mtihani wao.
Wanafunzi hao walisitisha masomo mwaka 2019 baada ya wazazi wao kujiunga na dhehebu hilo la kitamaduni. Kulingana na mkurugenzi wa elimu katika kaunti hiyo ndogo, inakisiwa takribani wanafunzi 280 wa dhehebu hilo waliacha shule kipindi cha baina ya Januari na Agosti.
Licha ya kwamba walikuwa wamesajiliwa kufanya KCPE kabla yao kuacha shule, hawakujitokeza kuandika mtihani huo wa kitaifa. Wala hawakupatikana nyumbani walipotafutwa na maafisa wa serikali. Inasemekana walitoroka baada ya wazazi wao kukamatwa kwa kukataa kuhesabiwa wakati wa zoezi la Sensa.
Habari njema ni kwamba, msako uliofanywa ulifanikiwa kurejesha watoto 40 shuleni. Hata hivyo, hii ni idadi ndogo sana (asilimia 15) ya waliotoroka.
Si jambo geni kwa wafuasi sugu wa dhehebu hilo, lenye wanachama wengi katika Kaunti ya Kitui, kukataa mambo ya kisasa, wakisisitiza kufuata mitindo ya ukale.
Habari za wanachama kukataa kwenda kutibia hospitalini, ama watoto wao kupewa chanjo, zimesheni waliko wafuasi hao. Kinachosikitisha ni kuwa, maisha ya wafuasi hao hutokomea bure kwa sababu yao kushikilia imani iliyopotoka.
Sasa maisha ya watahiniwa waliokosa kufanya KCPE yatavurugwa. Badala yao kupata maarifa yanayoletwa na elimu, watasalia katika ukale usioleta manufaa kwao wala maendeleo kwa jamii nzima.
Huu ni ukandamizaji wa aina ya kipekee kwani huwa umemteka mtu akili, haoni mazuri anayokosa na madhara anayojiletea.
Serikali italazimika kutumia mbinu tofauti kukabiliana na dhehebu hilo na mengineyo yaasiyokumbatia masuala ya kimsingi maishani, kama elimu, afya na makazi bora.
Kwanza, nguvu zitumike kukamatwa viongozi wao kwa kuhadaa wanachama wakiuke Katiba. Kisha kampeni kabambe ya kudumu ya hamasisho ianzishwe kwa lengo la kuwaondoa katika kasumba iliyowanasa. Tatu, itakuwa vyema serikali ikipeleka maendeleo ya kisasa katika makazi yao ili wajionee matunda ya elimu hiyo wanayoipuuza.