Tawasifu ya Abraham Kithure Kindiki, naibu rais mpya mteule
ENDAPO Bunge la Kitaifa litamuidhinisha Prof Kithure Kindiki kumrithi naibu rais anayeondoka, Rigathi Gachagua, Kindiki atakuwa naibu rais wa pili chini ya utawala wa serikali ya Kenya Kwanza.
Prof Kindiki, aidha, atakuwa naibu wa rais (wadhifa ambao awali kabla ya Katiba ya 2010 kupitishwa na kuanza kutumika, ulijulikana kama makamu wa rais) wa 12 katika Jamhuri ya Kenya.
Bunge, Ijumaa, Oktoba 18, 2024 limeandaa kikao maalum kujadili uteuzi wake, baada ya Seneti kupiga kura ya kumbandua Bw Gachagua na Rais William Ruto kupendekeza Kindiki kuwa naibu wake.
Gachagua, Alhamisi, Oktoba 17, maseneta walimpata na hatia ya makosa matano, yakiwemo ya ufisadi, kueneza siasa za chuki na ukabila, kati ya mengine, kwa jumla ya 11 ambayo Bunge la Kitaifa lilipitisha kumng’atua.
Huku taifa likijiandaa kuwa na naibu rais mpya, wengi wangetaka kujua Prof Kithure Kindiki ndiye nani?
Kwa mujibu wa cheti chake cha kuzaliwa, anafahamika kama Abraham Kithure Kindiki.
Ni raia wa Kenya, aliyezaliwa Julai 16, 1972 katika Gatuzi (Kaunti) la Tharaka Nithi.
Prof Kindiki ni baba na mume wa Dkt Joyce G. Njagi.
Kulingana na tawasifu yake, yeye ni Profesa wa Masuala ya Sheria, kando na kuwa mtumishi wa umma, ikiwa ni pamoja na kuwa mkwasi wa tajiriba ya uongozi na utawala wa umma.
Kabla kuteuliwa na Dkt Ruto mnamo Ijumaa, Oktoba 18, kuwa naibu wake, Prof Kindiki alikuwa akihudumu kama Waziri wa Usalama wa Ndani na Mikakati ya Serikali.
Aidha, amewahi kuhudumu kama Seneta wa Tharaka Nithi (2013 – 2022), na vilevile naibu spika Bunge la Seneti.
Prof Kindiki, ambaye pia ni wakili, ni mshauri wa masuala ya sheria na aliwahi kuwa mhadhiri (Profesa) katika vyuo vikuu kadhaa nchini.
Masomo
Prof Kindiki ni msomi, na mwaka 2000 alifuzu kwa Shahada ya Uzamili katika Masuala ya Sheria (Masters of Laws (LL. M) kutoka Chuo Kikuuu cha Pretoria, Afrika Kusini.
Miaka miwili baadaye, 2002, chuo hicho hicho cha Afrika Kusini kilimtawaza shahada ya Udaktari kwenye masuala ya Sheria (Doctors of Law – LL. D), tunu ya kimasomo iliyomfungulia mlango wa kuitwa Profesa.
Aidha, naibu rais mteule huyu mpya pia ana Shahada (Digrii) ya Masuala ya Uwakili na Uanasheria kutoka Chuo Kikuu cha Moi, bila kusahau Stashahada (Diploma) kutoka Taasisi ya Uanasheria Nchini (Kenya School of Law).
Akiwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Prof Kithure Kindiki alijivunia sifa kutokana na utendakazi wake kulainisha idara ya usalama Kenya, ikiwemo kukabiliana na kero ya wizi wa mifugo na ujangili Bonde la Ufa.
“Gatuzi langu awali lilikuwa ngome ya uhalifu kupitia wizi wa mifugo, kero iliyosababisha maafa. Kwa sasa, visa hivyo vimepungua mara dufu kwa sababu ya jitihada za Prof Kindiki,” akaandika Gavana wa Elgeyo Marakwet Wisley Rotich kupitia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii Ijumaa, Oktoba 18, akipongeza Prof Kindiki kwa kuteuliwa kuwa mrithi wa Bw Gachagua.
Prof Kindiki pia amesaidia kuleta mabadiliko katika Huduma ya Kitaifa kwa Polisi (NPS).
Hata hivyo, wakati wa maandamano ya Gen Z kukosoa serikali alinyooshewa kidole cha lawama kwa kusalia kimya vijana wakidaiwa kuuawa na kudhulumiwa na polisi.
Kalainisha idara ya uhamiaji
Idara ya Uhamiaji ambayo hasa inajukumika kutoa Pasipoti za Usafiri nje ya Nchi, awali ilikuwa jukwaa la ufisadi na ni kupitia bidii za Bw Kindiki sasa inaendelea kulainika na kunyooka.
Wakati mmoja, akiendelea kuhudumu kama Waziri wa Usalama wa Ndani alizuru makao makuu ya uhamiaji, Nyayo House ambapo aliitaja kuwa ‘eneo la uhalifu’ lengo lake likiwa kuondoa uovu uliokuwa ukisakatwa humo.
Tawasifu ya Prof Kindiki, hali kadhalika imeainisha michango yake katika nyadhifa mbalimbali za umma alizoshikilia, pasi kusahau akiwa Mhadhiri, na taasisi alizohudumu.
Mwaka 2015, alitambuliwa na Rais Mstaafu, Uhuru Kenyatta kupitia tuzo ya Elder of the Order of the Golden Heart of Kenya (EGH) kufuatia mchango wake katika Jamhuri ya Kenya.
Bunge la Kitaifa likipitisha uteuzi wake, Rais Ruto atamuidhinisha kwa kutia saini kisha aapishwe rasmi kuanza kuchapa kazi.
Isitoshe, sharti majina yake yachapishwe kwenye Gazeti Rasmi la Kiserikali kama naibu rais.