• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
TEKNOHAMA: Usitegemee app tu katika kupanga uzazi, nyingi zinapotosha

TEKNOHAMA: Usitegemee app tu katika kupanga uzazi, nyingi zinapotosha

Na LEONARD ONYANGO

KUNA njia tele za wanawake kujua siku zilizo na uwezekano mkubwa wa kupata ujauzito.

Kwa wanawake ambao mzunguko wa hedhi ni siku 28, wataalamu wa afya ya uzazi wanasema kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kupata mimba siku ya 14.

Siku ya 16 ndiyo ya uwezekano mkubwa zaidi kwa wanawake ambao mzunguko wao wa hedhi ni siku 30 au 32.

Mbinu ya kuhesabu siku inaweza kutumiwa katika upangaji wa uzazi kwa kuepuka kushiriki mapenzi au kutumia kinga siku kama hizo.

Siku ambazo mwili wa mwanamke unapojiandaa ‘kutoa’ yai, huwa na joto jingi kuliko siku nyinginezo. Kupanda na kupungua kwa joto pia kunaweza kutumiwa katika upangaji wa uzazi.

Katika kujaribu kupanga uzazi bila kumeza tembe au kudungwa sindano, wataalamu wa afya wameunda programu (app) tele za simu zinazolenga kuwasaidia wanawake kufahamu siku zilizo na uwezekano wa kupata ujauzito.

Mnamo Agosti, mwaka huu, Mamlaka ya Kudhibiti Ubora wa Vyakula na Dawa nchini Amerika (FDA) iliidhinisha app ya kwanza; Natural Cycles, inayosaidia wanawake kupanga uzazi.

App hiyo ya simu inahesabu siku na hata kupima joto la mwili wanawake. App hii hushauri wanawake kutumia kinga au kujiepusha na mapenzi katika siku za hatari.

Je, app za simu zinaweza kuaminika kama mbinu za kupanga uzazi?

Wataalamu wanasema kuwa kutumia app kama njia ya kupanga uzazi si salama kwa asilimia 100.

Wanasema kuwa asilimia 20 ya wanawake wanaotumia kwa uaminifu app ya simu kama njia ya kupanga uzazi hujipata na ujauzito.

Kulingana na wataalamu, matumizi ya tembe, upasuaji au sindano ni njia za kuaminika zaidi katika upangaji uzazi kuliko app za simu.

Wakati wa kuidhinisha app ya Natural Cycles, mamlaka ya FDA, ilisema kuwa uwezekano wa program hiyo kupotosha wanawake ni asilimia 7.

FDA pia inaonya kuwa wanawake wanaotaka kutumia app kama njia ya kupanga uzazi ni sharti wapate ushauri kutoka kwa madaktari kwanza.

“Siku za mzunguko wa hedhi hutofautiana kutoka mwezi mmoja hadi mwingine katika baadhi wanawake hivyo app zinaweza kuwapotosha,” ikasema mamlaka ya FDA.

Mbali na Natural Cycles, app nyinginezo ambazo hutumiwa ni Lemonaid, Virtuwell, Nurx na Maven na The Planned Parenthood.

App ya the Planned Parenthood pia inaweza kutumika kuwasiliana na daktari na hutumiwa kwa wingi katika maeneo ya Alaska, Hawaii, Idaho, Minnesota, na Washington nchini Amerika.

App za simu zinazolenga wanawake zinaendelea kutengenezwa huku wataalamu nchini India wakisema kuwa wamegundua dawa itakayotumiwa na wanaume kupanga uzazi.

Hiyo itakuwa dawa ya kwanza duniani kutumiwa na wanaume katika kupanga uzazi.

Mbinu zilizopo kwa sasa zinazotumiwa na wanaume kupanga uzazi ni kutumia mipira ya kondomu na kukata mirija ya kupitisha mbegu, maarufu Vasectomy.

Baraza la Utafiti wa Matibabu la serikali ya India tayari limekamilisha kufanyia majaribio dawa hiyo. Baraza hilo linasema dawa hiyo imeonyesha kufaulu kwa asilimia 98, kulingana na gazeti la nchini India, Hindustan Times.

“Majaribio yalifanyiwa jumla ya wanaume 303 na dawa hiyo ilithibitishwa kufaulu kwa asilimia 98. Haina madhara kwa watumiaji na sasa inaweza kutangazwa kuwa dawa ya kwanza ya kupanga uzazi ya wanaume,” akasema Dkt R.S. Sharma, mtafiti mkuu wa Baraza la Utafiti wa Matibabu la serikali ya India.

Dawa hiyo hudungwa sehemu nyeti kwa kutumia sindano na inakaa mwilini kwa kipindi cha miaka 13.

Watafiti nchini Amerika pia wameunda dawa ya kupanga uzazi ya kutumiwa na wanaume inayofahamika kama

Vasalgel, lakini wanasema kuwa itachukua kipindi cha miaka 10 ijayo kabla ya kuanza kuuzwa.

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Hatari ya sumu ipo kila twendako sio kwenye...

MAZINGIRA NA SAYANSI: Taa za mitaani ni hatari kwa wadudu,...

adminleo