Akili MaliMakala

Teknolojia ya AI kutoa mikopo kwa wakulima

Na SAMMY WAWERU February 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

TARATIBU ndefu kuomba mikopo kwenye mashirika ya kifedha ni kati ya changamoto zinazozingira wakulima wenye mashamba madogo.

Hilo hasa linatokana na ukosefu wa mahitaji yaliyowekwa na mashirika ya kifedha.

Kusaidia kutatua changamoto hii, chama kimoja cha ushirika nchini (Sacco) kimezindua mpango wa AI kutoa mikopo kwa wakulima.

Mpango huo wa kidijitali unalenga kukusanya habari muhimu kuhusu mkulima, habari ambazo zitatumika kutoa mkopo.

Kulingana na Fortune Sacco, chama kilichozindua programu hiyo, itasaidia kuondoa mahitaji mengi na taratibu nyingi zinazofuatwa kupiga msasa mkulima anapohitaji mkopo.

Chama hicho cha wakulima kinasema mpango huo wa AI utawezesha mkulima kupata hela, bila kupitishwa taratibu ndefu kama inavyoshuhudiwa kwenye Sacco na benki.

Isitoshe, kazi nyingi inayofanywa na wahudumu wa mashirika ya kifedha kupekua maelezo zaidi kuhusu mkulima itapungua.

Timothy Muthike Naibu Afisa Mkuu Mtendaji Fortune Sacco, akielezea kuhusu mpango wa AI kusaidia wakulima. PICHA|SAMMY WAWERU

Kwenye mahojiano na Akilimali wakati wa uzinduzi wa mpango huo unaojulikana kama AI-Powered Credit Scoring Solution for Farmers, Timothy Muthike Naibu Afisa Mkuu Mtendaji Fortune Sacco, alisema programu hiyo itarahisisha huduma za chama hicho kwa wakulima.

“Tunalenga sekta zenye mikakati maalum kama vile kilimo cha kahawa na chai, na zaidi ya yote zisizo na mpangilio kama vile ukuzaji wa ndizi, nyanya, muguka, avokado na maharagwe ya Kifaransa,” Muthike akaelezea.

Afisa huyo ambaye pia ni Msimamizi wa Kitengo cha Fedha, alilalamikia sekta za mimea hiyo kutengwa licha ya mchango wake mkubwa kwenye ukuaji uchumi (GDP), hasa katika utoaji wa mikopo.

Mimea hiyo haijajumushwa kwenye orodha ya zinazokusanywa data, hivyo wakulima wa mashamba madogo kuhangaika kupata mikopo.

Kupitia mpango wa Fortune Sacco, ambapo AI inatumika kukusanya habari – data kuhusu wakulima, wataweza kupata fedha kwa haraka ili kuwapiga jeki kuendeleza zaraa.

Programu hiyo inapania kukusanya habari muhimu za wakulima, ikiwemo data kuhusu ikiwa mkulima ameoa au kuoleka, maelezo ya mume na mke, idadi ya watoto na shule wanazosomea, kiwango cha shamba na idadi ya mimea.

Bw Timothy Muthike Naibu Afisa Mkuu Mtendaji Fortune Sacco, akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfumo wa AI utakaotumika na chama hicho cha ushirika kutoa mikopo kwa wakulima wanachama. PICHA|SAMMY WAWERU

“Kimsingi, maelezo hayo hayapo. Na kwa kutumia AI, tutaweza kukusanya habari muhimu za mkulima hivyo basi kurahisisha taratibu za utoaji mikopo, kinyume na itikadi za zamani ambapo anahitaji kuwa na wawekezaji wenza kumsimamia, hisa na mifumo ya uzalishaji,” Muthike alifafanua.

Aliongeza, “Tunachukulia mkulima kama mwekezaji wa thamani sana, na tunataka kuwa na ‘kifaa’ kitakachomsaidia na pia kuifaa Sacco. Matumizi ya teknolojia na data kufanya maamuzi kutoa mikopo, yatasaidia pakubwa kuboresha sekta pana ya kilimo.”

Mpango huo unadhaminiwa na German Agency for International Cooperation (GIZ), na unalenga kunufaisha wakulima 60,000 waliosajiliwa na Fortune Sacco.

Muthike, alifichua kwamba tayari wakulima wapatao 15,000 wameanza kupokea mikopo kupitia programu hiyo ya AI.

Wafadhili wengine ni kampuni za AI, data na zenye bunifu za kidijitali, ikiwemo Pathways Technologies.

“Kugeuza sekta ya kilimo iwe ya kidijitali, hatuna budi ila kuaga mifumo ya zamani isiyoleta mabadiliko na badala yake tukumbatie bunifu za kisasa kuikuza,” akasema.

Bw Joel Onditi, Afisa Mkuu Mtendaji Pathways Technologies. PICHA|SAMMY WAWERU

Huku ulimwengu ukikumbatia dijitali kuboresha utoaji huduma na bidhaa, Onditi anasisitiza haja ya ukusanyaji data katika sekta ya kilimo na ufugaji.

Anaamini teknolojia ya AI itasaidia serikali na wadauhusika muhimu kuangazia changamoto zinazozingira wakulima, ikiwemo kuwezesha mashirika ya kifedha kutoa mikopo kwa wakulima wa mashamba madogo.

“Teknolojia imeboresha sekta ya fedha. Kilimo pia kinahitaji kufuata nyayo hizo ili kuimarika,” Onditi anahimiza, akiainisha mianya tele ya ufanisi inayotokana na safu za kidijitali.

Kwa sasa, serikali inashughulikia mpango wa kitaifa wa ukusanyaji data za mifugo, unaojulikana kama National Livestock Master Plan intervention.

Mpango huo unalenga kuboresha sekta ya mifugo nchini, hasa kuhakikisha nyama za Kenya zinakuwa salama ili kuwahi masoko yenye ushindani mkuu ng’ambo.

Kufanikisha mpango wa Fortune Sacco, mwaka huu umepangiwa bajeti ya Sh80 milioni.

Pathways Technologies ni mojawapo ya kampuni zinazoshirikiana na Fortune Sacco kufanikisha AI kusaidia wakulima kupata mikopo, Joel Onditi, Afisa Mkuu Mtendaji akisema teknolojia ya kisasa itaboresha sekta ya kilimo. PICHA|SAMMY WAWERU

Kuafikia Sheria za Uhifadhi wa Data, Muthike anasema chama hicho cha ushirika kina mkataba wa makubaliano na kila mkulima, ambapo wamehakikishiwa usalama wa maelezo yao ya kibinafsi.

Anasema shirika hilo linatii sheria za data, na kwamba lina kikosi maalum kuhakikisha data hazidukuliwi.

Matumizi ya teknolojia ya AI, ni mojawapo ya mikakati kuvutia vijana kujitosa kwenye mtandao wa kilimo.

Vijana wengi wanalemewa kushiriki shughuli za kilimo kwa sababu ya kukosa hatimiliki za mashamba – hivyo basi kukosa dhamana kuwasimamia kuomba mikopo.

Hilo, linakwamisha ukuaji wa sekta ya kilimo.

Kulingana na Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo Kenya (KALRO), karibu asilimia 25 (sawa na milioni 6.5) ya watu wanaoshiriki kilimo inawakilishwa na vijana.