Makala

Tume ya polisi ilivyopokonywa majukumu na maafisa wakuu

Na  KAMORE MAINA March 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

IWAPO ripoti ya jopokazi lililoongozwa na Jaji Mkuu (Mstaafu) David Maraga kuhusu mageuzi ya polisi ingetekelezwa kikamilifu, makamishna wa Tume ya Kitaifa ya Huduma ya Polisi (NPSC) wangeondoka ofisini miezi sita kabla ya kumaliza muhula wao.

Hata hivyo, kutochukuliwa hatua zozote kwa mapendekezo ya jopo hilo kuliwafanya makamishna wa NPSC, wakiongozwa na Eliud Kinuthia, kumaliza muhula wao wa miaka sita.

Ripoti ya Maraga ilieleza kuwa, makamishna wa NPSC walishindwa kutekeleza wajibu wao kwa kuruhusu wakuu wa polisi katika makao makuu ya polisi Vigilance House kutwaa majukumu muhimu ya tume.

Ripoti hiyo iliongeza kuwa hatua hiyo, iliyotajwa kama mapinduzi kimyakimya ya maafisa wakuu wa polisi, ilisababisha NPSC kutochukua hatua, kuendeleza matatizo yale yale ambayo ilipaswa kutatua. Jopo lilipendekeza, miongoni mwa mambo mengine, kuondoka ofisini kwa makamishna wa sasa wa tume hiyo.

Rais Ruto alikuwa ameahidi kutekeleza kikamilifu mapendekezo ya ripoti ya Maraga kama sehemu ya ajenda ya serikali ya kurekebisha sekta ya usalama.

Baada ya kunusurika na kumaliza muda wao ofisini, makamishna wa NPSC sasa wamewasilisha ripoti yao ya kuondoka, wakitoa tahadhari kwa warithi wao—wawe waangalifu wasipokonywe mamlaka yao na wakuu wa polisi katika masuala ya kuwapandishwa vyeo na kuhamisha maafisa.Ripoti hiyo iliwasilishwa kwa Rais Ruto Jumatatu iliyopita.

Baada ya kupokea ripoti hiyo, Rais Ruto alisema serikali yake itatekeleza baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na tume inayomaliza muda wake. Makamishna hao walisisitiza kuwa suala hilo linapaswa kushughulikiwa ili kuzuia NPSC kunyang’anywa mamlaka na wakuu wa polisi.

Makamishna wanaoondoka walilalamika kuwa wakuu wa polisi katika Vigilance House huwasilisha tu orodha ya maafisa waliopandishwa vyeo baada ya mabadiliko hayo kufanywa.

Kwa mujibu wa sheria, NPSC ina mamlaka ya kuwapandisha vyeo na kuhamisha maafisa wa polisi kwa kushauriana na makao makuu ya huduma ya polisi.

Ripoti yao inasema kuwa wakuu wa polisi huwasilisha orodha ya maafisa waliopandishwa vyeo kwa tume baada ya mabadiliko hayo kutekelezwa.

Tume hiyo ilipendekeza kuwa wakuu wa polisi wanapaswa kwanza kuwasilisha majina na maelezo ya maafisa wanaokusudiwa kuhamishwa kwa tume kabla ya maafisa husika kuhamishwa.

Kwa mujibu wa tume, kushindwa kwa wakuu wa polisi kuwasilisha majina ya maafisa kabla ya kutekeleza uhamisho kumefanya baadhi ya mabadiliko kuonekana kuwa yana upendeleo.

Ili kutatua tatizo hilo, ripoti hiyo ilipendekeza wakuu wa polisi wazingatie kwa ukamilifu kanuni za uhamisho.

Rais Ruto alisema kuna haja ya kuendelea kuifanyia mageuzi huduma ya polisi ili kuhakikisha kuwa maafisa wana uwezo wa kukabiliana na mahitaji ya usalama wa nchi.

‘Hata tunapotambua mafanikio haya, tunakiri pia kuwa changamoto zinazohitaji umakini na juhudi za haraka. Masuala kama uajiri usio wa haki wa maafisa wa polisi, changamoto za bajeti, na hitaji la mpango endelevu wa ustawi wa maafisa wa polisi lazima yashughulikiwe bila kusita,’ alisema Rais.

Ripoti hiyo haikuzamia athari za mivutano ya mara kwa mara kati ya makamishna wa NPSC na uongozi wa polisi.

Makamishna wanaoondoka waliongeza kuwa timu mpya inapaswa kuangazia suala la maafisa waliokwama katika vyeo vyao kwa muda mrefu.

Ripoti ilisema kuwa hali hiyo imeathiri ari ya kazi ya maafisa wa polisi, ambao huenda wakahisi kutotiliwa maanani na kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Ili kutatua hili, ripoti ilipendekeza tume mpya ianzishe mfumo wa kupandishwa vyeo kwa kuzingatia utendaji kazi.