TUONGEE KIUME: Mapenzi ni kujitoa mhanga, wivu pekee hautoshi
IWAPO mpenzi wako ana wivu, anahisi kuwa unaweza kunyakuliwa na mafisi au mafisilettes, basi tulia, uko na bahati kwa kuwa hii ni ishara anakupenda.
Lakini haitoshi, inaweza kuwa anafanya hivyo kwa burudani unayompa ambayo hataki ugawie watu au mtu mwingine. Tegea nikupashe.
Wivu sio kila kitu kinachoweza kukufanya usadiki kwamba amekujaza kwa moyo wake. Peleleza zaidi kiwango chake cha imani na maisha yake ya kiroho. Ikiwa hapendi Mungu na sio tu kumpenda, kumcha kwa dhati, na anakusumbua muandamane kanisani au kwa masuala safi ya kiroho (masuala mengine sio safi) basi umeanza vyema, lakini bado.
Ili kujua iwapo amekomaa na kutosha mboga kabisa, usipagawishwe na nderemo zake chumbani zinazokufanya kusisimka au kupaa hadi mbingu ya saba. Lazima awe anakumanikia anavyofanyia moyo wake.
Nimesema kukumakinikia na kufanya hivyo kikamilifu na kwa vitendo. Akiwa wa mdomo mwingi, fikiria mara mbili; namaanisha weka baadhi ya alama kwenye parking uendelee kupeleleza.
Usiwe ni wewe unayemsaka. Lazima mtafutane, kama unamtafuta ukiwa na hamu ya kumuona na hafanyi hivyo, hata akikuonea wivu na awe moto wa kuwasha mwili wako na kuuyeyusha kila mnapokutana, mwache na usonge mbele. Wivu wake ni wa kujifanya. Kwake ni asiyekuwa machoni, hayupo moyoni.
Sasa naingia katika eneo hatari hasa kwa akina kaka; mtu anayedai anakupenda, hata akijawa na wivu wa kujaza bahari na akose kukutunza kama malkia au mfalme, unapoteza wakati naye. Na simaanishi uwe gold digger kwake.
Hapana, ninachosema ni kuwa mtu anayekupenda kwa dhati, atawajibika kuhakikisha uko sawa. Asipoonyesha dalili za kuwajibika, huyo ni mpita njia na wivu wake kwako hauna mashiko iwapo hamna historia uweze kuelewa hali na sababu ya dhati yake kutoweza kukutunza. Hapo mnaweza kusaidiana, uamuzi ni wako.
Lakini ili mtu kama huyo aweze kufuzu kuwa mwenye wivu chanya ni lazima adhihirishe kwa vitendo na maneno kwamba anakuheshimu. Heshima kaka, dada, thamani yake ni kupeana, ukiheshimu mtu na aitupe heshima hiyo kwa jaa la taka kisha akulipe kwa ukatili, hepa na usiangalie nyuma. Nasema tena, hepa!
Hili suala la kupeana heshima lina mapana yake pia, sio kwa heshima pekee. Mtu anaweza kuwa na wivu kukuhusu lakini awe hajakupa moyo wake bila masharti au uwe haujampa moyo wake vile vile bila masharti. Nakuachia hili ulitafakari, tena kwa kina. Na unapofanya hivyo nakuuliza, je, unaweza kuvumilia mtu asiyeweza kukupa zawadi hata kama ni lollipop? Kutoa ni moyo, sio utajiri lakini katika mapenzi, mtizamo ni tofauti kwa kutegemea mtu. Usimwekee mtu wako masharti kwamba usipokufanyia hili, hautamfanyie lile.
Mapenzi ni kujitoa mhanga kulinda mtu wako, wivu pekee hautoshi.