Makala

TUONGEE KIUME: Ukiona hizi dalili, jua kwamba uhusiano wako uko hali mahututi

Na BENSON MATHEKA July 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

UNATAKA kujua ni kwa nini uhusiano wako wa kimapenzi unaingia baridi na kukatika. Tega sikio nikupasulie.

Moja ya mambo haya yanachangia kuua mapenzi kati ya watu ambao walionekana vigumu kutengana.

Kukoma kuwasiliana au kukatiza mawasiliano, kunakuwa mwanzo wa mwisho wa uhusiano wetu. Hii inaweza kutoka kwa upande mmoja na kuathiri upande mwingine.

Mawasiliano ni lazima kwa uhusiano kuwa thabiti. Hapa ninazungumzia watu wawili wanaowasiliana hata kama wanatofautiana.

Ni vigumu kwa watu kukubaliana kwa kila kitu. Iwapo unakubaliana kila kitu na mtu wako kuna shida unayopaswa kung’amua mapema; nayo ni kuwa mmoja wenu anajifanya ili asimkosee mwenzake.

Haya ni makosa makubwa yanayoua uhusiano wa kimapenzi. Kutofautiana hakumaanishi hampendani; kujifanya ni kumaanisha kuwa hauna msimamo wako. Kuwa real iwapo unataka kuanza, kujenga na kudumisha uhusiano wa kimapenzi.

Kadiri watu wawili wanavyowasiliana, ndivyo wanavyojifunza kuishi pamoja lakini ikiwa wanafokeana, mapenzi huwa yanakufa. Mtu anayetaka kuua uhusiano wa kimapenzi huanza kwa kuchemkia mwenzake ili kuzua ugomvi.

Ugomvi unatokana na ukosefu wa mawasiliano na huwa unazaa mgogoro. Mkianza kupigana mara kwa mara, funganya virago, toroka, uwe mwanamume au mwanamke, jinusuru kwa kuwa hakuna hata chembe ya mapenzi huwa imebaki kati yenu na kuganda kwake kunaweza kuwa na matokeo mabaya.

Ukiona kila mmoja wenu anashughulika kivyake ilhali mlikuwa mnasaidiana au kufahamishana kila mmoja aliko, basi, usisubiri kuambiwa kuwa uhusiano wenu umeingia baridi, tayari uko ICU na kinachofuata na tangazo kwamba umekufa. Hei, kumbuka uhusiano wa kimapenzi huwa umekufa kitambo kabla ya kutangazwa umekufa. Upendo huwa unanyauka na kufa.

Na ukiona mtu wako ameanza ukuruba na watu wa nasaba yake na kutumia muda mwingi nao bila kukushirikisha, kaka na dada anza kujipanga, uhusiano wako na naye huwa umeanza kuyumba na nafasi ya kuurejesha huwa ni finyu sana hasa ikiwa mlikuwa na mipango ya kuoana.

Iwapo unadhani zangu ni ndoto, chukua hatua ufanye utafiti wa kina, utapata watu waliopitia haya, na badala ya kukosoa, ujipange usijipate katika hali hii.

Ukitaka uhusiano wako wa kimapenzi usife, epuka vishawishi vyote vinavyoweza kukuingiza katika uraibu wa vileo au ponografia. Wacha kutetea uraibu zaidi kuliko uhusiano wako wa kimapenzi. Huo uraibu unakufanya unyime mtu wako muda muhimu anaokuhitaji na hivyo kuua mapenzi kati yenu.

Kunyima mtu wako muda ukizama katika ulevi ni kuonyesha kuwa haumthamini na hali kama hii ikishamiri, mapenzi huwa yanahepa. Wewe ni mtu mwenye moyo wa chuma hivi kwamba hauwezi kusamehe mtu wako hata kwa makosa madogo, basi unachimbia kaburi uhusiano wako.