Tusemezane: Usiue ndoto yako maishani kwa sababu ya mapenzi na ndoa
USIKUBALI kuingia katika uhusiano wowote na mtu ukigundua anaweza kuua ndoto zako maishani.
Wale watu wanaokutaka uache kazi mkioana au ukatize masomo ili wakuoe.
Usidanganyike. Ndoa haifai kunyonga ndoto yako. Kwa hakika, inapaswa kuwa ya kutimiza unachoazimia maishani. Kukufanya uwe bora zaidi kwa sababu ya kuwa na mwenzi wa kukukamilisha, kukuunga mkono na kukutia shime.
Hivyo basi, iwapo mtu anayedai kuwa mkeo au mpenzi wako anatoa ishara za kuzima ndoto yako maishani, mwambie kwaheri. Muage kabisa na umsahau.
Huyo ni adui, ni pepo anayelenga kukunyima furaha yako maishani. Anataka uishi maisha yake na sio yako.
“Mpenzi anayekuwazia mema, hawezi kukubali uache masomo au kazi. Anakuhimiza na kukusaidia kupiga hatua.
Akilalamika kwa kuwa umeamua kuendelea masomo, huyo ni hatari. Hataki uwe na uwezo wa kukuza maarifa yako. Muambae kabla ya kuoana abadilike kuwa mzigo kwako,” asema mtaalamu wa mahusiano Jimmy Orwa.
Mojawapo ya zawadi bora zaidi kwa mpenzi wa mtu ni kumsaidia bila masharti yoyote kutimiza ndoto na maono yake. Hii ni kwa akina dada na kaka.
Saidia mpenzi wako kujijenga kutimiza ndoto yake na akikataa, elewa mapema huyo atakuleleta shida katika maisha ya baadaye. Safari ya mapenzi, asema Orwa, inahitaji wawili walio na maono. Bila maono, aeleza Orwa, hakuna matumaini.
“Iwapo unayeita mpenzi wako hafurahii unachothamini katika kutimiza ndoto na maono yako, busara inahitaji ujitenge naye. Mtu anafaa kuonyesha kwa vitendo kwamba anaunga mwenzake kutimiza ndoto zake maishani,” asema.
Iwapo anasita kukusaidia kuelekea malengo yako maishani na ana uwezo, au anafanya hivyo shingo upande, jiulize iwapo huyo ndiye utataka kuishi naye hadi kifo kiwatenganishe. Mtu anayekuruhusu kufuatilia unachopenda kufanya maishani, iwe ni masomo, biashara, kazi au kusaidia jamii usimuache, mkumbatie hata kama hana uwezo.
Mtu anayefurahia maono yako na kukusaidia kuyaboresha kimawazo na kifedha ni johari kwako. Huyo ni mtu mnayeweza kutembea pamoja wakati wa dhiki na neema.
“Kila mtu anayependa hutaka kuona mkewe au mumewe akiwa na furaha, akiimarika kwa hekima, nguvu na kikazi. Wanaume, wasikizeni wachumba wenu wanapowasimulia ndoto zao maishani. Walio katika ndoa, kusaidia mke au mume kunahitaji muda, nguvu, juhudi, pesa na kujitolea kwako. Mtu wako anaweza kufanikisha ndoto yake maishani ukimpa usaidizi na kumtia shime,” asema mshauri wa masuala ya mahusiano Diana Kajuju.
Anasema watu wanaohujumu ndoto za wachumba wao huwa hawana nia nzuri. “ Ndoa haifai kuwa ya kuua ndoto. Ndoto ya mwanamke katika maisha yake haifai kufa akiolewa na vile vile mwanaume hafai kuacha maono yake akioa,: asema Kajuju.