MakalaSiasa

TUZO YA AMANI YA NOBEL: Vizingiti vinavyofifisha nafasi ya Raila kuitwaa

August 6th, 2018 Kusoma ni dakika: 3

NA FAUSTINE NGILA

MAELFU ya Wakenya kwenye mitandao ya kijamii mwezi uliopita walishindia kumpigia debe kinara wa upinzani Bw Raila Odinga kuteuliwa kuwania Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2018.

Kwa kampeni iliyoanzishwa na raia wa Uingereza Adan Ali Abdi, watumizi wa mitandao kote duniani walihamasishwa kumteua kiongozi huyo wa chama cha ODM kupitia kwa tovuti ya change.org.

Waliounga mkono juhudi hizo walisema Bw Odinga anastahili kutwaa tuzo hiyo kwa jitihada zake za kuiletea nchi hii amani na pia Sudan Kusini kwa kuwapatanisha rais Salva Kiir na mpinzani wake Riek Machar. Walisisitiza kuwa mwanasiasa huyo amepigania demokrasia na kulinda haki za kibinadamu.

Walikariri kuwa kiongozi huyo aliyekula kiapo cha kuwa rais wa wananchi kisha kukubali kuingia kwa mwafaka wa kisiasa na Rais Uhuru Kenyatta, amebadilisha maisha ya mamilioni ya Wakenya kwa kujinyima uhuru na kupigania mageuzi na kuondoa utawala wa kiimla.

Bw Ali, alieleza jinsi Bw Odinga amekomboa taifa hili kutoka utawala wa kidikteta na kuleta demokrasia ya vyama vingi.

“Wakenya bado wangekuwa kwa giza bila juhudi za Bw Odinga. Kiongozi huyu amesaidia kuletea nchi yake amani wakati wa machafuko, na pia kuhusika moja kwa moja kusaka amani katika mataifa mengi ya Afrika,” aliandika kwenye intaneti.

Wafuasi wa kinara huyo wa upinzani waliweka linki ya uteuzi huo kwenye mitandao mingi ya kijamii inayomilikiwa na Bunge la Kitaifa na serikali za kaunti humu chini.

Wanafunzi wa vyuo vikuu pia hawakulala wakimfanyia Bw Odinga kampeni wakisema wakati wake sasa umefika kunyakua tuzo hiyo.

Majuzi, wakati akihojiwa katika runinga ya Citizen, kampeni hiyo iliibuka tena, huku Wakenya kwenye Twitter wakisema Bw Raila amefanya mambo mengi kuinusuru nchi hii licha ya kutobahatika kuwa rais.

Kila Mkenya atakubali kuwa mwanasiasa huyo alizuia umwagikaji zaidi wa damu hapo 2007/2008 alipokubali kugawana mamlakana na aliyekuwa rais, Mwai Kibaki, na kuokoa uchumi wa Kenya alipotia saini mwafaka na rais Kenyatta mapema mwaka huu.

Kila mwaka, wasomi, wanasayansi na washindi wa awali huwasilisha maombi yao wakilenga kushinda tuzo hiyo.

Lakini je, Bw Odinga anastahili kuteuliwa kwa tuzo ya Nobel ya amani? Ni kanuni zipi anafaa kufuata? Masharti ya uteuzi ni yapi? Ametimiza yote?

Kulingana na kanuni za Wakfu wa Nobel, uteuzi wa Tuzo ya Nobel kitengo cha Amani unakubaliwa iwapo umewasilishwa na mtu ambaye ni:

  • Mbunge, waziri serikalini au rais wa nchi.
  • Mwanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki na Mahakama ya Kudumu ya Suluhu ya The Hague
  • Mwanchama wa taasisi ya kimataifa ya Institut de Droit International
  • Mhadhiri chuoni, profesa wa historia, sayansi ya jamii, sheria, filosofia au dini. Pia mkurugenzi wa chuo kikuu au mkurugenzi wa taasisi ya utafiti kuhusu Amani na pia taasisi za sera za kimataifa.
  • Mtu ambaye awali alishinda Tuzo ya Nobel
  • Mwanachama wa bodi ya shirika au kampuni ambayo awali ilishinda Tuzo ya Nobel
  • Wanachama wa sasa na awali wa Kamati ya Nobel ya Norway
  • Washauri wa awali wa Kamati ya Nobel ya Norway

Wawaniaji wa tuzo hii ni watu au mashirikia yaliyoteuliwa na watu waliotimu vyeo vilivyotajwa hapa juu. Hauruhusiwi kujiteua mwenyewe.

Ukitazama kanuni hizi nane, hakuna yoyote ambayo Bw Odinga ametimu. Pia ukitazama waliokuwa wakimteua, pia hawatoshi mboga.

Wawaniaji hupigwa msasa na Kamati ya Nobel ya Norway ambayo ina wanakamati watano waliochaguliwa na bunge la kitaifa la Norway, na tuzo hiyo huandaliwa jijini Oslo na wala si jijini Stockholm, Sweden ambapo tuzo za Nobel katika Fisikia, Kemia, Udaktari, Fasihi na masomo ya Uchumi huandaliwa.

Uwasilishaji wa teuzi

Kamati ya Nobel ya Norway imeweka fomu ya uteuzi mtandaoni katika tovuti ya https://www.nobelpeaceprize.org/Nomination

Siku ya mwisho ya kuwasilisha uteuzi ni Januari 31 kila mwaka, saa sita usiku saa za Ulaya. Teuzi zinazowasilishwa baada ya tarehe hiyo huwekwa kwa orodha ya mwaka ujao.

Barua au baruapepe ya kuthibitisha wasilisho lilipokewa hutumwa kwa mwaniaji baada ya miezi kadha.

Mchakato wa uteuzi

Septemba – Kamati ya Nobel ya Norway hujiandaa kupokea teuzi.

Februari – Orodha ya waliowasilisha maombi ya kuteuliwa hutumwa kwa Kamati ya Nobel ya Norway jijini Oslo Februari mosi. Katika miaka ya hivi majuzi, kamati hiyo imepokea majina 200 kwa Tuzo ya Amani ya Nobel.

Februari – Machi – Kamati ya Nobel hupitia kazi ya kila mwaniaji na kuandaa orodha fupi.

Machi – Agosti – Washauri katika vitengo mbalimbali hupitia kazi za waliosalia kwa orodha huku wakitoa ushauri kuhusu walio bora zaidi.

Octoba – Huu ndio mwezi ambao washindi huchaguliwa. Mwanzoni mwa mwezi huu, kamati hiyo huchagua mshindi kwa kupiga kura ya siri. Anayeibuka na kura nyingi hushinda. Jina la mshindi sasa hutangazwa kwa umma.

Desemba – Washindi wa Tuzo ya Nobel hukabidhiwa tuzo rasmi katika sherehe ambayo huandaliwa Desemba 10 jijini Oslo. Tuzo hiyo huwa ni nishani ya Nobel na chati cha stashahada pamoja na stakabadhi inayothibitisha mshindi amepewa tuzo.

Kwa miaka 50, kanuni za Wakfu wa Nobel huzuia majina ya wawaniaji kutangazwa kwa umma. Majina ya wawaniaji, waliowateuwa, uchunguzi na maoni kuhusu tuzo hiyo husalia siri kuu. Siri hii hutobolewa baada ya miaka 50.

Ni wazi kuwa ingawa Wakenya na wafuasi wengine wa Bw Raila duniani wangependa atuzwe mwaka huu, yeye mwenyewe hajatimiza kanuni zinazohitajika, na hata kama angetimiza basi ashapitwa na muda ambao jina lake lilifaa kuwasilishwa kwa Kamati ya Nobel ya Norway.