Makala

Uchanganuzi: Hisia za Trump kuhusu nchi za Afrika zinajulikana, hivyo haya ndiyo ya kutarajiwa…

Na DOUGLAS MUTUA November 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

AMERIKA – na kwa kiasi fulani, dunia – itakuwaje chini ya utawala wa Rais Donald Trump katika muda wa miaka minne ijayo?

Swali hili linaafiki kwa sababu kuna utani unaosema kwamba Amerika ikipiga chafya, dunia inapata mafua. Utani huo unaashiria kiwango cha ushawishi wa taifa hilo tajiri na lenye nguvu zaidi kwa dunia nzima.

Trump ataanza kipindi chake cha pili na cha mwisho Januari 20 mwakani, hivyo tangu sasa hadi wakati huo tutashuhudia shughuli nyingi za kuunda serikali mpya katika kambi yake.

Hivi tumefikaje hapa? Trump, mwaniaji wa chama cha Republican, aliibuka mshindi katika uchaguzi uliofanyika Jumanne kwa kumshinda Makamu wa Rais wa sasa, Bi Kamala Harris.

Ilikuwaje Trump, mtu mkorofi ajabu, akashinda ushaguzi katika nchi ya wastaarabu? Ustaarabu, ukiwekwa katika mizani dhidi ya maslahi binafsi ya watu kama vile rangi, mfumko wa bei za bidhaa, ushawishi wa kisiasa na kadhalika, hauna lake.

Kimsingi, Wazungu wamelichukulia kwa uzito mno suala la uhamiaji, hivyo wamejitokeza kukomboa nchi yao kutoka kwa wahamiaji kwa ajili ya usalama wao wenyewe.

Walihisi kwamba wahamiaji kutoka Afrika, Asia, kusini na katikati ya bara la Amerika, wameongezeka mno nchini Amerika, wingi wao ukatishia nafasi ya kipekee iliyofurahiwa na Wazungu kwa muda mrefu.

Wazungu wasioficha hofu yao kwamba idadi yao inapungua sana kutokana na ongezeko la wahamiaji huuliza kweupe:

“Ingekuwa wewe, ungehisije ukiona jamii yako ikipoteza nguvu za kisiasa, kijamii na kiuchumi kwa kuzidiwa idadi na wageni?”

Mtizamo huo pekee unatosha kuwapa wengi hofu, wakajitokeza kimya-kimya na kumchagua mwenzao anaowatetea bila kificho, na kwa sasa mtu huyo ni Trump.

Wahamiaji tunaoishi Amerika tumeshuku kwa muda kwamba Trump ana wafuasi wengi sana wasiotangaza wazi wanamuunga mkono kwa sababu wanaaibikia mambo ya kibaguzi na chuki ambayo anasema hadharani.

Tatizo lao si kwamba anayasema, huenda hata wengi wao huyasema kisiri nyumbani. Kosa la Trump ni kuyasema wazi, watu wasiopaswa kuyasikia wakajua wanachukuliwaje.

Hata hivyo, Amerika ina Wazungu wengi ambao si wahafidhina wa aina ya Trump, kwa hivyo hatuwezi kuwahukumu wote kwa mpigo.

Wapo pia wahamiaji, hasa Waafrika, wanaomchukulia Trump kuwa Mkristo mwenzao na hivyo wanamuunga mkono kwa kuamini sera zake zinaendana na imani yao.

Suala ambalo limetokea kumhini Kamala zaidi ni la Uchumi, hasa kutokana na mfumko wa bei za bidhaa. Waamerika wameshindwa kabisa kuelewa kwa nini wanaambiwa uchumi unanawiri, fursa za kazi zinaongezeka, ila bidhaa za kimsingi ni ghali.

Bidhaa ambazo watu hununua kila siku kama vile vyakula na mafuta ya gari zinauzwa kwa bei za juu, hivyo zinawaumiza kila siku. Ungaliwasadikishaje kwamba maisha yangalikuwa bora chini ya utawala wa Harris, ambaye ni makamu wa rais wa utawala wa sasa unaowatesa?

Lipo pia suala la jinsia. Wamarekani wengi, hasa wanaume, bado hawajakubali kwamba wanaweza kuongozwa na mwanamke. Angalau wamedhihirisha hili mara mbili kwa kumkataa Kamala na Bi Hillary Clinton aliyeshindwa na Trump mnamo mwaka 2016.

Jingine pia ni ukweli kwamba Kamala alikuwa na takriban siku 100 pekee za kufanya kampeni baada ya Rais Joe Biden kushinikizwa kutowania urais tena kutokana na uzee.

Si siri kwamba wanachama wengi wa Democrat hawakufurahishwa na hatua ya kumpa Kamala tiketi ya chama moja kwa moja bila kufuata mchakato mzima wa mchujo. Wanaamini mchakato huo ungefuatwa, Kamala hangekuwa mwaniaji wa chama chao.

Pia, utawala wa Biden, ambao Kamala hawezi kujitenga nao, uliwaudhi Waarabu wengi walio raia wa Amerika kwa kutoishinikiza Israel kumaliza vita dhidi ya Lebanon na Ukanda wa Gaza.

Ingawa wengi hawakumchagua Kamala wala Trump, uamuzi wao wa kutofungamana na upande wowote ulimwathiri zaidi Kamala kwa kuwa, kikawaida, wao ni wafuasi wa chama cha Democrat.

Katika ulimwengu wa demokrasia, hakuna kura inayopotea, iwe imepigwa au la. Hii ina maana kwamba ukisusia uchaguzi badala ya kumchagua mwaniaji wako, unamchagua mpinzani wake.

Nimeuliza utawala wa Trump utaiathiri dunia namna gani. Afrika ijiandae kubaguliwa. Trump aliwahi kusema kuwa mataifa ya Afrika na mengine yanayoendelea ni mashimo ya mavi! Ana haja gani kuyatakatisha na kuhusiana nayo wakati huu?

Mataifa wanachama wa muungano wa kijeshi wa NATO nayo yanapaswa kujiandalia matusi, dharau na uchokozi usio na sababu kutoka kwa Trump. Aliyavuruga alipokuwa rais kati ya mwaka 2017 – 2020.

Atajaribu kuuvunja muungano huo au kuyazuia mataifa ya mashariki mwa Uropa kujiunga nao. Baadhi ya mataifa hayo yanatamani sana kuwa wanachama wa NATO ili yalindwe dhidi ya vitisho na dhuluma za Urusi.

Huenda Urusi ikashinda vita dhidi ya Ukraine kwa sababu Tump ni rafiki wa Rais Putin wa Urusi. Msaada wa kijeshi ambao Amerika imekuwa ikiipa Ukraine utakatizwa kuanzia mwaka ujao.

Huenda raia wa mataifa ya Kiarabu wakazuiwa kuingia Amerika. Anachohitaji kufanya Trump, na alikifanya alipokuwa rais mara ya kwanza, ni kutoa amri ya rais siku moja tu na basi!

Ataanzisha tena vita vya kiuchumi dhidi ya Uchina, Mexico na mataifa mengineyo, ambavyo vitaathiri Mwamerika wa kawaida pakubwa kwa kuwa bidhaa nyingi zinazouzwa Amerika huzalishiwa huko.

Waamerika nao pia watakipata kwa kuwa Trump ameapa kuwaadhibu mahasidi zake wa kisiasa. Hili litawezekana kwa sababu Mahakama ya Upeo ya Amerika ilisema kuwa rais hawezi kushtakiwa kwa makosa anayofanya akiwa mamlakani.

Miongoni mwa hatua za kwanza kabisa ambazo Trump atachukua akiingia ofisini ni kujisamehe makosa ambayo kwayo amekutwa na hatia, sikwambii na kuwasamehe marafiki zake waliofungwa gerezani kwa kutenda uhalifu katika harakati za kumuunga mkono.

Kwa mfano, amekuwa akisema kuwa watu waliofungwa gerezani kwa kuvamia majengo ya Bunge la Amerika mnamo Januari 6, 2020 ni mashahidi wasio na hatia. Ameahidi kuwasamehe.

Labda ni kitu kizuri kwamba Trump ameshinda; viongozi dhalimu wa mataifa yanayoendelea, ambao wangehusiana vyema na Amerika chini ya Kamala, watajiju! Raia wakiwajia juu, hawana wa kulilia.

Kwa vyovyote vile, maisha yataendelea. Mataifa na yatajifunza kujitegemea.

[email protected]