Uchoraji riziki tosha kwake
Na PETER CHANGTOEK
AMEKUWA akishughulika na shughuli ya uchoraji kwa muda wa mwongo mmoja sasa. Licha ya kuishi karibu na mtaa wa mabanda wa Mukuru, hilo halijamzuia kulifanya analolijua zaidi- sanaa ya uchoraji.
Lazaro Tumbuti, ambaye anasakini katika mtaa wa Lunga Lunga, eneo la Viwandani, jijini Nairobi, amekuwa akishughulika na sanaa hiyo, anayosema imekuwa kitega uchumi kwake kwa muda mrefu.
“Mimi ni msanii na mara nyingi hushughulika na sanaa ya uchoraji. Mara nyingi hufanya hivyo katika mtaa wa Mukuru, Viwandani,” adokeza Tumbuti.
Mchoraji yuyo huyo pia ni mwnachama wa kundi linalojulikana kwa jina Wajukuu Arts Project, linaloziendesha shughuli za usanii katika eneo la Viwandani, Nairobi.
Kundi hilo limekuwa likishughulikia shughuli mbalimbali za sanaa. Aidha, limekuwa likiwapa mafunzo watoto kuhusu masuala mengi ya sanaa.
Msanii huyo hutegemea shughuli hiyo kujiruzuku. “Mimi hutegemea kazi hii kupata riziki,” asema msanii huyo mwenye umri wa miaka 32.
Kwa mujibu wa msanii huyo ni kuwa, kundi lilo hilo la Wajukuu Arts Project lina wanachama thelathini na wawili (32), japo wale wanachama ambao hushughulika na uchoraji ni wanane (8) tu.
Kundi hilo limejitahidi kwa jitihada za mchwa na kuununua ukumbi ambao huutumia kuziendesha shughuli za sanaa.
“Tuliandaa maonyesho ya bidhaa na kufanikiwa kupata pesa tulizotumia kununua ukumbi. Hatukodishi ni wetu,” afichua msanii huyo, akiongeza kuwa wao pia hujitolea kuwapa mafunzo watoto kuhusu masuala mbalimbali.
Tumbuti pamoja na wenzake hupata fedha kutoka kwa mauzo ya bidhaa zao. Pia, kwa wakati mwingine wao huwapata wageni kutoka ughaibuni, ambao huzinunua baadhi ya bidhaa zao na kuzipeleka kwao.
Huziuza bidhaa zao kwa kutumia mitandao ya jamii kama vile Facebook na WhatsApp, miongoni mwa majukwaa mengineyo.
Kwa wakati mwingine wanachama hao hupata msaada wa fedha kutoka wasamaria wema au wahisani, hususan wanapozuru eneo ambalo wasanii hao hao huwafunzia watoto.
“Wao hutusaidia kifedha au kupitia kwa elimu, au hata kutupa mchango wa malighafi tunazotumia. Kwa upande wetu wasanii, sisi hutenga asilimia 20 (20%) ya fedha ambazo hutumiwa katika miradi ya watoto,” asema msanii huyo.
“Tulianzisha kundi hili mnamo mwaka 2004,” afichua Tumbuti, ambaye mbali na kufanya shughuli za uchoraji, hushughulika na shughuli za ufugaji wa sungura.
Baada ya kufunzwa na kupata ujuzi wa kutosha katika nyanja mbalimbali za sanaa, watoto hao hujiunga na kundi hilo la Wajukuu Arts project.
Tumbuti na wenzake huzichukua bidhaa zao katika maonyesho mbalimbali ili kuziuza. Anaongeza kuwa kuna maeneo ambayo wao hutumia kuonyeshea na kuziuzia bidhaa zao.
Msanii huyo anasema kuwa wao huziuza bidhaa zao kwa bei tofauti tofauiti, kwa kutegemea ujumbe ulioko kwenye michoro hiyo. Hata hivyo, bei zaweza kushushwa kulingana na maelewano baina ya mteja na mwuzaji.
Anasema kuwa bidhaa zao huuzwa kuanzia Sh20,000 kila moja. “Bei zinaweza kupanda hadi Sh30,000, ikitegemea bidhaa zenyewe,” aongeza msanii huyo.
Anafichua kuwa huchora michoro inayoakisi hali halisi ya watu na matukio yanayotukia katika ulimwengu wa sasa. “Najaribu kuwaelimisha watu kuhusu yanayoendelea katika mahali tunakoishi,” adokeza.
Hata hivyo, kuna baadhi ya ndaro ambazo wamewahi kuzipitia katika shughuli zao, kama vile kukosa soko la kutegemewa. Pia, anasema kuwa malighafi wanazozitumia ni ghali.
Tumbuti anawashauri vijana kuvitumia vipaji vyao badala ya kuzitafuta ajira za afisini, ambazo kuzitafuta kunamithilishwa na kumtafuta paka mweusi kwenye giza totoro.