Makala

UDA hatarini kusambaratika Mlima Kenya sababu ya masaibu ya Gachagua

Na MOSES NYAMORI, CHARLES WASONGA October 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MASAIBU yanayomzonga Naibu Rais Rigathi Gachagua yameibua changamoto mpya kwa chama cha United Democratic Alliance (UDA) kuelekea chaguzi zake za mashinani.

Uhasama kati ya Rais William Ruto na Bw Gachagua huenda ukaathiri maandalizi ya shughuli hiyo katika ngome ya UDA ya Mlima Kenya, ambako Naibu Rais anahusudiwa pakubwa.

Chama hicho kilikuwa kimepanda kuendesha chaguzi za mashinani mwezi ujao wa Novemba kufuatia agizo la Afisa ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) kwamba zikamilishwe ndani ya siku 180.

Awali, UDA ilikuwa imeratibu kwamba chaguzi hizo zifanyike Agosti lakini ikaziahirisha baada ya kulipuka mwa maandamano ya kupinga Mswada tata wa Fedha wa 2024 mwezi Juni mwaka huu.

“Kwa kuzingatia taratibu za uongozi bora na wajibu wa afisi hii, chama cha UDA kinaagizwa kukamilisha chaguzi za viongozi wake haraka iwezekanavyo lakini sio siku 180 baada ya kutolewa kwa barua hii,” Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu akasema kupitia barua kwa UDA Agosti mwaka huu.

Kando na UDA, chama cha Orange Democratic Movement (ODM) chake kiongozi wa upinzani Raila Odinga pia kinapanga kuendesha chaguzi zake za mashinani kuanzia Novemba mwaka huu.

Vyama hivyo, vinadaiwa kupania kubuni muungano kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 tayari vinashirikiana katika serikali ya sasa.

Mkutano wa Kamati Kuu ya Usimamizi (CMC) ya ODM ulioongozwa na Bw Odinga mwezi Septemba 2024, uliagiza Kamati ya Kitaifa ya Kushirikisha Chaguzi (NECC) kuanza maandalizi ya chaguzi za mashinani.

“Kwamba NECC imeagizwa kuanza maandalizi ya chaguzi za mashinani, zilizoahirishwa, katika mwezi wa Novemba,” akasema Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna kwenye taarifa kwa wanahabari baada ya mkutano huo.

ODM imefanya mabadiliko katika kamati hiyo ya NECC kwa kumteua Hamida Kibwana kuchakua nafasi ya Beatrice Askul, aliyeteuliwa Waziri wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Ustawi wa Kikanda.

Taifa Leo imeelezwa ODM inapanga kukamilisha chaguzi hizo za mashinani kisha iandae Kongamano la Kitaifa la Wajumbe kuchagua viongozi wa kitaifa mnamo Februari 2025.

Uchaguzi huo wa kitaifa utafanyika baada ya matokeo ya uchaguzi wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Mataifa (AUC) ambao Bw Odinga ni mmoja wa wawaniaji wake.

Bw Odinga amemteua Gavana wa Kisumu Profesa Anyang’ Nyong’o kuwa kaimu kiongozi wa ODM akielekeza juhudi zake katika kampeni za AUC.

Mwenyekiti wa NECC Emily Awita aliambia Taifa Leo kuwa kamati yake itakutana hivi karibuni kuandaa ratiba ya chaguzi hizo.

Naibu Kiongozi wa ODM na Seneta wa Vihiga Godffrey Osotsi alisema kamati ya CMC iliagiza kuwa chaguzi za mashinani zianzie katika ngazi za vituo vya kupigia kura hadi maeneo bunge.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) katika UDA Anthony Mwaura aliambia Taifa Leo kuwa bodi hiyo itaandaa mkutano kuweka tarehe mpya za chaguzi za mashinani.

“Tunarejea chaguzi za mashinani mwezi Novemba 2024 baada ya shule kufungwa. Tunapanga kukamilisha chaguzi hizo kufikia Desemba 15,” akasema.

Chama cha UDA kilikuwa kimeanza awamu kwanza  ya chaguzi zake Aprili 2024.

Lakini  kikalazimishwa kuzisitisha baada ya kufanyika katika Kaunti za Busia na Homa Bay pekee, kati ya kaunti tano zilizotarajiwa kuzifanya chaguzi hiyo katika awamu hiyo.

Chaguzi katika ngazi za maeneo bunge katika Kaunti ya Pokot Magharibi ziliahirishwa kwa hofu ya kutokea fujo huku chaguzi katika Kaunti za Nairobi na Narok zikIsitishwa kufuatia kesi zilizowasilishwa mahakamani kuzipinga taratibu zilizotumiwa.