UDAKU: Masaibu ya Khalif Kairo ni mwiba wa kujidunga au kaletewa na mahasidi?
WANASEMA usimpige mateke mwanamume mwenzio anapokuwa yupo chini maana dunia ni mduara, leo yeye kesho wewe.
Kauli hii hakika nimeishi nayo ila kuna wakati mwingine huwa nauliza kama ni kauli hiyo ni sahihi.
Naomba nitumie huu mfano: Huyu Khalif Kairo na skendo zake za ulaghai.
Msela anasisitiza kuwa kuna watu wanaotengeneza njama za kumharibia mafanikio yake.
Kama Khalif Kairo ni mgeni kwako, acha nikupe picha. Jamaa ameondokea kuwa miongoni mwa watumiaji X maarufu nchini. Amejizolea umaarufu mkubwa Twitter kutokana na maisha ambayo amekuwa akiringisha mtandaoni.
Akiwa na miaka 28 tu, Khalif Kairo aliwaaminisha wafuasi wake zaidi ya 310,000 kuwa yeye ni milionea. Utajiri wake alisema ameupata kutokana na biashara yake ya uuzaji magari.
Lakini mbali na hilo, tabia yake ya kuringisha maisha yake ya kifahari pamoja na kutoka na wanawake wa kishua pia ilimwongezea sifa.
Mrembo Cera Imani ambaye hakuna aliyekuwa akimfahamu, alipata umaarufu baada ya kuanza kudeti jamaa. Kairo aliishi maisha ya kutamaniwa na vijana wengi. Aliwafanya wengi vijana kutamani maisha yake.
Leo hii miaka mitatu tu, biashara yake ya magari imeanguka huku akiandamwa na visa kibao za ulaghai wa magari. Wikendi hii alikamatwa tena baada ya mteja aliyekuwa anatarajiwa kupata gari aliyokuwa amelipia kutoka kwa Kairo, kuikosa baada ya msela kushindwa kufikisha mzigo.
Mkufu wa Almasi
Niliona pia ex wake Cera pale Insta akihimizwa na mashabiki kuwa amrejeshee Kairo ule mkufu wa almasi wenye thamani ya Sh350,000 alionunuliwa jamaa alipompeleka mrembo huy Dubai kula bata.
Cera akajibu jamaa wala hakulipia mkufu huo, ila alirekodi video ya kuongopea eti kamnunulia.
Wapo ambao huenda watasema Cera ni mwongo, ila mimi nimeiamini kauli hiyo. Kairo hakulipia ila kwa sababu anapenda kuwaweka wafuasi wake presha ya jinsi gani kafanikiwa, ilimlazimu arekodi video aringishe.
Siwezi kumwamini baada ya kesi zote hizi za kuwalaghai wateja magari waliyolipia kisa anakosa kufikisha mzigo.
Biashara za Crypto currency
Kuna mtu TikTok anayedai kumfahamu vizuri Kairo amedai kuwa jamaa amekuwa kwenye biashara hizi haramu za Crypto Currency na Forex Trade.
Sina uhakika ila jamaa alivyosimulia, naye nimemwamini. Haiwezekani kila kitu kinamwendea kombo Kairo kama kweli kaka anafanya mambo yake wima.
Na kama umesahau, labda niwakumbushe tu, miaka miwili iliyopita Kairo alitimuliwa kwenye biashara ya magari Imports By Kairo. Kipindi anaondoka, Kairo aliposti mtandaoni na kutangaza kuwa ameamua kujiengua kama Afisa Mkuu Mtendaji wa Imports By Kairo na pia kaiachia kampuni hiyo hisa zote alizokuwa akimiliki pale. Kairo alisema amefikia uamuzi huo kutokana na sababu za kibinfasi.
Hisa za kampuni ya ‘Imports By Kairo’
Kauli hiyo ilibaki na mashimo kibao. Hivi wapi ulisikia mtu kawekeza halafu ghafla kaamua kuachia hisa zake zote tena kwenye kampuni ya uuzaji magari. Huu si uwongo tu. Kwa jicho la tatu, Kairo hakuwa na hisa zozote kwenye Imports By Kairo.
Kampuni hiyo ilijibu kwa mpigo na kukanusha kuwa Imports By Kairo ipo chini ya uongozi mpya ikisisitiza kuwa hamna kitu kama hicho.
Ilikanusha pia kuwa Kairo aliwahi kuwa Afisa Mkuu Mtendaji wake.
Ni wazi Kairo hajanyooka kama ambavyo ameishi kutuaminisha.