UFUGAJI: Umuhimu wa maji kwa kuku
Na SAMMY WAWERU
KUKU wanafugwa kwa minajili ya ama mayai au nyama.
Ufanisi katika ufugaji wa ndege hawa unaegemea vigezo mbalimbali.
Kulingana na wafugaji waliofanikiwa, ujenzi wa makazi yake unapaswa kutiliwa maanani. Wanasema ndege hawa wa nyumbani wawe na nafasi ya kutosha kuwaruhusu kutembea na hata kucheza.
Kuku mmoja anakadiriwa kutengewa nafasi ya futi mbili kwa mbili mraba, kwa mujibu wa maelezo ya Bw Okuta Ngura, mtaalamu tajika wa masuala ya ufugaji nchini hasa kuku.
“Kizimba kidogo chenye kuku wengi huchangia usambaaji wa magonjwa. Kinyesi chao kina gesi ya Urea, ambayo ikitangamana na maji, itakuwa hatari katika afya ya kuku,” anafafanua Bw Okuta ambaye pia ni mwasisi wa Ngura Poultry Care, shirika la kibinafsi linalotoa mafunzo ya ufugaji wa ndege.
Mtaalamu huyu anasema makazi hayapaswi kusongamana kuku, ili kuepuka changamoto za aina hiyo.
“Kuta nazo ziwe na mianya inayoruhusu gesi kuondoka na kuruhusu Oxijeni kuingia,” anashauri Bw Okuta.
Muhimu zaidi kutilia mkazo ni usafi. Mfugaji anahimizwa kuhakikisha kizimba ni safi kila wakati, ambapo kinapaswa kufagiliwa kila siku asubuhi.
Ili kukabiliana na vimelea hatari kwa kuku kama vile viroboto, mkulima unashauriwa kupulizia dawa dhidi ya wadudu hususan baada ya kufagia makazi.
“Mwanzo, kuku waondolewe. Kuna dawa tofauti za shughuli hiyo, hasa za ungaunga, imwagiliwe sakafuni na ukutani na sehemu wanakojificha,” anaeleza Elizabeth Mwangi, mfugaji Nairobi.
Lishe kwa kuku iwe na madini kamilifu, kiwango cha Protini kikihimizwa kuwa cha juu. Nyama na mayai, ni mazao yaliyosheheni Protini, hivyo basi madini hayo kwenye chakula chake yawe mengi. Madini mengine ni; Vitamini na Wanga, miongoni mwa mengine.
Isitoshe usafi katika chakula na maji uwe wa hadhi ya juu. “Katika jitihada zangu kufuga kuku nimegundua usafi kwa chakula na maji unachangia ufanisi. Vifaa vya lishe na maji viwe safi kila wakati,” asema Bi Lucy Makato, mfugaji wa kuku wa mayai na nyama eneo la Mumbi, kaunti ya Kiambu.
Kulingana na mfugaji huyu la muhimu tena zaidi kuzingatia ni kunywesha ndege hawa maji kwa wingi. “Kuku hawana kipimo cha mlo, hula kila wakati. Wanapaswa kuwa na maji usiku na mchana,” asema Lucy.
Kuku hawana sehemu ya haja ndogo, na huitoa kupitia kinyesi. Bw Okuta Ngura anasema ili kukiwezesha kutoka bila ugumu wowote kuku wanafaa kutiliwa maji kwa wingi.
Mdau huyu anaeleza kwamba visa vingi vya kuku kufariki kiholela pia vinachangiwa na ukosefu wa maji.
“Ni hatari kwa ndege hawa kukosa kiungo hiki muhimu. Ili chakula kisagige upesi, wanahitaji maji ya kutosha. Wanapoyakosa kinyesi huwa vigumu kutoka, suala ambalo husababisha maafa,” anatahadharisha Ngura.
“Kuku hula chakula kigumu kama vile punje za mahindi, mchele na chakula chao maalum, aina ya unga. Ni chakula ambacho wakikosa maji mwilini hakitayeyuka kwa shughuli muhimu ya usagaji (digestion),” anafafanua zaidi.
Farrel Wa Muthoni, mfugaji na mtaalamu eneo la Kikuyu, Kaunti ya Kiambu, anasisitizia haja ya kukumbatia mfumo asilia katika ufugaji wa ndege hawa wa nyumbani
Ili kudhibiti magonjwa, anapendekeza kwenye maji watiliwe mshubiri na pilipili.
Mshubiri au Aloe vera ni aina ya mmea wa kienyeji unaoaminika kutibu magonjwa anuwai; na baadhi ya wakulima wamekuwa wakiutumia katika kutibu kuku.
Bw Farrel anasema ni mfumo ambao kwake yeye ameuthibitisha kufanya kazi.
“Nimezoesha kuku wangu Aloe Vera na pilipili hoho. Huongeza kinga (immune) kukabiliana na magonjwa ibuka kwa kuku,” anaeleza Farrel.
Mchanganyiko huo huutia kwenye maji, ambapo kuku huunywa.
Mfugaji huyu pia anatilia mkazo ndege hawa kunyweshwa maji kila wakati na kwa wingi.