Uhuru awatuza waliobwagwa uchaguzini
Na WANDERI KAMAU
WANASIASA waliotemwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2017 ni miongoni mwa watu ambao wameteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta na mawaziri wake kuhudumu katika nyadhifa kuu kwenye mashirika mbalimbali ya serikali.
Bali na nyadhifa nyingi kukabidhiwa wanasiasa waliofeli kwenye uchaguzi uliopita, kigezo kingine kilichojitokeza ni vijana kuendelea kukaa kwenye baridi.
Teuzi hizo pia zinazua maswali kuhusu kujitolea kwa Rais Kenyatta na serikali yake katika kuheshimu Manifesto ya Jubilee ambayo inasema kuwa teuzi za serikali zitazingatia uwazi, taaluma, usawa wa kimaeneo na jinsia.
“Tunaamini katika mfumo mpya wa kisiasa ambao utahakikisha kwamba masuala ya kitaifa yanapewa kipao mbele kuliko mtu binafsi ama jamii anakotoka mtu. Tumejitolea kuanzisha Kenya Mpya inayozingatia uwazi na taasisi mahsusi zitakazowahudumia Wakenya bila kuwabagua kwa namna yoyote ile,” inaeleza Manifesto ya Jubilee.
Wanasiasa walioanguka katika eneo la Ukambani wamenufaika zaidi kwenye teuzi hizo. Kati yao ni Kalembe Ndile ambaye chama chake cha Tip Tip kilimezwa na Jubilee mnamo 2017, Wavinya Ndeti ambaye alishindwa na Alfred Mutua kwenye ugavana wa Machakos, Joe Mutambu aliyeshindwa kiti cha ubunge Mwingi ya Kati na Agnes Muthama aliyebwagwa katika kiti cha uwakilishi wa wanawake Machakos.
Uteuzi wa Bi Ndeti, ambaye aligombea kwa tiketi ya Wiper, unaonyesha mkono wa kinara wake Kalonzo Musyoka, ambaye siku za majuzi ameegemea upande wa Jubibee, katika kushawishi uteuzi wake.
Magavana walioangushwa David Nkedianye (Kajiado) na Joshua Irungu (Laikipia) pia nao walikumbukwa sawa na waliokuwa wabunge Gonzi Rai (Kinango), Zebedeo Opore (Bonchari), Joseph Lekuton (Laisamis), Alfred Khangati (Kanduyi), Joyce Lay (Taita Taveta), Moses Ole Sakuda (Kajiado Kaskazini), Jacob Macharia (Molo) na Abu Chiaba (Lamu Mashariki).
Baada ya kuwa kwenye baridi kwa muda mrefu, Bw Ndile aliteuliwa kuwa mwanachama wa Halmashauri ya Ustawishaji wa Huduma za Maji za Mito Tana na Athi (TAWDA) sawa na Bi Muthama.
Naye Bi Ndeti aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa Taasisi ya Maji ya Kenya (KEWI), Bw Mutambu kuwa mwenyekiti wa Mamlaka ya Raslimali za Maji (WRA) huku Bw Irungu akiwa mwenyekiti wa Bodi ya Kusimamia Huduma za Maji (WSRB).
Bw Nkedianye aliteuliwa mwenyekiti wa Mamlaka ya Ukusanyaji na Uhifadhi wa Maji (NWHSA), Bw Rai mwenyekiti wa Shirika la Usimamizi wa Shughuli za Uvuvi (KFS) huku Bi Lay akiteuliwa mwanachama wa Hazina ya Sekta ya Maji (WSTF).
Waziri wa Utalii, Najib Balala naye alimteua ndugu yake, Abdul Hakim Balala kuwa mwanachama wa Bodi ya Hazina ya Utalii (KTF).
Kufuatia teuzi hizo, Rais Kenyatta na mawaziri wake wamekosolewa pakubwa kwa kutowajumuisha vijana kwenye vyeo hivyo.
“Teuzi hizo si taswira nzuri hata kidogo kwa Rais Kenyatta, hasa anapolenga kuimarisha matumaini ya Wakenya katika utawala wake,” alisema Wakili Ndegwa Njiru, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.
Kwenye kampeni zake 2013 na 2017, mojawapo ya misingi mikuu ya kampeni ya Rais Kenyatta na Naibu Rais William Ruto ilikuwa ni kubuni nafasi zaidi za ajira kwa vijana na kuzingatia taaluma na uwazi katika teuzi za serikali.
Mnamo Desemba, Rais Kenyatta alijitetea vikali baada ya kulaumiwa kwa kumteua Makamu wa Rais wa zamani, Moody Awori kama mwanachama wa Bodi ya Hazina ya Michezo, Sanaa na Ustawishaji wa Kijamii. Bw Awori ana umri wa miaka 91.
Hata hivyo, Rais Kenyatta alijitetea vikali, akiwalaumu vijana kwa kuwa wafisadi wanapoteuliwa katika nafasi kuu serikalini.
“Ni heri nimteue mzee kama huyu ikiwa atalinda fedha za kuwasaidia vijana zisifujwe,” akajitetea.