• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
Uhuru sasa aonywa kuhusu uwezo wake kiushawishi Mlima Kenya

Uhuru sasa aonywa kuhusu uwezo wake kiushawishi Mlima Kenya

Na MWANGI MUIRURI

RAIS Uhuru Kenyatta ameonywa kuwa msimamo wake kuwa yeye ndiye atatoa mwelekeo wa urithi wa urais mwaka 2022 kwa jamii za Mlima Kenya kuwa ni hatari.

Ameonywa kuwa akumbuke yeye mwenyewe alikuwa mradi wa Rais Mstaafu Daniel Moi mwaka wa 2002 ambapo Moi alichukua maamuzi ya kusaka mrithi, lakini juhudi hizo zikagonga mwamba.

Mbunge wa Kikuyu, Kimani Ichung’wa ameonya kuwa hatari kuu katika hesabu ya Rais Kenyatta ni kuwa anajihisi kama aliye maarufu zaidi Mlima Kenya kiasi kwamba “hakuna mwingine aliye huru kukaidi.”

“Rais Kenyatta hana habari kwamba eneo la Mlima Kenya limejaa ukaidi kwa uongozi wake na sio suala la kufichika kwamba huenda ajipate bila sauti ya kutoa mwelekeo, na akiwa nayo, huenda ikawa hafifu,” anasema Ichung’wa.

Kwa upande wake, aliyekuwa Gavana wa Kaunti ya Bomet, Isaac Ruto anaonya kuwa jamii za Mlima Kenya huenda zikajipata zimetengwa kwa pakubwa na jamii zingine ikiwa hesabu ya Rais Kenyatta itatibuka.

“Kwa sasa sio siri kwamba mrengo wa Naibu Rais, William Ruto umeanza kuchukua tahadhari kuu kuhusu urithi wa 2022,” anasema Isaac Ruto.

Anasema kuwa kuna ile ahadi ya Rais Kenyatta kwa DP Ruto kuwa “mimi kuanzia 2013 nitasaka kuwa Rais kwa miaka 10 na kisha wewe uendelee kwa miaka mingine 10.”

Anasema kuwa kwa sasa Rais anaonekana waziwazi kuwa licha ya wengi katika eneo la Mlima Kenya kuchukulia ahadi hiyo kwa uzito, yeye ameanza kuonekana kuwa na mawazo mengine ya kuunga kwingine katika urithi huo.

“Tusemezane ukweli sasa: Rais Kenyatta anaonekana waziwazi kuwa anapanga njama ya kusaliti ahadi yake kwa Naibu Rais Ruto. Nasi tukiwa wanaofuatilia matukio haya kwa dhati tumemuonya DP Ruto achukue tahadhari kuu. Ikiwa hatakuwa na Plan B ya kujinasua kutoka usaliti huo, basi atajiingiza kwa mtego hatari wa kufeli na kutengwa katika siasa hizo za urithi,” anasema.

Katika hatari hiyo, Isaac Ruto anamuonya DP Ruto kuwa kwa sasa “unafaa kuwa unachumbia jamii nyingine kubwa iliyo na kura nyingi.”

Anamshauri ajipange kisawasawa kuziba pengo la “Mlima Kenya kuhamishwa kutoka kwako.”

Ni hesabu hiyo ambayo inaweza ikakanganya Mlima Kenya kwa kiwango kikuu kulingana na wadadisi.

Njia panda

Mwanasiasa mkongwe wa Kaunti ya Murang’a, Paul Mwangi Gichia Kamau almaarufu PMG Kamau anasema “sisi wa Mlima Kenya tunafaa tuwe tayari kwa lolote katika siasa hizi.”

Anateta kuwa kwa sasa eneo la Mlima Kenya limo katika njia panda katika hesabu ya 2022.

“Rais anasema kuwa anataka kuweka msingi wa amani kwa miaka 50 ijayo kuwa jamii za Mlima Kenya zitapata amani ya kufanya biashara katika kila pembe ya nchi na hivyo ni kupitia kuweka serikali ambayo itazingatia umoja wa kitaifa wala sio umoja wa jamii mbili kunyakua kiti cha Ikulu,” asema.

“Ikiwa jamii za Mlima Kenya zitamkaidi Rais jinsi ilivyo kwa sasa kukiwa na kundi la Ruto na Kieleweke linalojinasibisha na Rais mwenyewe, hesabu hiyo ya kiongozi wa nchi itatuacha pabaya sana,” anasema PMG.

Anasema kuwa kwa sasa aliye na guu mbele kukusanya kura nyingi za Mlima Kenya ni DP Ruto na ikiwa atakosa uungwaji mkono wa Rais na washirika wake, basi kuna matukio mawili ambayo yatazuka.

“Matukio hayo ni kura za Mlima Kenya kugawanyika kwa kiwango kikuu na wengi pia wasusie upigaji kura. Mlima Kenya utabakia bila mgao wa serikali au wa upinzani,” anaeleza

Anaonya kuwa kwa sasa kile kinahitajika ni Rais Kenyatta akusanye watu wake wote ndani ya chama cha Jubilee na wazungumze pamoja ili kila mbinu ya kuingia kwa debe mwaka 2022 iwe wazi.

Anasema kuwa ikiwa Rais atachagua kuendelea kunyamazisha kila sauti kupitia hasira za mkizi, vitisho na matusi, basi anaandaa hali halisi ya kufanya Mlima Kenya ujikwae pakubwa katika siasa hizo za 2022.

You can share this post!

KNCHR yapinga kupunguzwa kwa idadi ya makamishna wa IEBC

Wenye hela kugharimia mawasiliano ya wasiojaliwa kiuchumi...

adminleo