Makala

Ukataji miti unavyotishia kuangamiza miti asilia

Na PAULINE ONGAJI July 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 4

UNAPOPITIA barabara ya Kinango-Samburu kutoka Barabara Kuu ya Nairobi-Mombasa katika Kaunti ya Kwale, unakumbana na tofauti kubwa.

Kile ambacho hapo awali kilikuwa msitu wenye majani mengi, kimesalia kuwa eneo tambarare.

“Uharibifu wa msitu katika eneo hili umechangiwa na uchomaji makaa, shughuli ambazo zimeendelea kwa miongo kadhaa,” asema Bw Omar Weko, mwanzilishi wa Kenyans for Green World, shirika la kijamii la uhifadhi wa mazingira, katika Kaunti ya Kwale.

Kulingana na Bw Omar, Kaunti ya Kwale ni mojawapo ya sehemu ambazo zimekuwa zikizalisha makaa kwa wingi nchini.

Bw Omar Weko, mwasisi wa shirika la kijamii la Kenyans For Green World, katika Kaunti ya Kwale akielezea uharibifu uliosababishwa na ukataji haramu wa miti asilia. Hata hivyo, alisema kuwa wameimarisha uhamasishaji wa utunzaji mazingira na ukuzaji wa miti zaidi. PICHA | WACHIRA MWANGI

Lakini huku wasiwasi ukiendelea kuhusu shughuli ya uchomaji makaa eneo hili, kuna uharibifu mwingine mkubwa wa miti ya kiasilia, unaoendelea katika sehemu nyingine ya kaunti hii.

Agosti mwaka jana, Bw Blessington Maghanga, mhifadhi mkuu wa misitu wa shirika la uhifadhi wa misitu KFS, eneo la Kwale, alitoa tahadhari kuhusu ongezeko la uharibifu wa miti ya kiasili katika misitu na mashamba ya kibinafsi katika eneo hili.

Bw Maghanga alifichua kuwa aina mbili za miti ya kiasili – Afzelia Quanzensis, inayojulikana kama Mbambakofi na Milicia excelsa au kama inavyojulikana hapa kama Mvule – ilikuwa katika hatari ya kutoweka.

Kulingana na Bw Maghanga, uharibifu huu umeenea zaidi katika maeneo ambapo miti hii ilistawi kwa wingi.

“Hapo awali, kulikuwa na idadi kubwa ya aina hii mbili ya miti misituni hadi katika mashamba ya kibinafsi, lakini kwa sasa hali ni tofauti na huenda ikatoweka,” anaeleza.

Ekari 52.5 za msitu zilipotea ndani ya miaka 10

Kulingana na takwimu kutoka kwa Global Forest Watch, mfumo wa mtandaoni unaonakili hali ya misitu ulimwenguni, kuanzia mwaka wa 2002 hadi 2023, Kenya ilipoteza ekari 52.5 za misitu, huku Kaunti ya Kwale ikiwa miongoni mwa maeneo sita yaliyoathirika pakubwa na uharibifu wa miti, kati ya 2001 na 2023.

Ripoti ya Hali ya Kenya Water Towers ya 2018-2019 kwa Shimba Hills ilihusisha uharibifu na ukataji miti ovyo. Ripoti ilionyesha zaidi kwamba kibiashara spishi zilizolengwa ni pamoja na Milicia excels (African teak) na Afzelia quanzensis, uliendeshwa na soko tayari la mbao.

Kichocheo kikuu cha miti hiyo kukatwa kwa wingi ni thamani kubwa ya miti hii ya kiasilia, kutokana na ubora wa mbao zake.

“Mti mmoja wa mvule (jina la kisayansi: milicia excelsa) unaweza kukupatia takriban mbao zenye thamani ya Sh150,000 (dola1,159) ,” anaongeza Bw Maghanga.

Thamani hiyo pia inachochewa na na soko lililo tayari katika mataifa ya bara Asia, kutokana na sababu kwamba mbao kutoka kwa miti hii hudumu na ina uwezo wa kustahimili wadudu, na hivyo ni mwafaka katika utengenezaji fanicha za hali ya juu.

Mwaka jana, Dkt Joshua Cheboiwo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu ya Kenya (Kefri), alionyesha wasiwasi wake kuhusu biashara ya mbao inayovuka mipaka barani Afrika.

Shughuli za ukataji miti bila leseni

Kati ya masuala ambayo aliyahusisha na shughuli hii ni pamoja na wafanyabiashara wanaoendesha shughuli hii bila leseni, matumizi ya hati bandia na kutokuwepo kwa udhibiti thabiti wa biashara ya mbao mipakani.

Kulingana naye, masuala haya yalisababisha hasara kubwa katika rasilimali na mapato ya misitu. Hasa, biashara haramu ya mbao kati ya Kenya na Tanzania ilionekana kusababisha uharibifu wa hekta 70,000 za misitu, na hasara ya dola milioni 10 za mapato.

Kwa upande mwingine, Bw Maganga analaumu wakazi wa eneo hili kwa kuhusika katika biashara hii haramu ya mbao.

“Baada ya kukata miti asili kwenye mashamba yao, sasa wenyeji wameanza kutamani miti ya kienyeji katika misitu ya umma,” anaongeza.

Anasema kwamba kwa miaka mingi, maafisa wa KFS katika Kaunti ya Kwale, wamekuwa wakiwakamata wakazi wakikata miti msituni. Hata hivyo, juhudi zetu za kutaka kujua takwimu kamili ya idadi ya waliokamatwa haikufua dafu.

Hata hivyo, ingawa Bw Maghanga analaumu wenyeji kwa uharibifu unaoendelea katika misitu, kunao wanaoamini kwamba uhalifu huu unatekelezwa na watu wenye ushawishi mkubwa.

Idhini inavyohitaji kukata miti shamba la kibinafsi

Seremala akiunda kitanda kwa kutumia mti asilia wa Mvule, eneo la Lukore, Shimba Hills, Kaunti ya Kwale mnamo Februari 27, 2024. Wanamazingira wameibua hofu kuhusu ongezeko la uharibifu wa misitu katika eneo hilo. PICHA | WACHIRA MWANGI

Bw Rama Nassoro Yabo, Mwenyekiti wa Ushirikiano Welfare Group, chama cha wakataji mbao eneo hili, anafichua kwamba sio rahisi kwa wenyeji kupenya na kukata miti ya kiasili hata katika mashamba yao.

“Kwa mfano, hata kukata mti uliopandwa shambani lazima mhusika apate idhini ambapo lazima awahusishe afisa wa kilimo, mwenyekiti wa kijiji, chifu, msimamizi wa kata, na hatimaye shirika la KFS, kabla ya mtu kuruhusiwa kukata mti.”

Kwa upande mwingine, anasema, ni ngumu kupata kibali cha kukata mti wa kiasili.

Pia, uchunguzi wetu unaonyesha kwamba ni ngumu kwa mwananchi wa kawaida kuingia msituni na kukata mti wowote.

Kulingana na afisa mmoja wa chama cha uhifadhi wa msitu wa Shimba Hills, wahalifu hawa wamebadilisha mbinu.

“Hawatumii misumeno ya umeme ili kuzuia kelele, na pia hawatumii lori kubwa kusafirisha mbao. Badala yake, wao huweka magogo katika magari ya Toyota Probox ili kuzuia wasitambulike kwa urahisi. Hii ni kwa sababu hapa magari haya yanatumika kwa usafiri, na ten a ni madogo, na hivyo yanaweza kupenya katika vijinjia vidogo kwa urahisi,” aeleza.

Haya yakijiri, kando ya barabara ya Kwale kuelekea Lungalunga, ambayo ni kilomita chache tu hadi hifadhi ya Shimba Hills, kuna karakana kadhaa za mbao. Kunao wanaokiri kuwa wanaunda fanicha kwa kutumia mbao za Mvule, lakini wanasema kwamba mbao wanazotumia zinatoka katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Mti wa Mvule ulivyo hatarini kutoweka

Hata hivyo, kulingana na Dkt Willis Okumu, mtafiti katika Enhancing Africa’s Response to Transnational Organised Crime (ENACT), shirika linalokabiliana na ulanguzi wa rasilimali mipakani, mti wa Mvule umeorodheshwa miongoni mwa mimea iliyo katika hatari ya kutoweka, na hivyo biashara yake popote, ni kinyume cha sheria.

“Mtu yeyote anayedai kujihusisha katika biashara ya aina yoyote ya maliasili ambayo iko katika hatari ya kutoweka, huku akidai kwamba bidhaa anazotumia zinatoka nchi nyingine, anatekeleza uhalifu,” anaeleza.

Kwa upande mwingine, idadi ya aina hii ya miti inaendelea kutoweka katika sehemu hii. Takwimu kutoka Global Forest Watch zinaonyesha kwamba kati ya Desemba 23, 2022 na Juni 24, 2024, visa 2,494 vya ukataji miti misituni, viliripotiwa katika Kaunti ya Kwale.

Bw Maghanga anasema KFS inakabiliwa na changamoto katika utekelezaji wa sheria kali dhidi ya ukataji miti haramu.

Kwa mfano, anaeleza kwamba, chini ya Sheria ya sasa ya Utawala wa Misitu, masuala yanayohusiana na misitu mashambani yamegatuliwa.

“Sheria hii kidogo imepungukiwa kwani haidhihirishi wazi ikiwa ukataji miti unahusisha misitu tu au pia mashamba ya kibinafsi, na hapa ndipo wenyeji hupata mianya ya kukata miti.”

Sheria isiyowaadhibu wahalifu ipasavyo

Aidha, analalamika kuhusu sheria butu ambayo haiwaadhibu vilivyo wahalifu hawa.

“Kwa sasa, mkataji mti anaweza kukabiliwa na faini ya Sh2,000 (dola15.56) pekee kwa uharibifu wa mti ambao unaweza kuchukua hadi miaka 50 kukua. Katika baadhi ya matukio, wahalifu hupata hukumu ya wiki mbili mahakamani, na hali ikiwa mbaya zaidi, mhalifu wa aina hii anahukumiwa kifungo cha nje,” asema Bw Maghanga.

Hii imewavunja moyo maafisa wa KFS eneo hili, kila wanapokabiliana na uhalifu wa ukataji miti msituni.

“Maafisa wangu wamekuwa wakikata tamaa wakilinganisha juhudi walizochukua kuwakamata wahalifu, na adhabu ndogo wanayopata mahakamani.”

Kulingana na wataalamu, hii ni mojawapo ya changamoto kuu ambazo zitaendelea kuathiri juhudi za uhifadhi wa misitu, sio tu ndani ya hifadhi ya Shimba Hills, lakini pia katika misitu mingine kote nchini.

Makala haya yameandaliwa kupitia ufadhili wa Internews Earth Journalism Network.