Makala

Ukijenga uhusiano wako kwa uongo, jua unajipalilia makaa

Na BENSON MATHEKA November 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WANAUME wengi hutumia uongo kuingiza boksi vipusa wanaowamezea mate. Mahusiano mengi ya kimapenzi yamejengwa kwa msingi wa uongo.

Vipusa wanafaa kuweka kwenye mizani maneno matamu ya wanaume wanapowarushia mistari.

Unaweza kumeza chambo kisha kigeuke kuwa shubiri huku uhusiano uliotarajia ukupe raha katika maisha yako ukigeuka kuwa balaa.

Wanachokosa kufahamu wanaume wanaotumia uongo ni kuwa haudumu. Uhusiano wowote wa kimapenzi unaojengwa kwa msingi wa uongo ni sawa na nyumba iliyojengwa kwenye changarawe. Inabomoka wakati wowote kwa kuwa imejengwa katika msingi dhaifu.

“Mwanaume msema kweli ni mwaminifu, na hafichi chochote. Hata akiulizwa nini, hataficha ukweli,” asema mwanasaikolojia James Mwabili. Hata hivyo, anasema kwamba kinachofanya wanaume wengi kutumia uongo kunasa vipusa ni tabia ya kina dada.

 “Akina dada wanapenda wanaume wanaoonekana kufaulu. Hii ndiyo sababu wanaume wanaamua kudanganya wanafanya kazi kubwa au wako na mali ili kuwavutia. Tatizo ni kuwa ukweli ukibainika, uhusiano unatumbukia mashakani,” asema Mwabili.

Anasema vipusa huwa wanaamini maneno ya wanaume kwa mtizamo wa nje pekee badala ya kuthibitisha kwanza.

Anasema wanaume wanaotumia uongo ili vipusa wawakubali huwa hawana nia ya uhusiano wa kudumu.

“Ukijua mwanamume anakudanganya hata mkiwa wapenzi, ng’amua  kuwa ana nia ya kuwa nawe kwa muda mrefu. Kwa ufupi, lengo lake ni kukutumia tu kwa tamaa zake au kwa kupitisha muda,” aeleza.

Sarah Wamahiu, mtaalamu wa masuala ya mahusiano ya mapenzi anasema mtu anayetumia uongo kukuingiza boksi hakuheshimu.

“Hatari ya kwanza na ambayo watu hupuuza ni kuwa mtu anayetumia uongo ili umpende hakuheshimu. Mtu anayekuheshimu na mwenye upendo wa dhati huwa anasema ukweli. Nasikitika kuwa tajiriba yangu katika kushughulikia masuala ya mahusiano imenifunza kuwa ni wachache sana wanaosema ukweli wanaposaka wapenzi,” asema Wamahiu.

Wengi huwa wanaamua kutumia uongo baada ya vipusa kuwakataa wanapowaambia ukweli na kusahau kuwa wanaalika balaa katika maisha yao.

“Ingawa ukweli unauma, ni bora kuliko uwongo unaotimiza maslahi ya muda mfupi. Uaminifu  haufungi mtu, unamfanya kujihisi huru na kufurahia uhusiano wake akifahamu aliujenga kwa msingi imara,” asema Wamahiu.

Mwabili anasema kwamba mtu anayejenga uhusiano wake wa kimapenzi kwa ukweli huwa anathamini mwenzi wake.

“Ukweli huwa unakuza uaminifu. Huenda uaminifu usiwe rahisi nyakati fulani, lakini ni muhimu. Uaminifu hukua wakati mtu anahisi kuthaminiwa na kuheshimiwa na  kutimiza haya kunahitaji  ukweli,” asema.