IWAPO unataka kufurahia msimu wa Krismasi na mpenzi wako, usiige mtu mwingine. Cheza kama wewe kulingana na uwezo wako.
Watu hulalamika jinsi wamechoshwa na wapenzi wao msimu huu, jinsi mahanjam yamepungua kiasi cha kunyimana raha ya ndoa hata msimu huu wanaofaa kuchangamkiana zaidi.
Sherehe zinakosa ladha wachumba wanapoiga wengine badala ya kujipanga kulingana na uwezo wao.Mkijipanga vyema mtakolezana mahaba. Muhimu zaidi ni kuweka msingi wa kuaminiana.
.“Watu wasioaminiana ni watu wa kutuhumiana kila mara, na palipo na shaka mapenzi hayawezi kunoga. Muelewe mtu wako na uwezo wake wa kifedha, naye pia akuelewe. Dumisha lugha na matendo yako ya mapenzi au uyaimarishe, lakini usiige watakachofanya wapenzi wengine sikukuu hii,” asema mwanasaikolojia Eve Loko.
Aidha, anahoji kwamba wachumba hawafai kukita uhusiano wao katika joto la chumbani pekee msimu huu.“Usikubali mizizi ya uhusiano wenu iwe ni katika miereka ya chumbani pekee. Mapenzi yanahitaji kunogeshwa pia kwa njia zingine, kama vile kutembelea maeneo ya starehe mkiwa wawili tu au na watoto wenu,” aeleza.
Kisha ukifika wakati wenu wa faragha chumbani, cheza kama wewe pia umfurahishe mtu wako. Fahamu wakati mtu wako anakuhitaji ili umpe haki yake vilivyo. Kunyimana haki, ikiwemo ya tendo la ndoa na muda wa kulishana nyama ya ulimi, kunapunguza ladha ya uhusiano.
Kuna watu wanafanya wapenzi wao kusononeka kwani hawapatikana wanapowahitaji msimu huu wa Krismasi, wanawaacha katika upweke.
“Unapata mtu anazima simu au anakosa kumjulia hali mpenzi wake msimu huu anapokuhitaji mbambika naye. Ni makosa. Hata kama hujajaliwa pesa, patikana na uwe mtu mkweli.
Kwa yule anayekupenda kwa dhati, uwepo wako pekee unatosha,” Loko anashauri.Naye mtaalamu wa masuala ya mapenzi Silas Ithau anataka wachumba watumie msimu huu pia kusameheana.
“Iwapo umekuwa ukikwaruzana na mtu wako, huu ndio wakati mzuri wa kunyoosha mambo kwani shamrashamra ziko tele na mazingira ni ya raha na msamaha. Kuomba mpenzi wako msamaha sio ishara ya udhaifu, bali kiungo muhimu cha kukoleza penzi lenu,” anaeleza Ithau.
Kulingana naye, japo kupeana zawadi kumetajwa kama mbinu nzuri ya kuonyesha mapenzi msimu huu wa sikukuu, si ya pekee wala haipiku mambo madogo kushirikiana kwa shughuli za nyumbani.
“Mwanamume anayesaidia mkewe kwenda kununua vitu duka la jumla, kumsindikiza saluni, kutayarisha watoto na kupika atafurahia mapenzi ya kuridhisha msimu huu kuliko anayempa zawadi ya kifahari.
Ni raha sana kumshukuru mtu wako kwa kukuchagua wewe tu kati ya wengine wote, na anakupa mapenzi bila masharti mwaka mzima,” asema.
Mjuzi huyo wa masuala ya mapenzi asisitiza mambo madogo ambayo watu hupuuza ndiyo hukoleza raha msimu huu wa sherehe.