UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Changamoto za kutumia lugha ya kigeni katika kuwafundishia wanafunzi shuleni
Na MARY WANGARI
WANAFUNZI na wafuatiliaji wengine, jinsi tulivyojifunza kipindi cha wiki jana ni kwamba kuna uhusiano mkubwa baina ya lugha ya kufundishia na maarifa yanayokusudiwa kupatikana.
Ni muhimu kukumbuka kwamba lugha ya kufundishia inapaswa kuwa inayofahamika vyema na walimu na wanafunzi kwa jumla.
Kwa kujikita katika kauli hiyo, tunapata taswira inayosawiri hali ya elimu Tanzania.
Nchini humo, lugha ya Kiswahlili hutumiwa kuwafundishia wanafunzi katika shule za msingi ilhali lugha ya Kiingereza hutumiwa kuwafundishia wanafunzi katika shule za sekondari.
Bila shaka, hali hii humzuia mwanafunzi kuwa na mtiririko mwafaka wa maarifa aliyoyapata kutoka elimu ya msingi.
Pengo linalojitokeza kutokana na mkabala huu ni kwamba haufafanui ni kwa jinsi gani sehemu kubwa ya kazi zilizokwishafanywa zimejikita katika kutoa maelezo ya jumla kuhusu lugha ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia elimu kwa jumla.
Kama anavyosema Rubagumya (1990), Kiswahili kinapaswa kiutumike kufundishia elimu ya sekondari lakini kimezuiliwa na uhaba wa vitabu na uhaba wa walimu wa kukifundisha.
Inasikitisha kwamba hadi sasa, Kiswahili bado hakijapata dhima ya kuwa lugha ya kufundishia elimu ya sekondari.
Aidha, tafiti nyingi bado zinaonyesha udhaifu wa kutumia lugha za kigeni kufundishia elimu, na hivyo kupendekeza Kiswahili kitumiwe kama lugha ya kufundishia si kwa elimu ya sekondari tu, bali katika ngazi zote za elimu nchini Tanzania.
Athari
Kuna athari chungu nzima zinazotokana na hali ya kukosa kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia elimu katika shule za upili.
Athari hizi zinagusa walimu na wanafunzi wa shule za upili sio tu nchini Tanzania bali mataifa ya Afrika Mashariki kwa jumla.
Kwa upande wake Mammino (2000), ufundishaji wa elimu kwa kutumia lugha ya kigeni huathiri wepesi wa uwezo wa mwanafunzi kupata maarifa kwa upana na kwa kina.
Msanjila na wenzake (2011), wanadadavua kwamba, maarifa ni kitu kinachopanuka na kupata kina na upeo kwa njia ya matumizi ya lugha inayoeleka kwa walimu na wanafunzi.
Kwa mujibu wa maelezo ya wanaisimu hao, ni bayana kwamba wanafunzi wa sekondari nchini Tanzania huathirika kwa kukosa maarifa ya kiwango hicho kwa kuwa lugha inayotumika kuwafundishia ni ngeni kwao.
Baruapepe ya mwandishi: [email protected]
Marejeo
Bryman A. (2008). Social Research Methods. London: Oxford University Press.
Cummins, J. (2008). Teaching for transfer. Challenging the two-solitudes assumption in Bilingual education. In J. Cummins & N.H Homberger (Eds),Encyclopedia of Language and Education,2nd Edition,Volume 5.New York:Supringer Science + Business Media LLC.
Enon C.J. (1995). Educational Research, Statistics and Measurement. Kampala: Makerere University.