UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Changamoto zinazokabili Fasihi ya Watoto nchini
Na CHRIS ADUNGO
FASIHI ya watoto inapaswa kuangaliwa upya na kwa makini.
Fasihi ya watoto imepiga hatua kiasi fulani japo katika maeneo mengi bado ni changa mno. Fasihi ya watoto inayofahamika katika jamii nyingi za Afrika ya Mashariki, kwa kiasi kikubwa ni ile iliyo katika baadhi ya vitabu vya hadithi (ngano) na nyimbo za kitoto za makabila mbalimbali.
Katika maeneo mengi, kazi za watoto kama ushairi, riwaya fupi, tamthilia, na kadhalika bado hazijafahamika vyema. Juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanyika katika kuhakikisha kuwa fasihi ya watoto katika kumbo mbalimbali inakua na kushika mizizi.
Ingawa hivyo, inahitaji kukuzwa kiuandishi na kiuchambuzi. Changamoto tulizozifafanua katika makala ya awali zinabainisha uhitaji wa serikali, mashirika, wahisani na wadau wote wa elimu kupitia uandishi na usomaji wa fasihi ya watoto kuchukua hatua na juhudi za dhati ili kukuza na kuendeleza maarifa ya kundi hili muhimu kwa jamii.
Bila kufanya hivyo, fasihi hii itabaki kuwa changa na kuonekana kukosa umuhimu. Wa- toto wanapaswa kulelewa na kupewa vionjo mbalimbali vya malezi na elimu kupitia fasihi yao.
Katika makala haya, tutazidi kuelezea changamoto zinazoikabili fasihi ya watoto inayostahili kuendelezwa hata zaidi.
(a) Kuwapo kwa pengo katika ufundishaji wa Fasihi ya Watoto katika taasisi za elimu
Ufundishaji wa fasihi ya watoto unaonekana kuwa nyuma. Ili kazi za watoto ziwe nyingi, mitalaa inapaswa kuijali fasihi hii ya kundi maalumu kwa sababu inaonekana wazi kuwa kundi hili la wanajamii bado halijapewa kipaumbele.
Wamitila anasema: “Pamekuwako na pengo kubwa katika ufundishaji wa fasihi ya vijana katika taasisi zetu za kielimu kuanzia shule za sekondari hadi vyuo vikuu. Mitaala mingi inaelekea kutilia mkazo fasihi ya watu wazima.” Ukilinganisha fasihi ya watoto na fasihi ya watu wazima, utagundua kuwa ile ya watu wazima imekomaa zaidi, na hivyo kauli ya Wamitila inabaki kuwa ya kweli.
(b) Kuchelewa kutambuliwa kwa kundi la watoto kifasihi
Katika jamii nyingi, kundi la watu linalotambulika kwa kiasi kikubwa ni lile la watu wazima. Labda, kutambuliwa huko kunatokana na kulihusisha kundi hilo na shughuli za uzalishaji mali katika jamii.
Kutambuliwa kwa kundi hili la watu wazima kunaifanya hata fasihi inayolilenga kuwa maarufu zaidi kuliko makundi mengine.
Kwa maelezo hayo, fasihi ya watoto haina umri mkubwa kwa maana kuwa kundi la watoto limetambuliwa kimataifa hivi karibuni katika Karne ya 18 na 19. Kuchelewa kutambuliwa kwa kundi la watoto kama kundi muhimu katika jamii kunaifanya hata fasihi inayolihusu kundi hili kuwa changa. Changamoto hii inafanya fasihi ya watoto kudai juhudi zaidi kutoka kwa waandishi na wadau wa fasihi kwa sababu kazi zake bado ni chache sana.
Hapo awali, watoto hawakuwa na fasihi yao mahususi. Mambo mengi yaliyokuwa yanawahusu yalikuwa yanapatikana katika kazi za fasihi ya watu wazima.
(c) Msukumo mdogo wa serikali katika kufadhili uandishi na usambazaji wa vitabu
Serikali kwa kiasi kikubwa inaonekana kutotilia maanani ufadhili wa waandishi wa fasihi ya watoto.
Watu hupenda kusema kuwa ‘watoto ni taifa la kesho.’ Mtoto ni mtu mzima wa kesho. Maana yake ni kwamba watoto wanapaswa kuandaliwa leo ili kesho waweze kuendeleza taifa. Hata hivyo, kwa kiasi fulani serikali inalitambua hilo kwa sababu kuna miradi kadhaa inayowalinda watoto mfano, kampeni ya kukomesha vifo vya mama na mtoto, kampeni ya kukomesha ugonjwa wa Malaria unaowashambulia sana watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, kampeni ya kutokomeza ugonjwa wa surua, na kadhalika. Juhudi hizo za serikali zinatakiwa kuhamia pia katika uandishi wa kazi mbalimbali za kifasihi zinazowahusu watoto ili kuwaandaa kifasihi.
Njia mojawapo ni kuwezesha ufadhili wa uandishi na kuandaa makongamano na warsha mbalimbali ili kuhamasisha jamii kuliangalia kundi hili kwa makini zaidi.
(d) Kazi za watoto kupata hadhira ndogo
Mwandishi wa kazi za fasihi yoyote daima anaiandaa kazi yake huku akimfikiria msomaji wa kazi hiyo. Msomaji wa kazi ya fasihi ni kama mlaji wa chakula ambacho kimeandaliwa na mpishi (mwandishi).
Kama mpishi atapika halafu chakula chake kisipate walaji, upishi huo unakuwa hauna maana. Fasihi ya watoto, kwa kiasi kikubwa haijapata walaji wengi (wasomaji wa kutosha). Hii ni changamoto kwa serikali kama ilivyobainishwa hapo awali. Sababu nyingine ya kukosekana kwa wasomaji wa fasihi ya watoto, ni watoto kupenda kuangalia runinga na sinema kuliko kusoma
vitabu.
Kama mtoto au kijana hayuko chini ya usimamizi wa mzazi au mwalimu, mara nyingi hupendelea zaidi kuangalia runinga. Jamii kwa ujumla inapaswa kuwahamasisha watoto kusoma vitabu zaidi kuliko kutazama runinga. Ili watoto waweze kusoma zaidi vitabu, ni lazima tuhakikishe kwanza kuwa vitabu hivyo vinapatikana ili waweze kutumia muda wao mwingi kuvisoma.
(e) Ukosefu wa maktaba maalumu za vitabu vya watoto
Maktaba nyingi zina vitabu vya watu wazima (au mara nyingine mchanganyiko na vile vya watoto hasa vitabu vya hadithi). Hakuna maktaba maalumu ambayo ina vitabu vya watoto peke yake. Bado ukienda kwenye maktaba zote nchini, utakuta mchanganyiko wa vitabu vya watu wazima na vitabu vichache hasa vya hadithi kwa ajili ya watoto vikiwa pamoja.
Kama kundi hili la watoto lingekuwa limetambuliwa na serikali vya kutosha, tungetegemea kuwapo kwa maktaba zinazotoa huduma ya usomaji wa vitabu hivi. Kukosekana kwa maktaba kunazidi kudidimiza juhudi za kuendeleza uandishi na usomaji wa vitabu hivi vya watoto kwa sababu upatikanaji wake unakuwa ni tatizo.
(f) Changamoto za tasnia ya uandishi kwa ujumla
Kuna changamoto nyingi sana zinazowakumba waandishi wa kazi mbalimbali za fasihi na zisizo za fasihi.
Waandishi hasa wale chipukizi hukumbana na changamoto nyingi sana. Changamoto hizi huwakatisha tamaa na wakati mwingine huacha kuendelea kujaribu ili waweze kuchomoza kiuandishi.
Changamoto nyinginezo ni kazi nyingi kuandikwa na watu wazima, kuegemeza uandishi katika aina moja ya kazi za fasihi na kutofanyika kwa uchambuzi na uhakiki wa kutosha wa kazi za watoto. Tutazijadili nyingi za changamoto hizi za kimajumui katika makala yajayo.