UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Dhana na dhima ya vivumishi katika Kiswahili
Na MARY WANGARI
JINSI tulivyofafanua vielezi vya namna huelezea jinsi au namna kitendo kilivyofanyika.
Hata hivyo, baadhi ya wataalam wanahoji kuwa vielezi vya namna halisi ni maneno ambayo kihalisia huwa vielezi na hayawezi kubadilishwa mathalan kabisa, sana, mno na kadhalika.
Dhana na dhima ya vivumishi katika Kiswahili
Kivumishi ni neno au maneno yanayotoa taarifa zaidi kuhusu nomino na kwa kawaida hutangulia na nomino.
Vivumishi huelezea au kufafanua zaidi kuhusu nomino kwa madhumuni ya kupambanua, kutofautisha, kuelezea au kufafanua nomino husika miongoni mwa nomino nyinginezo.
Vivumishi vya sifa – Hivi hutumika kutoa sifa nomino mathalan mtu, kitu, mahali na kadhalika. Kwa mfano.
Mama amepika chakula kitamu.
Alison ni msichana mrembo.
Mti mrefu ulianguka.
Alivalia rinda jeusi katika sherehe.
Aliimba kwa sauti nzuri.
Mvulana hodari alituzwa.
Vivumishi vya sifa vimeainishwa katika vitengo viwili jinsi ifuatavyo:
Vivimishi vya sifa ambishi – Aina hii hujitokeza ambapo viambishi huchukua ngeli kulingana na nomino husika. Kwa mfano:
Mkeka mkuukuu.
Kikapu kizito.
Vivumishi vya sifa kapa, aushi au tasa – Hivi husalia vivyo hivyo pasipo kuathirika na minyambuliko ya ngeli.
Vivumishi vya idadi – Hivi hutupa maelezo zaidi kuhusu idadi, kiwango au kiasi cha nomino.
Kuna aina mbili ya vivumishi vya idadi jinsi vilivyoainishwa ifuatavyo:
Idadi kamili – Vivumishi vya idadi kamili ni vile vinavyotumia nambari kuelezea nomino. Kwa mfano:
Nilinunua machungwa kumi.
Mwindaji aliwanasa swara wawili.
Mwalimu aliwatuza wanafunzi watano.
Daktari alimwambia arejee baada ya siku saba.
Idadi isiyo dhahiri – Vivumishi vya idadi isiyodhahiri ni vile vinavyoelezea kuhusu nomino kwa jumla bila kutaja idadi kamili kwa mfano:
Alimpigia simu mara kadhaa.
Wageni walipikiwa chakula kingi.
Dereva alishikwa mateka siku chache kabla ya kuachiliwa.
Vivumishi vya kumiliki – Hivi ni vivumishi vinavyotumika kuashiria kuwa nomino inamiliki nomino nyingine.
Shina la vivumishi hivyo aghalabu huundwa kulingana na nafsi mbalimbali mathalan: -angu, -etu, -ako, -enu na kuwa changu, chetu, chako, chetu na kadhalika.
Ukitumia talanta yako vyema unaweza kwenda mbali.
Mwalimu aliwaambia wanafunzi wafunike vitabu vyao.
Taifa ketu lina utajiri mwingi wa kiasilia.
Baruapepe: [email protected]
Marejeo:
Kihore, Y.M., Massamba, D.P.B. na Msanjira, Y.P. (2003). Sarufi Maumbo ya Kiswahili. Dar es Salaam: TUKI.
Lukusa, S. (2005). The Logic of Bantu Numeral Terms. Mauritius: LASU.
Massamba, David P.B. (2004). Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Dar es salaam: TUKI