UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Dhana na dhima ya wahusika katika kazi za fasihi
Na MARY WANGARI
KATIKA makala ya leo, tutajadili kuhusu mbinu ya wahusika katika usanifu wa kazi za fasihi kwa kuchambua fasili anuwai za wataalam kuhusu dhana ya wahusika.
Jinsi tunavyofahamu, wahusika katika kazi za fasihi ni viumbe wanaopatikana katika hadithi yoyote ile na huwa sehemu ya kazi nzima iwe riwaya, tamthilia au hadithi fupi.
Aidha, wahusika wanaweza kufafanuliwa kama binadamu wanaopatikana katika kazi ya kifasihi na ambao wana sifa za kitabia, kimaadili, kifalsafa na kiitikadi, ambazo hutambulishwa na maneno au matendo yao.
Wahusika vilevile wanaweza kutambulishwa kupitia maelezo ya mhusika au msimulizi, msingi wa hisia, hali ya kimaadili, mazungumzo na matendo ya wahusika, ambayo ndiyo kiini cha motisha au uhamasishaji wa wahusika.
Kulingana na (Wamitila, 2002) TUKI (1998:169), wahusika wanafasiliwa kama miti au viumbe vinavyowakilisha watu katika kazi za fasihi.
Umuhimu wa wahusika katika kazi za fasihi
Wahusika hutumiwa kuwakilisha hali halisi ya maisha ya watu katika jamii inayohusika.
Wahusika hutumiwa kuwakilisha mawazo mbalimbali ya pande mbili au zaidi za mgogoro katika kazi za fasihi.
Wahusika husawiriwa kisanaa na mwandishi ili waweze kuwakilisha dhana mbalimbali za maisha katika jamii kama anavyofafanua Rono (2013) akimnukuu Msokile (1992:42-43).
Kwa kawaida, mwandishi au ukipenda fanani husawiri wahusika kwa wasomaji wake kwa kutumia sifa pambanuzi walizonazo, jinsi walivyo, mambo wanayopenda na yale wasiyopenda katika maisha yao na mengineyo.
Isitoshe, wahusika hutumia tamathali za usemi, methali, misemo, na nahau katika mazungumzo yao ili kujenga tabia na hali ya kisanaa.
Sababu za wahusika kutofautiana katika kazi za fasihi
Kulingana na mtaalam wa fasihi, Rono (2013) wahusika wa kazi za sanaa huwa na tabia zinazotofautiana kati yao kwa sababu mbalimbali kama zifuatazo:
Dhamira ya mwandishi – Hii inahusu lengo la mwandishi. Ni maudhui yapi anayokusudia kuonyesha kupitia kazi yake ya fasihi?
Utanzu husika wa kazi ya fasihi – Jinsi tunavyofahamu, vipera vya fasihi vinajumuisha tanzu mbalimbali zinazotofautiana.
Kwa mintarafu hii, ni vyema kufahamu kwamba aina ya utanzu husika inaweza kuathiri aina ya wahusika, jinsi wanavyosawiriwa na mwandishi, kuaminika kwao, mahusiano baina yao, uwakilishi wao na majina yao.
Wasiliana na mwandishi kupitia baruapepe: [email protected]
Marejeo
Njogu, K. na Chimerra, R. (1999). Ufundishaji wa Fasishi: Nadharia na mbinu. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
Syambo, K. Mazrui (1992). Uchambuzi wa Fasihi. Nairobi: East Africa Education Publishers.