UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Dhima na aina ya vielezi katika Kiswahili
Na MARY WANGARI
VIELEZI vya namna hufafanua jinsi au namna kitendo kinavyofanyika.
Kitendo kinaweza kufanyika kwa namna mbalimbali kwa mfano: polepole, kijeshi, kikatili, vibaya, vizuri na kadhalika.
Vielezi vya namna vinaweza vikaainishwa katika vitengo vitatu jinsi ifuatavyo:
Vielezi vya namna halisi – Hivi hutueleza jinsi kitendo fulani kinavyofanyika kwa kutumia maneno halisi pasipo kuyaambatisha na maneno mengine au vivumishi vingine. Kwa mfano:
Mwanasiasa huyo aliuawa kikatili.
Mtoto wangu amelelewa vizuri.
Askari walifika haraka.
Vielezi vya namna hali – Vielezi hivi hutueleza jinsi kitendo fulani kilivyofanyika na hujihusisha na tabia ya kitu, mtendaji au kitendo husika. Kwa mfano:
Rais aliingia jukwaani kwa kishindo.
Maharusi walikumbatiana kwa furaha.
Kijakazi alilima kwa bidii.
Vielezi vya namna kitumizi au ala – Hivi ni vielezi vinavyotoa habari kuhusu kitu, kifaa, mbinu au ala iliyotumiwa kufanya kitendo fulani. Kwa mfano:
Mfungwa alicharazwa kwa mijeledi.
Shangazi alikata tikiti maji kwa kisu.
Seremala alikata mbao kwa msumeno.
Mzegazega alibeba mitungi kwa rukwama.
Vielezi vikariri – Ni aina ya vielezi vinavyosisitiza jinsi kitendo kinavyofanyika kwa kutaja kielezi kinachorejelewa mara mbili mfululizo. Kwa mfano.
Alianua nguo upesiupesi
Usioshe vyombo ovyoovyo
KItwana alilima kiholelaholela
Mwanafunzi aliandika insha harakaharaka.
Mgonjwa alitembea polepole.
Vielezi vya kimfanano – Hivi ni vielezi vinavyotumika kuelezea jinsi kitendo kinavyofanyika kwa kulinganisha. Kwa mfano.
Mwanajeshi alipigana kishujaa.
Baba yake huzungumza kiungwana.
Mhudumu alimjibu kiheshima.
Vielezi viigizi – Hivi ni vielezi vinavyoigiza mlio au sauti ya kitendo kilichofanyika kwa kutumia tanakali za sauti.
Mwalimu alimzaba mwanafunzi mkorofi kofi pa!
Sarafu ilianguka majini chubwi.
Omar alianguka changaraweni tifu.
Samaki aliyeoza alinuka fe.
Vielezi vya vielezi – Hivi ni vielezi vinavyotumika kuelezea kielezi kingine na kwa kawaida hutanguliwa na kielezi badala ya kitendo. Kwa mfano:
Familia ilipomwona jamaa aliyetekwa nyara ilifurahi sana.
Sebule ilipambwa na kuvutia mno.
Mwimbaji aliimba vizuri kabisa.
Vielezi vya vivumishi – Hivi ni aina ya vielezi vinavyotoa habari zaidi kuhusu kivumishi. Kwa mfano:
Kassim ni mrefu sana.
Mtoto wake ana nidhamu mno.
Vielezi vya vivumishi au vielezi vinaweza pia kufafanuliwa kama vielezi vya kiwango kitenzi, kielezi kingine au kivumishi. Kwa mfano.
Mtoto alilia kwa uchungu sana.
Bikizee alitembea polepole sana.
Bi harusi alionekana wa kuvutia mno.
Baruapepe: [email protected]
Marejeo
Richards, J., Platt, J. na Weiber, H. (1985). Longman Dictionary of Language and Teaching Applied Linguistics. Edinburgh Gate: Pearson Education Ltd.
Lugemalira, J.M. (2005). A Grammar of Runyambo. Dar es Salaam: University of Dar es salaam.
Wesana-Chomi, E. (2003). Kozi Tangulizi Katika Sarifi Miundo ya Kiswahili. Sebha: Chuo Kikuu cha Sebha