UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Kiini cha makosa katika lugha
NA MARY WANGARI
BAADHI ya visababishi vya makosa katika lugha ni jinsi ifuatavyo:
Maumbo
Baadhi ya watu katika jamii hupuuza mofu za Kiswahili na kuongea zile zinazopatikana katika lugha mama.
Kwa mfano:
Aliendaga badala ya alienda.
Nipeko badala ya nipe.
Anasomanga badala ya husoma.
Wakati mwingine watu huongeza mofu kwenye neno. Kwa mfano:
nipee badala ya nipe
nielekezee badala ya nielekeze
Tatizo lingine na linalotokea sana ni pale ambapo watu huonyesha ukubwa na udogo wa majina ya Kiswahili usio wa kawaida.
Mifano:
Katoto badala ya kitoto
Lisaa badala ya saa
Kimtu badala ya jitu
Khatungi badala ya mtungi
Kwa sababu ya kuzoea mfumo wa ngeli katika lugha mama, watu wengi hushindwa kuzingatia ngeli za Kiswahili na hivyo kuvuruga upatanisho wa kisarufi. Tazama mifano ifuatayo:
ng’ombe hizi badala ya ng’ombe hawa
mtu mgani badala ya mtu gani
lijitu linene badala ya jitu nene
Miundo ya Sentensi
Matatizo katika kiwango cha sentensi aghalabu yanahusu kutozingatiwa kwa uwiano wa kisarufi. Asili ya mwingiliano huu ni lugha mama zisizozingatia mfumo wa ngeli. Mifano:
Makosa Sahihi
Nyumbani kumekujwa wageni. Nyumbani kumekuja wageni.
Mavitu zangu zimeibiwa. Vitu vyangu vimeibwa.
Mimi naenda kwa hapo. Mimi naenda hapo.
Tumemalizana? Tumemaliziana?
Maana ya Semantiki
Tatizo hili linatokana na hali ya kukosa ufahamu wa kanuni za kisarufi. Vilevile, tatizo hili linahusu kutotambua kati ya viunganishi na vihusishi.
Mifano:
Alienda na miguu badala ya Alikwenda kwa miguu
Nilipewa ni baba badala ya Nilipewa na baba
Tatizo la Kutafsiri Moja kwa Moja
Mifano:
Anakunywa sigara badala ya Anavuta sigara
Alirudisha ahsante badala ya Alishukuru
kuingiza bao badala ya kufunga bao
Nitaandikwa kazi badala ya Nitaajiriwa kazi.
Marejeo
Massamba, D.P.B. (2002). Historia ya Kiswahili 50 BK. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
Ipara, I. O. & Waititu, F.G. (2006). Ijaribu na Uikarabati. Nairobi: Oxford University Press.
Habwe, J. (2006). Darubini ya Kiswahili. Nairobi, Phoenix Publishers.
Maddo, U. & Thiong’o, D. (2006). Mazoezi na Udurusu: Kiswahili 102/2. Nairobi: Global Publishers.