UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Kiswahili kama fumbato la desturi na itikadi za jamii
Na CHRIS ADUNGO
LUGHA hubadilika kadri jamii inavyobadilika.
Kama sehemu ya utamaduni, lugha ni amali ya jamii inayoizungumza na ina alama ya umoja wa kitaifa kwa sababu kama kitendo, ni zao la amana ya jamii.
Lugha ni utambulisho wa jamii na kupitia kwayo, watu hupashana habari, hujenga uhusiano, huelimishana na kupatana au hata kufarakana.
Kiini kikuu cha lugha ni kudumisha mawasiliano miongoni mwa binadamu.
Kwa njia ya lugha, maisha ya jamii yanaakisiwa na kuifanya kuwa kioo cha jamii. Bila ya lugha ingekuwa vigumu kuurithisha utamaduni kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Akijadili nafasi ya lugha katika utamaduni, Mbeo (2006), anasema kuwa Kiswahili ni njia kuu ya mawasiliano ya wanajamii.
“Ilitumika kuanzia enzi za utawala wa kikoloni hadi leo. Imekuwa ni njia muhimu ya mawasiliano baina ya watawala na watawaliwa ili kuharakisha maendeleo ya taifa. Kiswahili ni lugha ambayo ni kielelezo cha ndani ya jamii za Waafrika. Imekuwa ikitumika kuelezea mila, itikadi na desturi ambazo ni nguzo muhimu za utamaduni wetu”.
Kwa mujibu wa Mazrui na Mazrui (1995), Kiswahili ni lugha iliyo na asili yake Pwani ya Afrika Mashariki na pia ni lugha ya Kibantu ambayo kwa karne nyingi imekuwa na mwingiliano mkubwa na lugha nyingi za kigeni. Kutokana na hali hiyo, nguvu za kuenea kwake zimetokana hasa na mambo makuu matatu ambayo ni biashara, utawala na dini.
Akichambua kuhusu utamaduni, Mbeo anasema kuwa utamaduni ni hali ya ustaarabu iliyofikia jamii ya watu kutokana na mafunzo au uzoefu wa kutenda kazi. Ni hali inayojumuisha imani, mila, mafunzo na desturi za jamii ambazo hutumika kama kitambulisho cha jamii husika zikilinganishwa au kutofautishwa na za jamii nyingine.
Utamaduni ni kielelezo cha uhai na utashi wa taifa na ni mzazi wa sekta nyinginezo za jamii kama vile teknolojia, siasa na uchumi.
Kwa hiyo utamaduni ni jumla ya mambo yote yaliyobuniwa na jamii ili kukidhi utashi na maendeleo yake. Sera ya Utamaduni (1997), inaelezea dhima ya utamaduni kuwa ni utambulisho wa taifa na watu wake.
Lugha ni nyenzo muhimu sana katika kuuelezea utamaduni wa taifa lolote liwalo kwani haiwezi kuwa utambulisho wa taifa bila kuelezea utamaduni wake.
Kiswahili ni kielelezo cha utamaduni wetu kwa sababu huhifadhi taarifa zake kwa njia mbalimbali kama maandishi, kanda zilizorekodiwa, katika mitandao ya kitovuti ambazo hurejelewa na wanajamii au vyombo vingine vya elektroniki.
Matumizi ya Kiswahili katika shughuli za utamaduni yamechochea maendeleo ya jamii kwa namna nyingi. Kiswahili hutumiwa na vikundi vya sanaa au vyama mbalimbali vya utamaduni kuwasilisha ujumbe uliokusudiwa.
Mathalani maarifa, itikadi, maadili na ufundi anuwai umekuwa ukiwasilishwa kwa kutumia Kiswahili. Aidha, sanaa za kuchonga vinyago au kutengeneza barakoa pamoja na kwamba zinahitaji kujieleza kwa kuzitazama tu, pale yanapohitajika maelezo, Kiswahili hutumika kutolea ufafanuzi wa fikra fiche katika sanaa hizo.
Matumizi ya Kiswahili hudhihirika katika nyimbo ambazo huwa na mafunzo ya maadili kwa mfano, kuwaelimisha wanajamii kuhusu madhara ya kuavya mimba, madhara ya zinaa na jinsi ya kujilinda na kuzuia maambukizi ya magonjwa hayo hatari.
Umahiri wa wasanii wa muziki katika kutumia Kiswahili unajidhirisha katika muziki wa kizazi kipya hasa wa kufokafoka.
Ijapokuwa baadhi ya watu wanaukashifu kuwa unaiga utamaduni wa kigeni, unawasilishwa kwa Kiswahili na unaelezea matukio yaliyomo kwenye mandhari yaliyojengeka kwenye misingi ya jamii za Kiafrika.
Katika magazeti na vyombo vingine vya habari, Kiswahili ni mojawapo ya lugha zinazotumika kufahamisha, kuburudisha na kuelimisha wanajamii kuhusu mambo kadha wa kadha yakiwemo ya utamaduni. Michoro ya katuni huambatana na maelezo yaliyoandikwa kwa Kiswahili ili kutoa mafunzo mbalimbali kwa hadhira lengwa. Kiswahili hutumika katika sala na hata kuendesha taratibu za kuabudu.
Viongozi wa dini hutumia Kiswahili katika kutunga sheria na kanuni pamoja na kuandika vitabu vya kuziadilisha jamii. Pia hutumika katika sherehe za jadi kwa mfano, katika jando na unyago, wakati wa harusi au kukabidhiwa madaraka na majukumu mapya.
Kwa kutumia Kiswahili, wazee huwaingiza wahusika katika hali mpya ya maisha. Huwafunza namna ya kuishi na kutenda mambo kulingana na majukumu yao. Huwaarifu na kuwaombea vijana kwa Mungu ili awaongoze, awalinde na kuwafanikisha maishani. Kiswahili hutumika katika kusimulia hadithi ambapo lugha ya nathari hutumika kutoa mafunzo mbalimbali. Mtambaji ana uwezo wa kutumbukiza hapa na pale semi zenye maana maalum ambazo zina mafunzo kwa wanajamii.
Kwa upande wa changamoto iliyopo kwa lugha hii ili iwe kielelezo cha utamaduni wa Mwafrika, ni kwamba baadhi ya watumiaji wa lugha hii hususan vijana, wanaidhalilisha kwa kuzungumza lugha isiyo ya heshima au staha huko mitaani, katika vyombo vya kusafiria au mazingira mengine anuwai.
Ieleweke kuwa maendeleo ya sekta zote, yawe ya kiuchumi, kisiasa, kiteknolojia, kijamii na kitamaduni, yanahusisha lugha katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku. Ni muhimu kufahamu utamaduni ni sekta mtambuko ambayo inahusiana na kuingiliana na maeneo mengine.
Hivyo sekta zote zinapaswa kuhimiza matumizi ya Kiswahili, iwe ni kwa mazungumzo au maandishi.
Vyombo vya habari ni sekta muhimu ya utamaduni wa jamii na vyenye nguvu kubwa katika kuutangaza, kuutetea na kuueneza utamaduni, kwa makusudi au bila kujua vinatumika kuudhoofisha utamaduni wa jamii, kuibua mitafaruku ya kiutamaduni au kueneza utamaduni wa kigeni usioifaa jamii yetu.
Ukiukaji wa maadili katika matumzi ya lugha, picha na michoro ni hali ambayo inalalamikiwa kila siku hasa katika runinga na magazeti.
Hivyo, zifanyike jitihada za kujenga uwezo wa wanahabari, wasanii na wanalugha kwa ujumla kwa kuwapatia mafunzo kuhusu utamaduni kwa kupitia semina, warsha, makongamano na matamasha mbalimbali ili hatimaye watumie Kiswahili kwa lengo la kukikuza badala ya kuitumia kibiashara tu kama ilivyo sasa. Pia vyombo vya habari vishiriki kikamilifu katika kuelimisha umma kuhusu matumizi fasaha ya Kiswahili.