Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Mazungumzo hujitokeza kama mtagusano wa kimaneno

March 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na CHRIS ADUNGO

ISTILAHI ‘mazungumzo’ inatumiwa sana katika miktadha isiyo ya kitaaluma kwa kuwa ni mawasiliano semwa yasiyo rasmi.

Mazungumzo ni mabadilishano ya hisia za moyoni, maoni au dhana. Ingawa hivyo, wachanganuzi-usemi hawako wazi na kile kinachomaanishwa na dhana ya ‘mazungumzo’.

Baadhi yao hutumia istilahi hii kufafanua aina yoyote ya utagusano-simulizi.

Cook Guy, katika kitabu chake ‘Critical Discourse Analysis’ (1989:59), anafafanua kuwa usemi wowote simulizi unaweza kuainishwa kuwa mazungumzo iwapo:-

(i) Hausababishwi kimsingi na kazi za kiutendaji.

(ii) Nguvu zozote za washiriki zisizo sawa zinazuiliwa kwa muda.

(iii) Idadi ya washiriki ni ndogo.

(iv) Zamu ni fupi sana.

(v) Usemi kimsingi ni kwa washirika na si kwa hadhira ya nje.

Mazungumzo hujitokeza kama mtagusano wa kimaneno wa mara kwa mara zaidi.

Mtu anaweza kuishi tangu utotoni mwake hadi uzeeni bila kuandika barua, kutunga shairi wala kujadili sera ya umma lakini ni nadra sana kuwepo kwa hali ambapo atakosa kabisa fursa ya kuzungumza na marafiki wenzake.

Katika hali hii, mazungumzo basi ni tukio-usemi (speech event) la kila siku.

Tunashiriki katika mazungumzo kwa ajili ya takrima, burudani, kupiga umbea na kuthibitisha kuungana kwetu kirafiki au kufanikisha kazi fulani kama vile kupata usaidizi na mwongozo masomoni, kuagiza chakula hotelini, kupangisha chumba, kujieleza katika mahojiano ya kutafuta kazi, nk.

Zamu

Njia mojawapo ya kufanikisha mazungumzo ni ushikaji zamu. Ushikaji zamu ni mbinu wanaoitumia wazungumzaji kupokezana na kuendeleza mazungumzo yao. Ni kubadilishana majukumu ya uzungumzaji kati ya msemaji na msemezwa.

Dhana hii hutokea bila ya kuangaliana kiusemi na aghalabu hushirikisha mipumuo (pauses) michache. Huongozwa na kanuni za jumuiya-lugha inayohusika. Taratibu za zamu hubadilika sio tu baina ya tamaduni ila pia baina ya lugha mbalimbali. Mpishano katika hali fulani husika utaruhusiwa katika baadhi ya jamii zaidi kuliko nyingine.

Ushikaji zamu huongozwa na viashiria mbalimbali ambavyo huwawezesha wazungumzaji kuingia na kutoka katika mazungumzo. Kunyamaa kwa mzungumzaji mmoja ni ishara ya kumpokeza mwenzake zamu katika mazungumzo.

Zamu hubadilika kulingana na mtu anayeshiriki mazungumzo na hali ya mazungumzo husika.

Tafiti kuhusu jamii za Kimagharibi zinaonyesha kuwa mwisho wa zamu ya mzungumzaji mmoja na mwanzo wa zamu ya afuataye aghalabu hupishana takriban kwa usahihi na punde kamili.

Mpishano wa zamu hutukia tu katika takriban asilimia tano au ndogo zaidi ya mazungumzo, hali inayoeleza kwa namna moja au nyingine kimsisitizo kuwa wazungumzaji wanajua wakati na mahali hasa pa kuingilia katika kushiriki kwao mazungumzo.

Wao wenyewe kwa wenyewe huashiriana kuwa zamu moja imekamilika na nyingine inafaa ianze.

Wasemaji huashiria kuwa zamu yao iko karibu kuisha kwa kutumia au kuzingatia viashiria vya kimaneno au vya kiziada-lugha.

Kwa vile zamu huishia katika sentensi kamili, ukamilifu wa sentensi huenda ukaashiria mwisho wa zamu.

Matumizi ya sentensi zinazoishia kwa maswali (question tags) ni moja ya mbinu dhahiri katika kuonyesha au kumkaribisha mwenzi au mshirika wa mazungumzo aanze kuzungumza.

Kwa mfano:

X: Leo kuna upepo mkali sana, sivyo?

Y: Bila shaka.

Mwisho wa zamu vilevile unaweza kuashiriwa kwa kuongeza au kupunguza sana kiimbo cha sauti. Hali hiyo inaweza kudumishwa zaidi katika mazungumzo yasiyo rasmi kwa kuvuta silabi katika neno la mwisho.

Semi nyingine zinazoashiria kumalizika kwa zamu ni pamoja na matumizi ya maneno kama vile “ushafahamu?“, “ushaona?“, au viingizi “mmh“, “ahaa“, “enhe“, nk.

Viashiria vingine ni matumizi ya viziada-lugha kama vile mipumuo, ishara za mikono, miondoko ya mwili au hata hali ya msemaji na msemezwa kuangaliana.

Msemaji anaweza kuchagua ni nani atakayeshika zamu ya kuzungumza kwa kutaja jina lake au kumrejelea kwa maelezo machache.

Kwa mfano, Spika katika mazingira ya bungeni anaweza kusema: “Mheshimiwa Waziri wa Elimu…” kwa maana ya kuwa ni zamu ya waziri huyo pengine kujibu au kuuliza swali, kupinga hoja, kuchangia maoni au hata kuhutubia kikao husika cha bunge.

Ubadilishanaji wa zamu una umuhimu maalum katika mazungumzo kwa kuwa mpishano baina ya zamu huenda ukaashiria hasira, wasiwasi au haja ya kutaka kusahihisha kinachosemwa na mzungumzaji.

Vivyo hivyo, vituo baina ya zamu vilevile hubeba maana maalum. Msemaji anapofikia sentensi ya mwisho, mshika-zamu mwingine ataanza kuzungumza bila ya kuambiwa.

Hii ni kwa sababu washiriki hutambua kukamilika kwa sentensi au usemi. Ushikaji zamu pia hutokea pale ambapo wazungumzaji wawili wanaacha kuzungumza kwa pamoja.

Kwa mfano:-

Farah: Asiyeshiriki mashindano hashindi lakini…

Rashid: Hushindwa!

Ikiwa Rashid alilenga kukamilisha usemi wa Farah, basi atakayeshika zamu ifuatayo katika kuendeleza mazungumzo ni Farah.

Mbali na ushikaji zamu baina ya wazungumzaji wawili, kuna ushikaji zamu unaodhihirika kwenye makundi ya wazungumzaji kama vile katika mijadala au tetezi za wahusika mbalimbali kortini.

Isitoshe, ushikaji zamu unaweza kuashiriwa ama kiisimu, kivitendo au kimiondoko miongoni mwa wahusika wanaoshiriki mazungumzo.