Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Mbali na lugha za mama, wasomi waandike pia kwa lugha asili

February 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na EVAN MWANGI

NAMUUNGA mkono kwa dhati mtaalam wa fasihi Ngugi wa Thiong’o katika harakati zake za kuhifadhi na kukuza lugha za Kiafrika.

Amezungumzia swala hili nyeti katika ufundishaji wa lugha na fasihi tangu miaka ya sabini, hata katika vijitabu vyake vya watoto kama vile Njamba Nene na Mbaathi i Mathagu (Shujaa Hodari na Basi Lenye Mabawa).

Hata hivyo, anajulikana sana duniani kutokana na yale ambayo ameyaandika katika kitabu chake mashuhuri ‘Decolonising the Mind’ (Kujikomboa Kiakili) alichochapisha mwaka 1986.

Katika kitabu hiki, Ngugi anaona Kiingereza kama “cultural bomb” (bomu la mfumo wa maisha) ambalo nia yake ni kudhoofisha jinsi Waafrika wanavyoishi na maendeleo yao kijamii, kiuchumi, kisiasa n.k. kwa kuzambaratisha “mother tongues” (lugha za mama).

Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya upili ya St Peters Mumias wafundishwa somo la Bayolojia na Mwalimu Martin Wanjala Januari 17, 2019. Picha / Isaac Wale

Hivi karibuni Ngugi amezindua kitabu kipya alichoandika kwa lugha yake ya mama, Kikuyu.

Kitabu hiki, ‘Kenda Muiyuru’ (Kenda Iliyojaa/Kumi) kinahadithia asili ya jamii ya Wakikuyu kutoka kwa familia za wasichana tisa wa Gikuyu na Mumbi, wanzilishi wa kabila hilo, mfano wa Adamu na Hawa katika maelezo yaliyo kwenye Kurani Tukufu na Biblia.

Hasa, wasichana hao wa Gikuyu na Mumbi walikuwa kumi, lakini Wakikuyu wakihesabu wanaita ‘kumi’ ‘kenda iliyojaa’ (tisa iliyokamilika) ndio waepushe vitu, wanyama, au binadamu wanaohesabu kutokana na mikosi.

Lugha zinazozungumzwa Kenya ni nyingi, zaidi ya arobaini. Lazima zote tuzihifadhi, juu hakuna lugha inaweza jiona kama ni bora kuliko nyingine. Tukilinganishwa na mataifa mengine ya Kiafrika, kama vile Ghana na Afrika ya Kusini, Kenya tuko nyuma katika kukuza lugha zetu juu tunasoma tu Kiswahili kama lugha ya taifa, Kiingereza kama lugha ya masomo na ofisi, na, kwa wale wako na bahati kusomea shule za mzingi vijijini, lugha zetu za mama (kama vile Dholuo, Kikuyu, au Ekegusii).

Ukitoka kabila hili, hujui lugha ya kabila lile. Si Wakikuyu wengi, mimi nikiwa mmoja wao, wanaoweza kuongea Kimaasai ama Kidholuo. Bali wananachi wa Ghana na Afrika ya Kusini wanaongea lugha tofauti za kiasili za nchi zao. Si ngumu kupata mtu kutoka Ghana akiongea zaidi ya lugha tano na lahaja tofauti tofauti za kitamaduni. Lakini ni Wakenya wangapi wanaweza kuongea zaidi ya lugha moja, tukiweka Kizungu na Kiswahili kando?

Wasomi kadhaa, kama vile Doris Sommer katika kitabu chake ‘Bilingual Aesthetics’ (Mitizamo Kisanaa kwa Lugha Zaidi ya Moja) wameonyesha manufaa tunayopata kutokana na kuweza kutumia lugha nyingi kwa wakati mmoja, hata kama tutafanya makosa tukiongea lugha zingine.

Lugha hizi hufanya tuwakubali watu ambao ni tofauti na sisi kiukoo, kitabaka, kidini na kimawazo. Kuongea lugha za kiasili za Kenya, bali na lugha zetu za mama, ni dawa tegemevu ya kukabiliana na janga la ukabila. Ndiposa kwa sasa najifundisha Ekegusii, Dholuo na Kikamba.

Lugha ni kama mimea kwa mkulima; lazima tuzitunze kwa makini.

Msomi wa lugha kutoka Afrika Kusini, Neville Edward Alexander (1936-2012), amesisitiza kwamba kuhifadhi lugha zetu ni jukumu kiwango moja na kuhifadhi mazingira yetu. Lugha zinaangamia, na tusipojihadhari tutapata zimezamia kwenye bahari ya lugha za kigeni.

Ngugi hutumia Kiingereza kupigia debe lugha za kitamaduni. Sasa tupige hatua nyingine na kutumia lugha hizo katika kusambaza falsafa zetu na matokeo ya utafiti katika vyuo vya juu kama vile wanavyofanya wasomi wa Tanzania, mfano Tadeo Andrew Satta katika kitabu chake Msingi wa Methodolojia ya Utafiti: Muhtasari wa Mwongozo kwa Ajili ya Wanafunzi wa Uzamili na Uzamivu katika Sayansi ya Uongozi. Sifikirii wasomi wa Kenya wanaguza hata magazeti ya lugha ya Kiswahili. Kwao Kimombo tosha!

Mimi sitaandika kwa Kikuyu, lugha yangu ya mama, kama Prof. Ngugi wa Thiong’o. Hili ni chaguo la kibinafsi, sababu moja ikiwa nimejimudu kwa Kikuyu kufikia kiwango cha kuwa sina mengi mapya ya kuongezea kuijua hiyo lugha zaidi ya vile naijua sasa.

Lakini hata kama naweza kuandika na kuongea kwa Kiswahili, sijazatiti vilivyo kwa kutumia hii lugha. Hivyo nitakua nikijiimarisha kiusomi, kiakili, na kilugha kwa kutumia Kiswahili.

Kuna sababu kadhaa za Wakenya kama mimi kuogopa kutumia lugha zingine za kitamaduni bali na lugha ya mama. Moja yake ni “imposter syndrome” (hali ya kujisikia laghai). Yaani unajiona kama barakala, kujifanya unatumia lugha ambayo huijui kamili. Unaonelea heri uiachie mabingwa wayo. Kama wanavyofafanua Joe Langford na Pauline Rose Clance, wasomi wa Georgia State University, Marekani, hili ni tatizo linalowakumba wasomi wengi. Wanachelewesha uandishi na utafiti mpaka ule wakati watafikia “perfection” (ukamilifu).

Lakini ni katika jitihada za kutafuta huu ukamilivu ambao tutajiimarisha katika uzamivu kilugha na kimawazo, sio kukaa kitako kungojea miujiza kutoka mbinguni ambayo itatufanya mabingwa wa lugha bila kujikwaa na kuanguka siku za mwanzo mwanzo.Linalonipa moyo ni kwamba hata mwandishi shupavu wa Kiswahili Shaaban bin Robert, ambaye amesifiwa kuwa “Shakespeare wa Swahili,” mwenyewe hakuwa Mswahili haswa kikabila. Wasomi wengi wa Kiswahili wenye asili ya Kiswahili kama vile Alamin Mazrui, Said Ahmed Mohamed, na Farouk Topan pia wamekataa sisitizo kuwa lazima waandishi wa Kiswahili wawe Waswahili.

Ndio hata kama sina umahiri mkubwa wa Kiswahili, na matumishi yangu pengine yako na dosari nyingi, na vilevile sijasoma hii lugha na fasihi yake kwa darasa lolote baada ya kumaliza shule ya sekondari, nitakuwa nikiandika makala kadhaa ya kitafiti kila mwaka kwa Kiswahili ili niielewe zaidi.

 

Prof. Mwangi hufundisha Kiingereza Northwestern University, Marekani. Ni Mshiriki wa Public Voices Fellowship, kupitia OpEd Project.

Baruapepe: [email protected]