Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Mchakato wa utafiti katika utamaduni wa Kiswahili

January 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WANGARI

ILI kufanikisha tafiti kuhusu utamaduni wa Kiswahili, kazi mbalimbali zimehusika ambazo ni pamoja na kitabu cha ‘Tungo Zetu’.

Hiki ni kitabu pekee ambacho hadi sasa kimezama kitaaluma kuhusu Msingi wa Mashairi na Tungo nyinginezo.

Kando na michakato binafsi ya uandishi kuhusu ugozi, kazi nyinginezo zinajumuisha Uswahili wa Waswahili pamoja na matukio ya Zanzibar ya 1964, ambapo mwanafasihi Ibrahim Noor Shariff amejikakamua kueleza mapisi ya Waswahili na mambo yao.

Isitoshe, pia ameweza kutufunza mengi kuhusu arudhi yaani mipango ya tungo na kumkosoa Sheikh Kaluta Amri Abeid katika kitabu chake cha Sheria za Kutunga Mashairi na Diwani ya Amri.

Kuna mawimbi ya mihemuko dhidi ya juhudi za mwandishi K.A. Abeid lakini inarekebika bahari ya fikira za mhakiki inapotulizana katika kurasa za mbele.

Kwa mfano, wasomaji wengi wanafahamu kuhusu tarehe ya urudhi, utendakazi wa tungo, upungufu katika maelezo ya tungo na mijadala mbalimbali kuhusu kipengele cha ushairi, fani ambayo ina mapisi marefu sana katika Utamaduni wa Kiswahili.

Kwa upande wake, Shariff anakiri kuwa, “Iwapo ni kweli kwamba bahari ya tungo za Kiswahili ni ya maji makuu, basi ni wazi kabisa kuwa yaliyozungumzwa humu ni maelezo ya kimuhtasari tu kuhusu fasihi hiyo.”

Shihabuddin Chiraghdin ni mtaalam mwingine ambaye hapaswi kusahaulika katika watenzi wa kazi bora za lugha ya Kiswahili na Utamaduni wake.

Makala yake “Kiswahili na Wenyewe” yangelingana naye kwa hija, haja na jiha, uzito wake ungekuwa mkubwa zaidi.

Hata hivyo, aliweza kujenga msingi madhubuti uliothibitisha kweli yakinifu kwamba Waswahili ni watu hai na hao ndio wenye lugha ya Kiswahili.

Sisi wengine sote ni watumiaji na hatuna budi kurejea kwao – ama wakiwa na “vibandiko” vyao au bila – kujifunza kutoka kwao na kujiimarisha katika utajiri wa Kiswahili asilia.

Uswahili hivi leo si kinyang’anyiro tena. Katika mlolongo mrefu wa waandishi wa kazi zetu, Maalim Haji Chum ni mtafiti msomi mwingine ambaye ameshughulikia sana tafiti za lugha ya Kikae au Kimakunduchi na Utamaduni wake.

Amebobea mno katika utafiti wa Taasisi ya Kiswahili na lugha za Kigeni, Zanzibar, kutokana na data zake binafsi ambazo amezikusanya binafsi na kuzitumia katika uandishi wake.

Aidha, Maalim Haji Chum amepambanua nyanya anuai ikiwemo mapisi ya Wilaya ya kusini, asili za majina ya miji na mitaa, uchumi na mila, lugha ya Kikale, fani mbalimbali, ngoma, jando, daku, shomoo, miongo na sherehe za kuaga mwaka.

Kazi hii ni ya msingi sana kwa mtafiti yeyote wa Kikae na Utamaduni wa watu wa mwambao wa kusini.

Umuhimu wa kazi hizi zilizotajwa na nyingine nyingi ambazo hazikutajwa (kama vile kazi za Mzee Hamisi Akida, Whiteley, Mnyampala na Shihabuddin, Mohamed Bakari, S.A. Muhammad, Mohamed Abdallah na kazi zote za fasihi) ni mkubwa sana.

Katika kizazi hiki, ni matumaini kuwa hivi karibuni tutapata kitabu au vitabu vitakavyojadili Historia ya Kiswahili kwa upana na undani wake, Utamaduni wa Kiswahili kwa kina cha haja na hivyo kuweza kukiegemeza Kiswahili Sanifu katika Kiswahili asilia ili kiwe na mashiko ya kudumu.

Kadiri ya mapanuzi na maendeleo yake, makuzi na matumizi yake, Kiswahili Sanifu, kama lugha nyingine zote, sharti kiwe na kwao, kiwe na wasemaji hai wa kwenda kuulizwa kweli ya usahihi wa mambo.

 

[email protected]