UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Mchango wa Mwanafalsafa Aristotle katika ukuzaji Fasihi
Na WANDERI KAMAU
ARISTOTLE alikuwa mwanafuzi wa Plato.
Alijiunga na chuo cha Plato katika mwaka wa 367KK.
Kitabu chake mashuhuri kuhusu fasihi kinaitwa ‘The Poetics’, hata ingawa ni kazi ambayo haikukamilika.
Ni vipande vipande vya fikra za Aristotle ambavyo vitaeleweka vizuri kwa kutilia maanani falsafa yake yote kuhusu ulimwengu uliomzunguka.
Tofauti kubwa kati ya Plato na Aristotle ni kwamba Plato alikuwa mwanafalsafa dhahania, naye Aristotle alikuwa mwanasayansi asilia. Ni kweli kwamba Aristotle aliendeleza mkakati wa kusemezana unaopatikana katikan kazi za Plato.
Hata hivyo, Aristotle anafasiri hali ya dhahania kupitia mazingira yakini na thabiti yaliyomzunguka binadamu.
Yaani vitu vilivyopo vyenyewe vinasheheni sifa zinavyovijumuisha katika mabadiliko yake.
Ingawa hakuna ushahidi kwamba Aristotle alinuia kumpinga au kumjibu Plato moja kwa moja, mawazo na mapendekezo yake yanadhihirisha kwamba alifahamikiwa na fikra za mwalimu wake.
Kwa upande wa fasihi, Aristotle anayarejelea masuala yayo hayo aliyoyazungumzia Plato.
Anakubaliana na Plato kwamba fasihi ni Sanaa inayosawiri mazingira yanayomzunguka mtu.
Huiga kibunifu
Hata hivyo, anadai kuwa hali hii ya kuiga ndiyo huifanya fasihi kutukuka. Aristotle anashikilia kwamba fasihi haiigi kikasuku; kinyume na haya, fasihi huiga kibunifu kwa kuzingatia mambo yanayoathiri maisha ya binadamu.
Maoni ya Aristotle kuhusu sanaa kwamba sanaa huiga hali asilia inayomzunguka mtu hayatokani na uchanganuzi wake wa fasihi; yanatokana na kitabu cha ‘Meteorology’ ambacho kinazungumza kuhusu utaalamu wa upishi.
Sanaa huiga mazingira kama ambavyo upishi unavyorahisisha tendo la kukimeng’enya chakula.
Sanaa huhamasisha hali asilia katika harakati ya hali hiyo kutimiza malengo yake. Mapengo ambayo mazingira hushindwa kujaliza hujalizwa na sanaa.
Kulingana na maoni ya Aritstotle, sanaa hufanya shughuli ile ile ambayo mazingira hufanya.
Tofauti ni kwamba sanaa hutumia mkakati wa kijabarati zaidi katika kulitimiza kusudi lake ikilinganishwa na mazingira.
Fasihi humtukuza mwanadamu, sifa zake za kuweza kuumba zikamleta karibu na Mwenyezi Mungu.
Ujuzi wa mwanasayansi
Aristotle alitumia ujuzi wa mwanasayansi asilia kufikia maamuzi yake.
Mwanasayansi asilia hutumia mishipa yake ya fahamu kufanya majaribio na kufikia uamuzi kuhusu kadhia mbalimbali anachozungumza.
Aristotle anaanza ziara yake kwa kutambua orodha ya tanzu za fasihi zinazopatikana katika ujirani wake.
Baadhi ya tanzu za fasihi anazotambua ni nyimbo ambazo hughaniwa pamoja na ala za muziki kama vile zeze au kinubi, futuhi na tanzia.
Tanzu za fasihi zinagawanywa katika makundi tofauti tofauti kulingana na:
(a) Usawiri wa wahusika: Wahusika wanaweza kuchorwa katika upotovu wao (futuhi) au katika utukufu wao (tanzia). Inawezekana kuwa na wahusika wanaochanganya upotovu na taadhima kama katika tamthilia inayochanganya futuhi na tanzia. Wahusika wanaweza kusawiriwa kiuyakinifu bila kupigiwa chuku au kudunishwa kupita kiasi.
(b) Kuchanganya masimulizi na maongezi: mtunzi anaweza kuchanganya masimulizi na maongezi kama anavyofanya Homer katika tenzi zake.
Kilele kuhusu tanzu mbalimbali za fasihi kinafika wakati ambapo Aristotle anazungumzia tanzia.
Katika kufanya hivi, Aristotle anazungumzia asili na dhima ya fasihi na wakati huo huo kuyajibu maswali yanayotokana na falsafa ya Plato.
Aristotle anaiona tanzia katika mkabala mmoja na somo elimu-uhai au bayolojia.
Tanzia
Anasisitiza kuwa baada ya tanzia kupitia katika hatua mbalimbali za mabadiliko ilifikia hali yake halisi na kikamilifu na kukoma.
Tanzia hii ni kama kiumbe kimoja kinachokua hadi kufikia ukamilifu wake.
Aristotle analinganisha mabadiliko ya tanzia na mabadiliko ya utanzu wa drama ya Kigiriki kwa ujumla.
Mabadiliko ya utanzu huu yanaanza na sherehe za matambiko yaliyonuiwa kumwabudu mungu Dionosia na kukamilika pale ambapo watunzi kama vile Sofokile wanatunga tamthilia zao.
Kwa mujibu wa maelezo ya Aristotle, tanzia ni maigizo ya matukio yenye ujumbe mzito yanayowasilishwa kwa lugha inayonawiri, yazindue hofu na huruma ili hatimaye maigizo hayo yaripue hisia za ndani kutoka katika nafsi za hadhira.