UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Methali na misemo ya Abagusii inayochipukia katika ngano – 2
Na ENOCK NYARIKI
SUALA lililojitokeza wazi katika mjadala wetu wa awali ni kuwa kuna mshabaha mkubwa baina ya baadhi ya misemo na methali za jamii ya Abagusii na ngano kutoka jamii hiyo hususan ngano za wanyama.
Tulieleza kuwa ili kuelewa maana ya ndani ya methali hizo ni muhimu kuelewa nususi ya visa ambavyo kwavyo zimehimiliwa. Tutaendelea kuiangazia mifano mingine mingi ya methali ambazo zimehimiliwa katika ngano.
Mong’ainwa tari monene
Kabla ya kuitafsiri methali hii na kuonyesha matumizi yake katika mazingira ya Abagusii ni muhimu kueleza kuwa miongoni mwa wanyama wanaojitokeza sana katika ngano za Abagusii ni ndovu na sungura.
Sungura na tembo wanapotumiwa kwenye ngano hizo masuala mawili muhimu hujitokeza: busara na upumbavu. Tembo husawiriwa kama mnyama ambaye huzitegemea nguvu zake katika kuyatekeleza mambo.
Mara nyingi, nguvu hizo ambazo haziambatani na maarifa huishia kumfeli na kumtia aibu mnyama huyo.
Licha ya kuwa sungura ni mnyama mdogo asiyekuwa na nguvu nyingi, husawiriwa kama mwenye maarifa kuliko wanyama wengine wengi, ndovu akiwa mmoja wa wanyama hao. Masimulizi yaliyomtumia sungura na ndovu au tembo aghalabu huonyesha jinsi sungura humdanganya tembo kutenda mambo fulani ambayo huishia kumnufaisha sungura au kumkejeli ndovu na kumfanya kuonekana mjinga.
Neno ‘mong’ainwa’ ni nomino kutokana na kitenzi ‘kong’ainwa’ chenye maana ya kudanganywa. Tafsiri ya methali hii ni kuwa “Hakuna aliye mkubwa sana hivi kwamba hawezi kudanganywa’’. Methali hii imehimiliwa katika kisa cha ndovu na sungura. Inasemekana kuwa siku moja, sungura alijisemea kimoyomoyo kwamba zilikuwa zimepita siku nyingi kabla ya kumdanganya mnyama. Kwa hivyo, aliondoka nyumbani kwake kwa kusudi la kumtafuta mnyama wa kumdanganya. Akiwa mbali, alimwona tembo akiwa ameketi kwenye kigoda nyumbani kwake. Sungura alimkabili tembo huku pumzi zikimwenda mbiombio na kumwuliza:
“Bwana Tembo, wewe hujasikia kuwa kimbunga kikali kinachowateka wanyama na kuwapeleka baharini kimetokea? Mimi mwenyewe nimenusurika kimbunga chenyewe kwa kutimua mbio.”
Atua moyo
Habari za sungura ziliuatua moyo wa tembo akamwuliza sungura kumsaidia. Sungura alimwambia aambue magome ya miti. Ndovu aliyaambua magome mengi ya miti na kumkabidhi sungura. Sungura alimweleza kuwa kwa kumfunga kwenye mti mkubwa uliosimama kwenye kiambo chake, ule upepo mkali usingeweza kumbeba na kumtosa baharini. Sungura alimfunga ndovu ki ki ki hivi kwamba licha ya ukubwa wake, ndovu asingeweza kujinasua kutoka kwenye kile kifungo. Ndovu alipoanza kutokwa na jasho, alimwuliza sungura:
“Bwana sungura, ninaona kimbunga kimekawia sana nami ninatokwa na jasho!”
“Hata mimi ninaona kwamba unatokwa na jasho,’’ Sungura alimjibu.
“Je, kimbunga chenyewe kitakuja?” ndovu aliuliza tena
“Hata mimi ninashangaa iwapo kweli kitakuja,’’ sungura alijibu kwa kejeli.
Hatimaye, sungura alimgeukia ndovu na kumwambia: “Bwana Tembo, Hakuna mtu yeyote aliye mkubwa hivi kwamba hawezi kudanganyika. Endelea kukaa hapo mpaka utakapomwona mnyama mwingine umwambie akufungue.’’
Kutokana na methali hii, linajitokeza funzo kubwa kwamba hapana mtu yeyote; awe mkubwa au mwenye mamlaka ambaye hawezi kuingia kwenye mtego wa ghiliba. Kwa mfano, wapo viongozi walioenziwa duniani lakini baada ya kulingwa na mambo madogomadogo waliishia kuporomoka.
Mfungamano uliopo baina ya methali na misemo ya jamii ya Abagusii una umuhimu mkubwa kwa yeyote anayejifunza jinsi ya kuzitumikiza semi hizo katika mazungumzo ya kila siku. Visa vya ngano za wanyama husaidia katika kuifanya methali au msemo wenyewe kukumbukika.
Aidha, wanyama ambao hutumiwa katika visa vyenyewe humwakilisha binadamu katika mazingira yake ya kawaida.
Alhasili, baadhi ya methali na misemo ya Kiswahili inaweza kukumbukika vyema kwa sababu imefungamana mno na ngano za kusisimua kutoka jamii hiyo. Methali nyingine zinafungamana na tajriba ya maisha ya wanajamii.
Jambo hili ni tofauti na methali za Kiswahili – nyingi ambazo zinatokana na mashairi kongwe. Kwa hivyo, uelewa wa maana za methali hizi ulitegemea sana uelewa wa matumizi yazo katika mashairi hayo.