UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Misingi ya uteuzi wa lugha ya kufundishia kwenye taasisi za elimu
Na MARY WANGARI
KUNA ulinganifu wa lugha ya Kiswahili na Kiingereza, lugha ya kufundishia katika ngazi zote za elimu, na lugha ya kufundishia masomo ya sayansi kulingana na tafitii zilizofanywa na Kamugisha na Mateng’e (2014).
Hata hivyo, hakuna utafiti ambao umefanyika wa moja kwa moja wa kuchunguza uhusiano baina ya kutotumika kwa lugha ya Kiswahili katika ufundishaji wa masomo katika shule za sekondari na kushindwa kwa wanafunzi kupata maarifa yaliyokusudiwa.
Kwa muda sasa, kumekuwa na hali ya kuelekezeana kidole cha lawama kuhusu lugha ya kufundishia elimu ya sekondari nchini.
Hii hasa ni kutokana na matokeo mabaya ya mitihani.
Kwa mintarafu hii, kumekuwa na mapendekezo yaliyotolewa hususan nchini Tanzania kuhusu haja ya kubadilisha lugha ya kufundishia iwe ni Kiswahili.
Ni vyema kufahamu kwamba lugha ya kufundishia ni chombo muhimu cha kubebea maarifa na stadi za mwanafunzi.
Aidha, changamoto kuu zinazoibuka baina ya wanafunzi na walimu wakati ambapo lugha ya kufundishia haieleweki vyema.
Tatizo kuu linalowafanya wanafunzi kukosa maarifa ya elimu katika shule za upili linatokana na kufundishwa kwa kutumia lugha wasiyo na umilisi wake.
Nyenzo muhimu
Mekacha (2000), anafafanua kwamba lugha ni nyenzo inayowezesha binadamu kufikiri, kuwasiliana, kuhifadhi na kurithisha maarifa.
Lugha ni nyenzo muhimu sana katika kufikiri.
Binadamu anapotumia lugha hufikiri kwanza, anapotaka kusema lolote hufikiria kwanza jambo la kusema namna ya kusema ili ujumbe aliokusudia kuuwasilisha ufikishwe kwa msikilizaji bila utata.
Hivyo basi, ni muhali kwa watu kufikiri bila kutumia lugha.
Mtu anapofundishwa katika lugha anayoifahamu vizuri huelewa anachofundishwa na huweza kueleza vyema alichojifunza kwa maneno yake na hata huweza kuwa na ugunduzi na uvumbuzi wake binafsi kwa vile hufikiria kwa kutumia lugha anayoielewa.
Msanjila na wenzake (2011) wanaeleza kwamba lugha ya kufundishia inapoteuliwa visivyo,huwa kunajitokeza vikwazo vingi ambavyo huathiri ufanisi katika kutoa, kubuni na kuendeleza maarifa.
Vikwazo hivyo ni wajifunzaji kuwa na mtazamo wa kutoipenda lugha hiyo,kuondoa juhudi ya kuijua na kuitumia, hivyo kukwamisha michakato ya ujenzi na utoaji wa maarifa muhimu kwa maendeleo ya jamii.
Baruapepe ya mwandishi: [email protected]