UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Msambao wa Kiswahili Uganda kabla ya Ukoloni
Na WANDERI KAMAU
HISTORIA ya maendeleo na usanifishaji wa Kiswahili pamoja na shughuli za Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki imezungumzia Tanzania na Kenya kuliko Uganda.
Labda sababu yake ni kwamba Kiswahili hakikupewa nafasi ya kuenea huko kama kilivyoenea Kenya na Tanzania.
Waganda walipinga kusomeshwa kwa Kiswahili katika shule zao wakati serikali ya kikoloni ilipokuwa tayari kukuza Kiswahili.
Wakati sera ya lugha ilipobadilika dhidi ya Kiswahili kote katika Afrika Mashariki, kuanzia mwaka 1950, Kiswahili kiliondolewa shuleni kwa kuwa hakikuwa tena lugha iliyotambulika katika shule za Uganda.
Katika makala hii, tutazamia sera ya lugha nchini Uganda, na jinsi ilivyokuwa ikibadilikabadilika, kufikia wakati Kiswahili kilipoondolewa shuleni.
Lugha zilizotumika kufunzia: Kuanzia mwaka wa 1925, suala la ni lugha zipi za Kiafrika ambazo zingetumika kusomesha katika madarasa ya mwanzo ya shule za msingi kote nchini Uganda, lilijadiliwa na serikali ya kikoloni.
Kwanza, uamuzi ulitolewa kwamba Kiganda kitumike katika eneo lote lililokuwa likitumia lugha za Kibantu.
Kisha, kamati ikaundwa kuchagua lugha mwafaka ya kutumia katika eneo la Kinailoti la mikoa ya Kaskazini ma Mashariki. Kamati hiyo pia ilipaswa kutayarisha tafsiri ya vitabu vya shule katika lugha zilizochaguliwa.
Kiingereza kingetumika kuanzia madarasa ya juu ya shule za msingi na kuendelea.
Mwaka 1926, Idara ya Elimu iliamua kutumia lugha tatu za Kiafrika katika shule za msingi.
Lugha hizo ni:
(a) Kiganda-Kilichotumiwa Buganda na sehemu ya Kaskazini ya Mkoa wa Mashariki.
(b) Kiacholi-Kilichotumika katika Mkoa wa Kaskazini
(c) Kiteso- Lugha iliyotumiwa katika shule za eneo la kati la Mkoa wa Kati.
Lugha nyingine zote za Kiafrika zilitambuliwa kuwa “lahaja ndogo” ambazo hazingetumiwa ila katika shule za malezi.
Kiwango cha elimu na vitabu: Kiwango hicho cha elimu kilisemekana kwamba hakikuhitaji vitabu na kwamba wanafunzi wengi hawakuendelea na masomo huko kwa kuwa walijiunga na shule za msingi ambako wangetumia moja kati ya lugha tatu zilizochaguliwa.
Kufikia mwaka 1927, vitabu kadhaa vilikuwa vimeandikwa kwa Kiganda, lakini kulikuwa na matatizo katika lugha nyingine mbili.
Gavana aliandika kumbukumbu kuhusu jambo hili, nalo baraza la kutoa maamuzi kuhusu elimu ya Waafrika likajadiliwa kwa kirefu. Matokeo yake ni kwamba, ilionekana ni vyema Kiacholi na Kiteso zitumiwe kama lugha za kusomeshea katika shule za msingi zilizokuwa katika maeneo hayo tu (ya Acholi na Teso).
Ilikubaliwa kwamba Kiswahili kisomeshwe kama somo katika shule za msingi na kwamba vitabu vya masomo kama vile Afya, Jiografia na Kilimo viandikwe kwa Kiswahili.
Uamuzi wa kusomesha Kiswahili ulifikiwa kwa sababu ya matatizo ambayo hayakuweza kutatuliwa wakati huo ya kutafsiri vitabu katika lugha za Kiteso na Kiacholi.
Sababu nyingine kubwa pia ni ile athari iliyotokana na kutumiwa kwa Kiswahili katika nchi za Kenya, Tanganyika na Zanzibar.
Ripoti ya Idara ya Elimu ya mwaka wa 1927 inaongeza kwamba, “Ama lugha hizi mbili si lugha za kwanza kwa watu wengi walio katika maeneo hayo, na kwao Kiswahili hakitakuwa shida kukielewa kuliko Kiteso na Kiacholi.”
Kwa hivyo, sera ya lugha iliruhusu kutumiwa kwa lugha za kwanza kusomesha wanafunzi wote katika miaka miwili ya kwanza ya masomo, kiwango ambacho vitabu havikuhitajika sana.
Baada ya kiwango hicho, wanafunzi walianza kujifunza Kiswahili, lugha ambayo iliwawezesha kusoma idadi kubwa ya vitabu ambavyo vilikuwa vikiongezeka kwa wingi.
Kiswahili kilitambuliwa kuwa lugha ya kipekee ambayo ingerahisisha mawasiliano katika nchi za Afrika Mashariki.
Kilitambuliwa kuwa lugha ya watu wengi ambayo ingetumiwa katika kuvichapisha vitabu vingi vya shule na vya fasihi. Gavana Gowers ambaye alikuwa Gavana wa Uganda wakati huo alikiunga mkono Kiswahili. Katika mwaka wa 1928, alipendekeza Kiswahili kitumiwe badala ya Kiganda kama lugha ya elimu na utalawa nchini Uganda (Ladefoged et al 1971: 88).
Sera hii ya kufunza lugha za kwanza zikifuatiwa na Kiswahili ilifuatwa katika mikoa yote ya Uganda ispokuwa mkoa wa Buganda.
Hapo mwanzoni, Kiswahili kilipingwa katika Mkoa wa Mashariki, lakini baadaye kilikubalika kuliko Kiganda, ambacho kingetumika ikiwa Kiswahili hakingetumika.