Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nadharia na aina za uhakiki katika Fasihi

February 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na WANDERI KAMAU

UHAKIKI huwa kiungo muhimu sana katika kazi za fasihi. Katika makala iliyopita, tuliangazia mwoano wa fasihi na uhakiki kwenye kazi za kubuni.

Makala ya leo yataangazia aina za uhakiki na matumizi yake katika kazi za fasihi:

Uhakiki sadfa: Huu ni uhakiki unaotokea bila sababu maalum. Kwa mfano, mtu anaweza kusoma makala fulani na kutoa maoni yake bila kutarajia.

Marejeo na bibliografia:

Ni namna ya uhakiki wenye lengo la kuieneza kazi fulani ya fasihi. Kazi ambazo hazijulikani katika aina hii ya uhakiki hutangazwa na kujulikana.

Uhariri: Ni uhakiki unaofanyiwa kitabu kabla ya kitabu chenyewe kuchapishwa.

Katika uhakiki wa aina hii, kitabu huweza kusahihishwa endapo kina makosa. Kwa haya, mhariri anaweza kutoa maoni yake kuhusu uzito na upungufu wa kazi inayoshughulikiwa.

Baada ya kiwango hiki cha uhakiki, mswada waweza kuchapishwa ama usichapishwe.

Mapitio: Aghalabu hufanyiwa kitabu kilichochapishwa hivi karibuni. Mapitio hukitangaza kitabu kwenye umma mkubwa wa wasomaji.

Ufundishaji: Unahusu ufafanuzi wa vitabu vya fasihi au masimulizi ya kifasihi. Uhakiki unaweza kufanywa darasani, redioni, mihadharani au katika miongozo ya uhakiki iliyotungwa na wahakiki. Katika ufundishaji wa fasihi, wanaofundisha wanatazamia kwamba:

(i) Wanaofundishwa watakumbuka wanayofundishwa pengine kwa ajili ya kupita mitihani

(ii) Tajriba, hisia, mielekeo na mitazamo ya wafundishwao itabadilika kutegemea mambo mapya wanayofundishwa.

(iii) Wafundishwao wataiga mitindo mipya ya uandishi na uhakiki na kuishilia kuwa waandishi au wahakiki.

Propaganda: Katika fasihi, huu ni uhakiki unaosambaza malengo yasiyohusiana moja kwa moja na fasihi. Uhakiki wa kipropaganda hufanywa kwa minajili ya kisiasa au kampeni nyinginezo. Uhakiki huu hujikita katika ujenzi wa taswira inayolenga kujenga hisia kuhusu jambo fulani. Huwa unatokea sana katika majukwaa ya kisiasa, ambapo baadhi ya waandishi huandika vitabu ya kuwasifu ama kuwakosoa wanasiasa wanaoshiriki kwenye zoezi husika la kisiasa. Uhakiki huu mara nyingi huwepo katika nchi zilizostawi kimaendeleo kama Amerika na Uingereza.

Upigaji marufuku: Ni uhakiki ambao hukusudia kupiga marufuku baadhi ya maandishi kwa kuwa maandishi hayo hayaoani na maono fulani katika jamii. Uhakiki huu pia hutumika na baadhi ya serikali kuzuia msambao wa machapisho ambayo yanaikashifu. Kwa mfano, riwaya ‘Rosa Mistika’ na tamthilia ‘Kaptura la Marx’ yake Profesa Euphrase Kazilahabi zilipigwa marufuku nchini Tanzania, mara tu baada ya kuchapishwa kwa msimamo wake mkali dhidi ya mfumo wa Ujamaa.

Uhakiki wa kitaalamu: Ni uhakiki ambao hufanywa na wataalamu, wasomi na wanachuo kwa kufuata kanuni maalum. Uhakiki unaotegemewa utatolewa tu, iwapo mhakiki atatumia mihimili ya kinadharia inayotangamana na uamuzi unaofanywa.

Uhakiki wa aina hii huithamini kazi ya fasihi kivyake na katika muktadha wa kazi za fasihi nyinginezo.

Nadharia za uhakiki wa fasihi

Nadharia za uhakiki wa fasihi ni miongozo inayomsaidia msomaji wa kazi husika ya fasihi kwa muhjibu wa vigezo vilivyowekwa au vinavyozalika kutokana na uchunguzi wa aina mbalimbali za fasihi (Eagleton, 1983, Njogu & Chimerah, 1999).

Aina za Nadharia: Aina za nadharia zinatokana na jinsi nadharia hizo zilivyoundwa.

(a) Nadharia asilia: Hii ni nadharia isiyotokana na nadharia nyingine yoyote. Nadharia asilia inajitosheleza na haina uhusiano wa moja kwa moja na nadharia nyingine. Tunapozungumzia nadharia ya uhalisia, tuna maana ya jinsi ya kuzitunga na kuzihakiki kazi maalum za fasihi.

(b) Nadharia nyambuaji: Ni nadharia ambayo imetokana na unyambuaji wa nadharia iliyokuwepo hapo awali. Kwa hivyo, nadharia ya aina hii ni kimelea cha nadharia iliyoitangulia. Kwa mfano, vigezo vinavyoubainisha urasimi wa Kimagharibi ni uigo na ufuasi wa sheria. Urasimi mpya ni kimelea cha urasimi mkongwe.

(c) Nadharia changamano: Ni nadharia ambayo imeundwa kutokana na nadharia mbili au zaidi. Kuna nadharia inayoitwa uhalisia. Pia, kuna mfumo wa kuzalisha mali ambao unaitwa ujamaa. Uhalisia ni nadharia ya kutunga na kuhakiki kazi za fasihi inayonuia kuionyesha jamii katika uyakinifu wake. Nao ujamaa ni mfumo unaolenga kuwasawazisha, kwa kiwango kikubwa, walimwengu katika mahusiano yao na njia za kuzalisha mali.

Tutaendeleza nadharia hizi katika makala yajayo.

 

[email protected]