Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Othografia katika Kiswahili: Sehemu ya Kwanza

January 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na WANDERI KAMAU

KATIKA utangulizi wa kitabu ‘A Handbook of the Swahili Language’, Askofu Adam Steere alijadili suala la tahajia au hati za maandishi ya Kiswahili kwa undani.

Karibu maandishi yote ya Kiswahili kabla ya wakati wake yalikuwa yameandikwa kwa hati za Kiarabu. Mengi kati ya maandishi hayo yalikuwa ni tenzi na mashairi ya kidini na mambo ya kawaida yaliyoandikwa kwa lahaja ya kishairi ya Kaskazini, ambayo Steere alishuku iwapo ilieleweka na watu wengi.

Ingawa Kiswahili cha wakati wake kilikuwa kikitumiwa katika kuandikiana barua, Steere anasema kwamba barua kama hizo zilianzia na salamu kwa Kiarabu na pia maneno na vifungu vya maneno ya Kiarabu.

Tathmini ya Steere

Stere alitambua kwamba hati za Kiarabu hazifai kuandikia Kiswahili kwa sababu lugha ya Kiswahili inazo irabu tano ikilinganishwa na irabu tatu za Kiarabu. Kuhusu konsonanti, hati za Kiarabu zina upungufu wa konsnanti za ‘g’, ‘p’, na ‘v’. Steere aliandika hivi:

“Kwa hivyo, Waswahili wanalazimika kuandika ‘ba’, ‘f’ au ‘p’ wakikusudia kuandika ‘mb’ au ‘b’; wanaandika ‘’ghai’ badala ya ‘g’, ‘ng’, ‘ng’, ‘fa’ badala ya ‘v’, ‘mv’ na ‘f’, ‘ya’ badala ‘ny’ na ‘y; ‘shin’ badala ya ‘ch’ na ‘sh ; pia wanaiacha ‘n’ inapozitanguia d, j,y na z.”(Steereb 1870:5).

Kwa hivyo, ni wazi kwamba hati za Kiarabu hazifai na hazitoshelezi maandishi ya Kiswahili kwa sababu ya kutatanisha. Ili kuonyesha matatizo ya hati hizi, Steere anaandika hivi:

“Nilipokuwa Zanzibar, kulikuwa na barua iliyotoka Kilwa kuhusu vita. Barua ilitaja kwamba mtu mmoja kati ya wale waliopigana alikuwa amekufa au amevuka na hakuna aliyeweza kusema kile kilchokuwa kimetendeka. Konsonanti mbili za mwisho zilikuwa ‘fa’ na ‘gaf’ zikiwa na vitone vitatu juu yake. Ikiwa vitone viwili vilikuwa vya herufi ya kwanza, mtu huyo alikuwa amekufa. Ikiwa vitone viwili vilikuwa vya herufi ya pili, alikuwa hai, lakini vitone hivyo vilikuwa katikati hivi kwamba hakuna aliyeweza kuvigawanya. Iwapo Kiarabu kingekuwa na herufi ‘v’, ingekuwa wazi (Steere 1870:6).

Hati za Kiarabu

Zikilinganishwa na hati za Kiarabu, hati za Kirumi hazileti matatizo yoyote katika kuandika Kiswahili. Sababu yake ni kwamba wasomi wengi wa Kiswahili waliokuja baada ya Krapf na Steere waliamua kutumia hati za Kirumi walizokuwa wamezizoea baada ya hati za Kiarabu zilizokuwa zikitumika kuandika Kiswahili.

Mara nyingi, maneno na mizani katika Kiarabu huishia kwa konsonanti. Hili pia ni jambo lingine linalozifanya haati za Kiarabu zisifae katika kukiandika Kiswahili.

Dhehebu la UMCA lilichapisha vitabu kwa kufuata mtindo uliotumiwa kuchapisha vitabu vya Steere. Wamisheni wa Kizungu walifanana na waanzilishi wa uchunguzi wa Kiswahili kwa kuwa ilikuwa rahisi kwao kutumia hati za Kirumi badala ya zile za Kiarabu.

Mkutano wa Dar es Salaam wa mwaka 1925 uliamua kutozitumia hati za Kiarabu pamoja na konsonanti za Kiarabu kama vile ‘kh’.

Uamuzi huu wa mwaka 1925 uliwakasirisha wengi, ikiwa ni pamoja na gazeti la Mombasa, Al-Isiah, kama tutakavyojadili.

Profesa Carl Meinhof alipohudhuria mkutano wa Mombasa wa mwaka 1928, waliohudhuria walikuwa na nafasi ya kushauriana naye kuhusu othografia ya Kiswahili. Meinhof alipendekeza ‘c’ itumiwe badala ya ‘ch’.

Badala ya kutumia alama tatu za maandishi (ng) kusimamia sauti moja, alipendekeza kuwa ‘n’ yenye mkia itumiwe kama ilivyo katika maandishi ya kifonetiki.

Lakini mashauri haya ya Meinhof hayakukubaliwa. Wasomi wa Kiswahili wakati huo walijiona kuwa sahihi, na kwamba mapendekezo ya Meinhof yalifaa tu katika maandishi ya kifonetiki katika isimu lakini hayakufaa katka othografia ya kawaida ya Kiswahili.

Katika majadiliano yao, waliona kwamba ingekuwanvigumu kupiga taipu ‘n’ yenye mkia. Tatizo hili lingetatuliwa hapo mwanzoni kwa kupiga taipu herufi ‘j’ juu ya ‘n’ wakingojea kurekebisha kwa mashine na kwa hivyon tatizo la kuandika sauti ya kwanza ya neno ‘ng’ombe’ kwa sauti mbili na alama (ng’) lingali linaendelea.

Upungufu mwingine wa othografia ya Kiswahili unaoweza kutajwa hapa ni kule kukosa kutofautisha konsonanti za kipua (nazali) ambazo ni mizani ‘m’ na ‘n’ za kwanza katika maneno ‘mmea’ na ‘nne.’

 

[email protected]