UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Sifa zinazofanya isimu kuwa sayansi ya lugha
Na CHRIS ADUNGO
KATIKA hali ya kawaida, utakuta kwamba ni mazoea kwa mtu kusema “mimi ninajua lugha” au “hawa hawajui lugha”.
Lakini je, ni nini hasa maana ya kujua lugha?
Kujua lugha ni ule uwezo wa kutambua na kubainisha sauti pekee za lugha, kujua namna sauti hizo zinavyoungana na kuunda maumbo ya maneno, kujua namna maneno yanavyoweza kuundwa na kugawanywa, kujua jinsi maneno yanavyounga na kutengeneza tungo, kujua maana ya maneno na misemo mbalimbali ya lugha husika na kuweza kutumia lugha hiyo katika miktadha tofauti ya mawasiliano.
Kwa maelezo hayo, tutakuwa tumejibu swali la kuwa kujua lugha ni nini. Swali la mjua lugha ni nani hapa linakuwa si tata tena kwani mtu anayekuwa na sifa zote hizo za hapo juu, tutasema ni mjua lugha.
Hoja kuwa lugha ni mfumo, inamaanisha kuwa lugha ina muundo unaohusisha viambajengo mbalimbali. Viambajengo au vipashio hivi ni sauti, neno na sentensi. Kwa pamoja, vipashio hivi hushirikiana kuunda tungo zenye maana na kama tungo hizo hazina maana au kama haziwasilishi ujumbe wowote, basi tunasema haziwi lugha.
Viambajengo hivi, hushughulikiwa na tanzu tofautitofauti za isimu muundo. Tanzu hizi ni fonetiki na fonolojia ambazo hushughulikia sauti za lugha, mofolojia ambayo hushughulikia maumbo ya maneno na jinsi lugha inavyounda maneno, sintaksia ambayo hushughulikia namna sentensi zinavyoundwa na kanuni zinazotawala uundwaji wake na semantiki ambayo hushughulikia maana katika viwango vyote vya lugha.
Kwa ujumla, tanzu hizi zote zinahusiana kwa ukaribu, zinashirikiana na kukamilishana.
Fasili iliyozoeleka na pengine inakubalika na wataalamu wengi wa lugha ni kuwa isimu ni elimu ya sayansi ya lugha. Ni uchunguzi wa kisayansi na wa kimantiki kuhusu vipengele na sifa mbalimbali za lugha. Swali ambalo tunaweza kujiuliza ni kwamba; “Kwa nini isimu ni sayansi?”
Verma et al (1989:29), wanasema kuwa isimu ni sayansi kwa kuwa hufuata na kutumia mbinu za kimsingi za utafiti wa kisayansi. Mbinu hizo ni kama vile uchunguzi uliodhibitiwa, uundaji wa mabunio, uchanganuzi, ujumlishi, utabiri, urekebishaji au ukataaji wa mabunio na majaribio na uthibitishaji.
Kwa hatua hizi, tunathubutu kusema kuwa isimu haichunguzi lugha kiholela tu, bali kwa mwelekeo maalumu. Katika kuchunguza lugha, wanaisimu hutumia misingi ya kisayansi kama zifanyavyo sayansi nyingine. Misingi hii ni kama vile:
Uwazi
Dhana hii inamaanisha kuwa masuala katika isimu huelezwa kwa udhahiri usio na utata wowote. Hoja huelezwa bila kuleta vuguvugu lolote la kimaana kinyume na mawasiliano yasiyo ya kisayansi.
Utaratibu
Habwe na Karanja (2003) wanaeleza kuwa utaratibu na uwazi ni dhana zinazokaribiana sana. Bila kuwa na uwazi, ni vigumu kuwa na utaratibu na kinyume chake. Utaratibu ni kufanya jambo kwa mpangilio mzuri unaobainika. Utaratibu unaweza kuhusisha wakati, idadi, umuhimu na hata ukubwa.
Urazini
Habwe na Karanja (2003) wanasema kuwa, katika kushughulikia na kuelewa lugha, mwanaisimu hujikuta akiwa na kazi ya kutimiza majukumu ya kueleza maana na asili ya lugha, kuchambua muundo wa lugha, kueleza uhusiano kati ya lugha na asasi nyingine za mwanadamu na kuibua nadharia mbalimbali za lugha.
Umilisi Na Utendaji
Umilisi ni ujuzi alionao mjua lugha kuhusu lugha yake. Ni ujuzi alionao mjua lugha ambao upo katika ubongo wake. Ujuzi huo huhusu kanuni zinazotawala lugha hiyo husika. Ujuzi huu humwezesha kutambua sentensi sahihi, zisizo sahihi na kupambanua sententi zenye utata. Ujuzi huo humwezeha pia kupuuza makosa ya kiutendaji katika mazungumzo kama vile kuteleza kwa ulimi, kukatisha sentensi n.k.
Utendaji ni kile asemacho mjua lugha katika muktadha wa mawasiliano ikiwa ni pamoja na makosa ya kiutendaji ya bahati mbaya na yale ya kukusudiwa. Ni udhihirikaji wa ujuzi wa lugha alionao mjua lugha.
Uamilifu Na Urasmi
Uamilifu au utumizi ni elimu inayohusu muundo wa lugha kwa kurejelea kazi zake za kijamii katika mawasiliano. Inamchukulia mtu binafsi kama kiumbe-jamii na kuchunguza namna anavyojifunza lugha na kuitumia katika mawasiliano na wanajamii wenzake.
Urasmi ni elimu ya maumbo dhahania ya lugha na mahusiano yake ya ndani. Huzingatia maumbo ya lugha kama uthibitisho wa kimalimwengu bila kuzingatia namna jamii inavyowasiliana.
Uelezi Na Uelekezi
Uelezi ni mtazamo ambao huelezea ukweli wa lugha jinsi ilivyo na inavyotumika na jamii-lugha husika. Si namna lugha inavyotakiwa kutumika. Isimu elezi haiweki kanuni ngumu au sheria ngumu zozote zinazotokana na mawazo ya mtu kuhusu lugha fulani, bali huelezea lugha kwa kuangalia namna lugha hiyo inavyojidhihirisha yenyewe. Huelezea sheria na kanuni ambazo mzungumzaji mzawa ameziweka kichwani na zinazoakisi uwezo wake wa lugha.
Kwa kifupi, haielezi wala kuagiza namna mtu anavyotakiwa kutumia lugha, bali jinsi lugha ilivyo na inavyotumika miongoni mwa wamilisi wa lugha hiyo.
Uelekezi ni mtazamo unaojaribu kuweka bayana kanuni za usahihi wa namna watu wanavyotakiwa kutumia lugha katika mawasiliano ya mara kwa mara.
Kanuni Za Usahihi
Kwa mujibu wa Joos (1961), lugha rasmi haina madakizo au mapambo na aghalabu inahusishwa na kujitambulisha kwa wageni. Hujiepusha na urudiaji isipokuwa tu pale ambapo msisitizo unahitajika.
Katika kukwepa udondoshaji, lugha rasmi huzingatia kanuni zote za kisarufi na usahihi. Lugha rasmi ni aina ya mawasiliano yanayotumika katika mazungumzo na maandishi yaliyo rasmi kama vile kwenye mazingira ya afisini, mahakamani, uwasilishaji wa maazimio, maagizo, miongozo, nyaraka muhimu za kiserikali, hati za idara mbalimbali, matangazo ya kisheria au makala ya kitaaluma.
Katika matumizi ya lugha hii, usahili na ukweli wa mambo yanayojadiliwa ni kigezo muhimu sana kuzingatiwa.
Mfumo wa lugha unaotumika katika matini ya kisheria kwa mfano, ni ule unaosisitiza kabisa usahili wa lugha ili kujaribu kuzuia ufafanuzi unaogongana na sheria hizo. Aidha, mawasiliano katika shughuli rasmi hayafanywi ovyo tu bila ya kufuata mpangilio maalum wa matukio. Badala yake, huzingatia mtiririko maalum unaokusudia kuleta ukamilifu wa maana.
Lugha huhusisha matumizi ya zana za kiisimu zinazofanana au kulingana katika kuelezea mambo.
Mazungumzo yoyote rasmi hupangwa kabla ya kuwasilishwa ili kuepuka uradidi na urejeshi mwingi. Ni mpangilio huu wa hali ya juu ndio unaoipa lugha hii jina lake. Kuna matumizi ya istilahi maalum zinazohusu masuala ya afisini au kidiplomasia. Aidha, vyeo au nyadhifa za wahusika mbalimbali hutajwa.
Huzingatia uwazi kwa kuepuka matumizi ya misimu, nahau, mafumbo au lahaja. Kwa ujumla, lugha rasmi ni namna ya mawasiliano katika nyanja za utawala, uendeshaji wa uongozi na masuala ya kisheria.