Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Tathmini ya vitabu vya kufundishia Kiswahili kwa wageni

June 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MARY WANGARI

SUALA la uteuzi wa vitabu vya kufundishia huzua changamoto kutokana na hali ya kutofautiana kwa malengo ya wadau husika ambao ni wanafunzi, taasisi, waajiri, walimu na wazazi au walezi.

Kutofautiana huko kwa malengo ya wadau kunajidhihirisha kwa njia zifuatazo:

Kutofautiana kwa malengo ya mwanafunzi kwa mfano kutokana na viwango tofauti vya wanafunzi.

Tofauti zinazotokana na kitabia, kiuchumi, kiuelewa, kiutamaduni na hata kiumilisi.

Tofauti katika viwango vya wanafunzi mathalani kiwango cha kati, kiwango cha juu na kadhalika.

Kutofautiana kimaamuzi. Kwa mfano, taasisi moja tu ihusike katika uandaaji wa vitabu vya kufundishia mathalani Wizara ya Elimu.

Tofauti katika uzingatizi tofauti wa vitabu mathalani bei, mwonekano, na hata upatikanaji wake.

 

Namna ya kukabiliana na changamoto hizo

Shughuli ya kuteua vitabu vya ufundishaji hukumbwa na changamoto chungu nzima.

Hata hivyo, kuna mbinu mbalimbali zinazoweza kutumiwa na wadau husika katika juhudi za kusuluhisha changamoto hizo.

Changamoto hizo zinaweza kukabiliwa kwa njia zifuatazo:

Malengo ya kozi ni sharti yaangaliwe

Bainisha wanafunzi wanaolengwa

Mkabala utakaotumia kufundishia

Stadi za lugha. Je kitabu kimekidhi stadi zote za lugha?

Ubora wa mazoezi yaliyotolewa ndani ya kitabu

Mfuatano wa masomo/mada. Je, ni mgumu au rahisi?

Msamiati uliotumika.

Hali ya jumla ya kiisimu jamii. Je, kitabu kimetumia lahaja, lugha rasmi, na vigezo vya kiutamaduni?

Muundo mzima wa kitabu. Chapa yake ni ndogo au kubwa?

Sifa za kitabu bora cha kufundishia lugha kwa wageni

Kila somo/kitabu kiwe na lengo mahususi la kumsaidia mwanafunzi kuwasiliana.

Kila kitabu kiwe na matini ya lugha kama inayozungumzwa na wazawa.

Kila kitabu kiwe na kielelezo cha mazingira halisi. Kwa mfano, salamu.

Msamiati na sarufi kukidhi matakwa ya wanafunzi.

Matumizi wa vielelezo halisi kama vile picha, magazeti, tangazo, kadi na kadhalika.

Kila kitabu lazima kiorodheshe sauti zilizo katika lugha husika ili aweze kuzielewa.