UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Uandishi kama sanaa ya mawasiliano
Na CHRIS ADUNGO
KATIKA makala ya awali, tulisisitiza kuwa kuna matatizo ambayo ni ya kipekee kwa waandishi chipukizi, na kwamba matatizo hayo hutoweka mara baada ya mwandishi kufaulu kuchapisha, ama kuwa na mizizi, au kukomaa katika sanaa ya utunzi.
Lakini hulka ya uumbaji inafutilia mbali wazo hili kwani kila zoezi la uumbaji ni kitendo kipya; hivyo matatizo ya aina fulani yatajitokeza daima na kuwaathiri waandishi wa viwango vyote – chipukizi na aliyepevuka.
Ni wazi, basi, tofauti kati ya mwandishi chipukizi na yule aliyekomaa imo katika namna mwandishi anavyoyashughulikia matatizo yahusuyo uandishi wa fasihi, katika ujuzi wake wa kutumia vyombo vya kazi yake anapoumba.
Baadhi yao hushindwa katika jambo hili na kubakia chipukizi daima, huku wengine wakifaulu na kukomaa. Makala haya yanajihusisha na waandishi wa riwaya pekee na yatajadili matatizo ya waandishi chipukizi katika kiwango cha matatizo yasiyoisha ya kitendo cha uumbaji, yaani, matatizo yahusianayo na maumbile ya sanaa na dhima yake katika mawasiliano.
Sanaa ni mawasiliano. Kuandika ni kuwasiliana, ni itikadi, imani, hisia nzito za mikanganyiko, huzuni au furaha, kupinga yale yasiyo ya haki, au kuyajaribu katika vitendo mawazo mapya yajitokezayo kichwani.
Ari ya kuwasiliana na kutoa habari ni tabia iliyokita katika maumbile ya wanadamu, na ni chimbuko la furaha, utambuzi na ukuaji wa nafsi. Ari ya kuwasiliana ni tofauti na uwezo wa kuwasiliana.
UTARATIBU
Mawasiliano ya dhati yanahitaji utaratibu wa aina yake; yanahitaji utumizi wa lugha na mbinu zake, kama vile ishara, picha, tamathali, n.k, ambazo zinafahamika kwa mwandishi pamoja na wale akusudiao kuwasiliana nao.
Msamiati wa lugha hii unatokana na maisha ya kila siku ya mwandishi, tangu utotoni wakati mazingira yanajitokeza kwake kihisia, na kutokana na mwongozo wa watu wazima na wazee wa jamii.
Katika ngazi hii ya awali, habari na maarifa hutunzwa katika ubongo wa mtu atakayekuwa mwandishi, ubongo ambao daima unajishughulisha. Mwandishi hupata maarifa kutokana na mazingira yake yanayomkuza na huyatumia katika kupanga mawazo yake.
Suala la utaratibu je? Vipi mwandishi anaufikia utaratibu katika kazi ya fasihi ili kuwasiliana? Kwanza yabidi tueleze maana ya utaratibu huu. Kwanza yafaa tuelewe kuwa hadithi ya kubuni si kiini, wahusika na mazingira tu, bali ni ujumla wa mambo yote haya katika mwelekeo wa hadithi nzima yasababishwayo na mahitilafiano, yakuzwayo hadi upeo na hatimaye kufikia mwisho na kutanzuliwa.
Huu utaratibu ndio uipayo kazi ya kubuni uzito wake na nguvu yake, na wakati uo huo kuitofautisha kazi ya sanaa na maisha halisi, japokuwa kuna kulandana kwa aina fulani. Pindi mwandishi aufikiapo utaratibu huu katika kazi ya riwaya, umaana wa matendo na kubadilika kwa wahusika hueleweka na kwa hiyo maana ya kazi hiyo kujitokeza.
Mtu asomaye hadithi hiyo ataweza kuwatazama wahusika katika mienendo yao kama vile ni watu halisi, msomaji atafuatilia matendo yao na kujitambulisha nao, au kutokubaliana nao au hata kuwahukumu.
HUKUMU
Hiki kitendo cha msomaji cha kujihusisha, kutokubaliana au kuhukumu mhusika katika riwaya ndicho kimwezeshacho kujifunza na kushiriki kimawazo katika mwenendo wa mabadiliko.
Fasihi, kwa hiyo, ina uwezo wa kutupa kile ambacho maisha halisi yasingetupa kirahisi, au yangetupa kwa gharama kubwa.
Waandishi wote hutamani kufaulu katika jambo hili na kutoa kazi bora. Hapo ndipo ulipo ugumu kwa waandishi chipukizi walio wengi. Suala hili lina maana gani kwa waandishi chipukizi?
Jambo mojawapo la msingi na muhimu kwa mwandishi yeyote ni uwezo wa kuhisi juu ya mambo yajitokezayo katika mazingira (watu, hali, matukio, n.k.); upeo wa hali ya juu wa kuyachunguza maisha, kuyatafakari na kuyatafsiri (hata kama si kwa usahihi wakati mwingine). Mwandishi anahitaji ujuzi wa kumwezesha kuyatafsiri kikamilifu yale ayafahamuyo kisanaa.
Anahitaji kuelewa, kwa mfano, kwamba bila msomaji kuwa na hamu ya kazi yake, kazi hiyo haitasomwa hata kama jambo lizungumzwalo ni muhimu sana.
Kwa hiyo, kuna umuhimu wa kuelewa nini kitakikanacho katika kubuni hadithi – vitu kama kiini cha hadithi, wahusika, mazingira; jinsi hitilafu zijitokezavyo, upeo na suluhisho; ufundi wa kuchagua kwa makini yale yaliyo muhimu; sauti hai na ulinganifu wa mwendo unaowafanya wasomaji kupata uzoefu kihisia wakati wanaposoma. Mtindo, herufi, sarufi na alama za vituo huiongezea uzuri kazi iliyoandikwa.
MTINDO
Mtindo humwezesha msomaji kupata maana ya kitu kizima na si neno moja moja. Kwa maneno mengine, kile akifahamucho mwandishi (mtazamo wake wa maisha) lazima kioanishwe vizuri katika kazi yake ya kubuni na kile riwaya yake inachojaribu kukisema. Busara, kipawa na ufundi ni muhimu kwa waandishi wote, na hususan kwa waandishi wachanga ambao inabidi wajitahidi kupita kiasi.
Hadi kufikia hapa, tunaweza kuelewa kwa nini waandishi wengi chipukizi hukwama katika hatua za mwanzo. Si kwa sababu hawajui la kusema, au hawana msamiati wa kutosha, bali ni kwamba kunahitajika ujuzi na maarifa ya msingi ya maumbile ya fasihi pamoja na njia maalumu ya kubuni.