UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Uhusika wa mhusika katika kazi za fasihi
Na MARY WANGARI
WAHUSIKA katika hadithi ni mhimili mkubwa katika vipera vya fasihi: fasihi andishi na fasihi simulizi.
Kulingana na Msokile (1992), akiwanukuu Penina Muhando na Ndyanao Balisdya, wahusika wanaweza kuumbwa kinafsia, kiakili na kimwili.
Kutokana na ujenzi wa aina hii, mhusika huonyesha wasifu wake wa ndani na nje au anaweza kuonyesha mabadiliko yake kila anapokutana na mazingira tofauti.
Mhusika pia anaweza kuonyesha mabadiliko katika uhalisia wake kwa kuzingatia nguvu zinazomzunguka kama vile utamaduni, siasa, uchumi na kadhalika.
Kwa upande wake Wamitila (2008:369), wahusika ni nyenzo kuu katika fasihi kwa sababu ndio dira ya matukio na matendo yanayopatikana katika kazi ya kifasihi inayohusika.
Ni vyema kuelewa kuwa mtazamo wa dhana ya wahusika huweza kutofautiana kutegemea mkabala anaouchukua mhakiki na nadharia ya fasihi inayohusika.
Kwa nini mhusika?
Cha msingi ni kwamba, mhusika ni mtendaji katika kazi ya kifasihi na huwa kielelezo cha viumbe wanaopatikana ulimwenguni.
Hata hivyo, si lazima sifa zote za mhusika zifungamane moja kwa moja na za binadamu na ndiposa jina mhusika hutumiwa badala ya kiumbe, mti au mtu.
Isitoshe, mwelekeo wa kuwahusisha wahusika wa kifasihi na binadamu wanaopatikana katika hali halisi huathiri kwa kiasi fulani matarajio ya usawiri wa uhusika.
Upo mwelekeo mkubwa wa kuwachunguza wahusika wa kifasihi kwa kuwafungamanisha na binadamu halisi na hata, labda kutokana na athari za mielekeo ya kimaadili ambapo kwa mfano, wahusika wakuu hutarajiwa kuwa na maadili fulani.
Hata hivyo, Kundera (2007) anatoa hoja kwamba wahusika wa kifasihi hawahitaji kupendwa kutokana na maadili yao bali kinachotakiwa ni kuwaelewa.
Aidha, anaeleza anafafanua kuwa matendo yanayopatikana katika kazi ya kifasihi huhusishwa na wahusika na ni nguzo kuu ya dhamira na maudhui yanavyoendelezwa katika kazi husika.
Kwa upande wao wataalam Njogu na Chimerah (1999:45), wanafafanua wahusika kama viumbe wa sanaa wanaobuniwa kutokana na mazingira ya msanii yanayoweza kuwa ama kijiografia, kihistoria, kijamii, kitamaduni au ya kisiasa.
Wahusika vilevile hujadiliwa kwa namna wanavyoingiliana na dhamira sifa inayojitokeza kutokana na hulka yao.
Kwa jumla, wahusika wa aina yoyote wawe watu au viumbe hurejelea na huakisi sifa na tabia za binadamu katika jamii husika.
Wasiliana na mwandishi kupitia baruapepe: [email protected]
Marejeo
Njogu, K. na Chimerra, R. (1999). Ufundishaji wa Fasishi: Nadharia na mbinu. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
Syambo, K. Mazrui (1992). Uchambuzi wa Fasihi. Nairobi: East African Educational Publishers.